Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kuwapongeza Kamati ya Sheria Ndogo kwa kazi kubwa wanayoifanya, lakini nimekuwepo kwenye Kamati hiyo kipindi cha nyuma kidogo miaka mitano kwenye Kamati ya Sheria Ndogo. Changamoto zilizokuwepo zilikuwa kubwa sana, nichukue nafasi hii kumpongeza Mama yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, amefanya kazi kubwa kwa kipindi hicho ambacho alikuwepo, lakini bado una kazi ya kufanya, pamoja na pongezi unayo kazi ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu pamoja na nia njema kwenye Ibara ya 97 Kifungu Kidogo cha Tano, cha Bunge kuamua kukasimu kwenye mamlaka nyingine kutunga kanuni na hizi sheria ndogo, ile maana yake inaondoka kunapokuwa na makosa mengi sana na kuondoa tafsiri halisi ya kukasimisha ili waweze kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotunga sheria hapa, sheria tukishamaliza kuitunga haiwezi kuanza kutekelezwa bila kutunga kanuni na sheria ndogo, lakini shida inakuja hapo tu wanapoenda kutunga sheria ndogo hizo na hizo kanuni, zinakwenda kuondoa kabisa maana halisi ya ile sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hizi dosari ambazo Kamati imezungumza leo ni zile sheria ndogo tu chache zilizofika kwenye Kamati, lakini kuna madudu mengi sana. Mimi nataka kusema kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mpaka sheria ije kuwa Gazetted imepita kwa watu wengi sana, ina maana watu wote hao hawana macho, hawaoni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii shida tunapoiona leo na ukiangalia hapa makosa yote ambayo yanaonekana kwenye hizi sheria ndogo, mengi wanatunga hizi sheria kwa ajili ya tamaa na kujikita kwenye adhabu zaidi kuliko kuwasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo lazima kama Bunge tuyaseme. Kamati ya Sheria Ndogo imepewa nafasi kubwa ya kuwasilisha taarifa zake mara kwa mara ndani ya Bunge, lakini inapotokea imekuwa ni azimio, Bunge limepitisha tunaamini kabisa kwamba waliopewa nafasi Serikalini watakwenda kutekeleza kwa kuwa Bunge tayari limeazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea mpaka leo tunazungumza hapa kwamba dosari, Sheria Ndogo zenye dosari 19 hazijafanyiwa kazi. Kwa namna nyingine hakuna lugha nyingine ya kuzungumza zaidi ya kusema ni dharau kwa Bunge kutokuheshimu Mamlaka ya Bunge. Sasa maumivu yanapotokea kwa Watanzania hawaangalii mamlaka zile ambazo tulikasimu watunge, wanaangalia ni Bunge limeamua kuwaumiza wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tutazungumza nini kipya zaidi ya kuwaambia hawa ambao hawajatekeleza waende kutekeleza au adhabu nyingine zichukuliwe na wao ili wajue kwamba kuna maumivu makali yanatokea kwa wananchi wetu. Mimi nimuombe Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo, leo tunapozungumzia Sheria Ndogo unazungumzia maisha halisi ya Watanzania kule chini. Kwa hiyo, inapotokea hizi dosari utakuta mwananchi amehukumiwa kwenye kosa hilo hilo la Sheria Ndogo, ameadhibiwa baadaye ndiyo mnakuja kugundua makosa wakati tayari wananchi wameshaumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo lazima, sasa hivi tunapotunga hizi Sheria Ndogo zianze kupitiwa kabla ya kuanza kutumika. Kwa sababu unakuja kugundua wakati maumivu tayari yameshatokea kwa Watanzania, lakini ukizitazama hizo Sheria Ndogo nyingi zimezungumzia adhabu hazijaweka sehemu ya uwajibikaji wa Serikali, na ndipo shida inapoanzia hapo. Kungekuwa na uwajibikaji nafikiri wote tungerudi kuziangalia hizi Sheria Ndogo kabla ya kuanza kutumika kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiangalia hata kwenye Mabaraza ya Madiwani, wale wataalam wetu wanashindwa kyutumia taaluma zao kuwaambia sheria hii haitafaa kama ambavyo wanataka kupitisha, wakati mwingine ni tamaa ya kutaka makusanyo. Kwa hiyo, wanatunga sheria ambazo hawaangalii athari kwa Watanzania, wanangalia makusanyo kwewnye Halmashauri yao. Sasa hatuwezi kwenda hivyo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotunga hizo kanuni na Sheria Ndogo kuna taratibu za kufuata ni pamoja na kuangalia Sheria Mama imesema nini. Kama inaanza kukiuka mapema Sheria Mama inawezekanaje wataalam waliopo huko ambao ndiyo wawakilishi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanaruhusu zinapita mpaka zinaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo tunaposema kwamba Sheria Ndogo zimeshakuwa gazetted leo inawezekana katika zile ambazo tayari mnazipeleka kwenye gazeti la Serikali zilishaanza kutekelezwa huko miaka mingi, halafu mpaka ije ifike kwenye Kamati. Hizi Kamati, kwa mfano yale makosa ambayo ni ya kiuandishi siyo kazi ya Kamati kuja kuangalia hayo makosa, hivi Ofisi ya Mwanasheria hawakuona kwamba hizi hazitakiwi kuingia kabisa kwenye Sheria Ndogo? Mpaka zinakuja kufika kwenye Kamati ndiyo wanagundua, yaani Kamati ndiyo wanagundua kwamba kuna kosa la kiuandishi. Hii Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kunashida gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mimi niombe, inawezekana pia kutokufanya semina elekezi za mara kwa mara kwa Wanasheria wetu kwenye Halmashauri. Tulizungumza mwaka juzi Mheshimiwa Jenista Mhagama, alifanya hivyo mwaka jana, lakini usifanye mara moja moja, hawa watu waiteni ili angalau wabadilishane uzoefu, na wakati mwingine tusitunge sheria kwa sababu sehemu fulani wametunga ndiyo maana inatupeleka kwenye tamaa. Sheria hizi lazima ziendane na mazingira halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na Sheria Ndogo ambayo inazungumzia kwamba ni marufuku mwananchi kuzurura kuanzia saa nne usiku, hiyo ni sheria ya wapi? dunia gani? Sasa unaweza ukaona mpaka inatungwa, inapitishwa hivi kweli hakukuwa na wataalam waliyoipitia mpaka ikafika ikaanza kutekelezwa. Haya mambo hayakubaliki. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi ya kuzungumza hapa, lakini hatuwezi kuzungumza wakati kuna maazimio kadhaa ambayo yameshapita hamjatekeleza. Nimuombe Mheshimiwa Mchengerwa ameingia TAMISEMI. TAMISEMI ni kitu kikubwa sana ambacho utekelezaji wake ni mgumu, lakini ukiangalia kwenye dosari hizi Sheria Ndogo ambazo zina dosari nyingi zimeelekea TAMISEMI ambazo hazijatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hatutakuhukumu moja kwa moja, lakini hapo alikuwepo Waziri na Bunge limeshaazimia, haiwezekani Bunge linaazimia tunakuja tena kwenye Bunge lingine yale mambo hamjatekeleza ni dharau kwa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe Kiti chako, hatuwezi kuwa tunapoteza muda kuzungumza mambo ambayo tayari Bunge lilishaazimia ni dharau kwa Bunge. Baada ya kusema hayo kwa kuwa mengi yameshazungumzwa ninaomba Ofisi yako Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ongeza umakini kwenye kupitia sheria hizi ambazo zinaumiza watanzania. Ahsante sana. (Makofi)