Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Jamal Kassim Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia, nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Magomeni kwa kunichagua kuja kuwa mwakilishi wao katika Bunge letu hili Tukufu. Ni imani yangu ya kwamba tutashirikiana pamoja katika kuleta maendeleo ndani ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, niwapongeze Watanzania kwa kuendelea na kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi na kukipa fursa kuongoza nchi yetu kwa kipindi kingine. Naamini hivyo hivyo kwa Wazanzibari wenzangu wataendelea kukipa fursa chama chetu kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wachangiaji waliotanguliwa kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; Waziri Mkuu na timu yote ya Serikalini kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameanza kuifanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Nimpongeze Dkt. Mpango na timu yake yote kwa kuwasilisha Mpango mzuri kabisa ambao umekwenda kujibu au kutafsiri ile dhana ya Rais wetu ya kusema anataka kuipeleka nchi yetu kuwa nchi ya viwanda. Niwapongeze sana Wizara kwa kuandaa mpango wetu huu mzuri na kuwasilisha vizuri katika Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo nitayagusia, eneo la kwanza, ni eneo la kodi. Nimpongeze Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenyewe kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuweka mikakati kuona namna gani tunaendelea kukuza makusanyo yetu ili tuweze kumudu mahitaji yetu ya maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejionea ongezeko kubwa kabisa la ukusanyaji wa kodi ambalo taasisi yetu ya TRA kwa kipindi hiki cha miezi miwili ambayo imefikia. Niwapongeze sana na juhudi hizo waziendeleze ili kukuza makusanyo, kwa sababu tunaamini kabisa makusanyo hayo ndiyo yatafanya Mpango wetu utimie na yale maendeleo ambayo tunakusudia kuwapelekea wananchi yafikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la kodi, kwa kipindi kirefu kabisa, kumekuwa na masikitiko au malalamiko yanayohusu masuala ya bidhaa na vitu ambavyo vinatoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mfumo wetu wa kodi uliokuwepo hivi sasa kwa bidhaa hizi zinazotoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara kunakuwa na tozo la kodi ambalo linaitwa difference.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati tunajiuliza, iweje tufikie hapo? Tuna Taasisi moja ya kodi ambayo ni TRA, Taasisi hii na Zanzibar ipo, inatumia sheria moja na mwongozo huo huo mmoja, wa Kamishna huyo huyo mmoja wa Forodha. Tumekwenda kutengeneza mfumo ambao umetengeneza urasimu, manung‟uniko na baadhi ya wakati hata ukokotoaji wa kodi hizi hauko wazi, wananchi wetu hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana television yake tu akifika pale Bandarini Dar es salaam anaambiwa alipie kodi hajui alipie kodi vipi na ile TV ameinunua Zanzibar. Kwa hiyo, mambo kama haya, are very peanut, lakini huko mtaani tunakwenda kutengeneza bomu ambalo wananchi wetu wanalinung‟unikia lakini Serikali yetu inachukua muda mrefu kabisa kulipatia majawabu mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi najiuliza, TV ili itozwe kodi ya forodha maana yake lazima mkadiria kodi aijue CIF yake, aliijuaje? Kwa hiyo, hizi kodi hazina base yoyote, tumekuwa tunatengeneza fursa ya maafisa wetu kujiamulia tu haya mambo na kwa asilimia kubwa yametengeneza urasimu na mifumo ya rushwa. Kwa hiyo, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri, hili jambo linawezekana, halihitaji mshauri mwelekezi, yeye mwenyewe anatosha kulielekeza, kulifuta, hao wananchi basi wa-enjoy fursa ya Muungano wetu, Wabara waende Zanzibar na bidhaa zao bila tabu, Wazanzibari wakija bara, waje bila taabu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nitalizungumzia, eneo la viwanda. Tumeona kabisa Mheshimiwa Rais, toka alivyokuwa katika kampeni zake na alivyozindua Baraza lake la Mawaziri alikuwa anazungumza sana kuhusu suala la viwanda. Lengo lake ni kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Nampongeza na namuunga mkono katika hilo na naamini kabisa, viwanda ambavyo tutavianzisha ndiyo vitakwenda kujibu matatizo ambayo nchi yetu inayakabili kwa sasa, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda matatizo ya ajira kwa vijana wetu, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda kujibu matatizo ya masoko kwa wakulima wetu, wafugaji na wavuvi. Viwanda hivi hivi ndiyo vitakwenda kujibu tatizo letu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha. Hiyo ni kengele ya pili nimeshauriwa hapa.