Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kujadiliana kwa upendo wa hali ya juu lakini na wivu wa maendeleo kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru sana wajumbe wa Kamati yetu ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati tunajadiliana jambo hili kwenye kamati, tuliifanya kazi hii kwa uzalendo wa hali ya juu na Kamati yetu wametushauri tukiwa ndani ya kamati na tumechukua ushauri wao na tutaendelea kuufanyia kazi kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu imesema hapa ikatoa maoni na ushauri kwa Serikali wakati wakiwasilisha taarifa yetu hapa ili ilipowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wetu mdogo wangu Mheshimiwa Mariam Ditopile. Niwashukuru sana na nikushukuru mno kwa usomaji mzuri na nia uliyoitanganza. Sisi kama Wizara tumekuelewa, na naamini na wajumbe wote wa Kamati tumekuelewa, basi tunakwenda kutenda jambao nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Kihenzile kwa kutuongoza vyema kwenye Kamati yetu, tangu ilipokuwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, na hata ilipobadilioshwa na kuwa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi aliifanya kazi yake kwa uzalendo wa hali ya juu na kwa weledi wa hali ya juu, na hatimaye Mheshimiwa Rais ameweza kumteua na kuwa Naibu Waziri, nampongeza sana. Sisi kama Wizara tunatambua kazi yake njema aliyoifanya kwetu kwa jinsi aliyotushauri. Kama Wizara mawazo yake tutaendelea kuyafanyia kazi pamoja na wajumbe wote wa Kamati yetu. Hakika sisi kama Wizara tunawashukuru sana na tunatambua mchango wenu mwema wa utendaji wa Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru wewe kwa jinsi ulivyoliongoza Bunge letu tukufu siku hii ya leo na siku zote ambazo umekuwa ukituongoza kwenye majadiliano ndani ya Bunge letu hili. Nikushukuru na nikupongeze sana. Tumeyapokea yote yaliyosemwa na Waheshimiwa Wabunge, tumepokea hoja, ushauri pamoja na maelekezo kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge nane waliochangia jambo letu hili ambalo tumeliweka mezani. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuweza kutushauri sisi kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati nawasilisha hoja hii pale mwanzoni, kwamba tayari Serikali yetu ilikuwa inaendelea kushiriki kwenye majadiliano, kwenye utekelezaji wa itifaki hii. Tulikuwa tunashiriki kwa sababu sisi ni wajumbe kwenye Jumuiya yetu ya Maenedeleo Kusini mwa Afrika, lakini tulikuwa hatuna uwezo wa kwenda kutekeleza kile ambacho kilikuwa kinajadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo leo hii Waheshimiwa Wabunge tumelileta mbele yenu, tunawaomba sana muweze kuridhia. Na niwashukuru Wabunge wote nane mliochangia, mmekubali kuridhia itifaki hii ili kama Taifa sasa twende kunufaika nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya ya awali naomba nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utayari wake wa kuona Taifa letu linashiriki kule duniani kupitia diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kushirirki vizuri kule duniani kama na majirani zako bado hamjajiimarisha ushirikiano hasa ushirikiano huu wa kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu alituelekeza na ametoa maelekezo kwa itifaki zetu zote zinazohusu biashara kwenye ukanda wetu, zote ziweze kufanyiwa kazi na tuziridhie. Ni kwa sababu ya utayari wake, wa kuona Watanzania wananufaika na uwepo wa Taifa letu na uwepo wa benefits zote tulizonzo ndani ya Taifa letu, comparative advantage tuliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema na amekuwa akisema siku zote, tusiendelee kuongelea comparative advantages tulizonazo kama Taifa tu na badala yake lazima tuzitumie hizo sasa kunufaisha Taifa letu. Na moja ya utekelezaji wake huu ni kuletwa kwa Itifaki hii leo ya Biashara ya huduma, ili Watanzania washiriki kwa pamoja kunufaika na uwepo wa Taifa letu kijiografia hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, amejibu baadhi ya hoja mabazo Waheshimiwa Wabunge wamezisema, na mimi wala siwezi kuzisema zote. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba hoja zote mlizozitoa zinatuwezesha sisi tunapoingia kwenye majadiliano kule kwenye utekelezaji wa Itifaki hii kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, tuweze kupeleka hoja za wananchi kupitia nyinyi Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo sina sababu ya kuzijibu zote hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri wangu amesema, kwa hiyo mimi nawashukuru sana mmetupa nguvu mmetupa hoja ya Kwenda kuendeleea kuzisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizisemee mbili tu. Hoja ya kwanza niliyoulizwa ni kwamba, kwa nini tumechukua zaidi ya miaka kumi na tatu hadi leo ndio tunaleta Itifaki hii ndani ya Bunge letu tukufu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge nilianza kulijibu jambo hili tukiwa tunajadiliana hapa. Moja ya sababu ambayo tumechukua muda huu mrefu ilikuwa ni kuwaandaa Watanzania ili tunapoingia waweze kunufaika kwa asilimia kubwa na kuingia kwetu kwenye utekelezaji wa Itifaki hii. Serikali yetu baada ya Mheshimiwa Rais wetu kusaini mwaka 2012 tulitafuta Mshauri Mwelekezi ambaye ni Mtanzania, akazunguka kwenye sekta zote akakaa na wafanyabiashara wetu na hata sekta hizi ambazo tumeweza sasa kuingia tumeona sekta za mwanzo sita ilikuwa zimetoka kwa wadau wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Watanzania ambayo ni sekta binafsi imeshirikishwa kwa asilimia 100. Kwa hiyo hii ilikuwa sababu ya kwanza kwa nini tangu mwaka 2012 hatujaleta itifakii hii ndani ya Bunge letu tukufu, tulikuwa tunawaandaa Watanzania ili waweze kunufaika na itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili lilosababisha tuchukue kipindi chote hiki ni kuandaa miundombinu wezeshi ya kwenda kunufaika na itifaki hii ya Azimio la Biashara ya Huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeandaa Taifa letu miundombinu ya barabara. Taifa letu sasa linaunganishwa na nchi zote tulizopakana nazo, kwa hiyo hii ilikuwa ni mojawapo tuhakikishe tumeungana na mataifa yote kupitia barabara zetu, tumekamilisha. Sasa tuna zaidi ya magari 36,000 yanayopita on transit kupitia barabara zetu ambayo ni moja ya miundombinu muhimu ya kuhakikisha huduma zinafika kwenye nchi nyingine. Kwa hiyo ya kwanza ilikuwa ni maandalizi haya ya miundombinu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mmeongelea kuhusu uwekezaji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme. Tunaridhia tukiwa sasa tuko tayari; asilimia 95 ya bwawa letu limekamilika tunaenda kuwa na umeme wa ziada tunaziambia nchi za jirani zetu, nchi zetu tulizonazo kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, tuko tayari sasa kuwafikishia huduma ya nishati ya umeme. Hiyo yote ilikuwa ni kuwaandaa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kuanzia Serikali ya Awamu ya Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Awamu ya Tano na sasa Serikali ya Awamu ya Sita tumewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Ni wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Rais amezindua mkongo mwingine To Africa 5G, zile si za kubaki Tanzania. Tunufaike Watanzania lakini tuwaambie nchi za Kusini mwa Afrika kwamba sasa tuko tayari kuwahudumia kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Miundombinu imewekwa vizuri sasa tunapeleka huduma, tunaridhia leo Watanzania tukiwa sote tuna uwezo wa kuwahudumia kwenye sekta zote tulizo nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na ndugu zangu Watanzania, kwamba hatujachelewa. Tumesema theluthi mbili ya nchi za Kusini mwa Afrika zilizotakiwa kuridhia ili utekelezaji huu uanze zimefikiwa mwaka 2022, Januari, ni mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi hatuko nyuma kwa hiyo tuko tayari kuingia sasa. Na kama ilivyo kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akisisitiza, kwamba tunapokwenda kujiunga na kanda hizi za kiuchumi na kibiashara tusiingie kama wasindikizaji. Hili pia ninyi Waheshimiwa Wabunge mmesema, kwamba tuingie kama washindani, na ndilo lengo lililokuwa la Serikali yetu. Mazingira sasa ni mazuri, mazingira yameandaliwa tuendelee kunufaika sasa na uwepo wetu kwenye Jumuiya hii ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie jambo moja la mwisho. Nimshukuru sana Mheshimiwa dada yangu Jenista Mhagama kwa kusema, Serikali tunajiratibu. Na hata leo tunapohitimisha hapa ushauri elekezi niliousema mwanzo alishaainisha sera, sheria na kanuni ambazo zitaonekana kama vikwazo tunapoelekea kule kufanya biashara hii ya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu walishaanza kuturatibu kupitia kitengo alichokitaja Mheshimiwa Waziri; kwa hiyo tumeanza kuzifanyia kazi hizo kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, Serikali tuko tayari, sisi mmesema kama waratibu wa biashara ndani ya Taifa letu tunafanya kazi kwa ukaribu sana na Ofisi ya Waziri Mkuu. Yote tunayaainisha tunamkabidhi Mheshimiwa Waziri Mkuu, na yeye anakaa na sisi kama Serikali; tunaweza kuyashughulikia moja baada ya jingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo sera, nimetaja moja, Sera ya Biashara ya Mwaka 2003, zipo hatua za mwisho katika kupitishwa na Serikali yetu ili iweze kuchukua yote mliyoyasema Waheshimiwa Wabunge, tupo hatua za mwisho na tunaendelea kuifanya kazi. Niwatoe hofu Serikali yetu imeweka miundombinu wezeshi na mizuri, ufanyaji biashara ndani ya Taifa letu umerahisishwa kwa kiwango kikubwa. Mmesemea issue ya leseni Serikali tulishaiona tunaendelea kuifanyia kazi, na kupitia Bunge letu Tukufu tuna imani matamanio ya wafanyabiashara wetu wa ndani ya nchi, yatafikiwa lakini pia wafanyabiashara wetu ambao watatoka nje ya nchi kuja kutuletea teknolojia zilizo kule kwenye nchi zao pia nazo tutaendelea kuzishughulikia hatua baada ya hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema maneno haya naomba sasa kuleta kwenye Bunge lako Tukufu Itifaki hii ya Biashara ya Huduma ya SADC, Ili Bunge letu liweze kuridhia kama Sheria yetu na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 163, Ibara ndogo ya 3(e) inavyotuelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.