Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kuweza kuchangia, nakushukuru kwa hilo. Pili ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuliongoza Taifa hili vizuri.

Tatu, ninapenda kuwapongeza Mawaziri wote waliofanikiwa kuhudhuria katika vikao vyetu vya Kamati ya kudumu ya Sheria Ndogo, kwani kwa kufanya hivyo wamekuja kujadili dosari mbalimbali ambazo tumeziona katika sheria ambazo wamekasimiwa kuzitengeneza na Bunge lako hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dosari hizi kwa kweli huwa zinakwamisha utekelezaji wa sheria mama au zinaleta usumbufu katika utekelezaji wa sheria hizi kwa wananchi. Katika Sheria Ndogo hizi huwa kuna majedwali mbalimbali ambayo hukusanya taarifa mbalimbali ambazo zipo kwa wingi na ambazo zinahusu mambo yanayofanana.

Mheshimiwa Naibu Spika, dosari katika majedwali haya huwa yanaathiri sana au kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa sheria hizo, ambazo huwa zimetungwa kutokana na Sheria Mama na kama nilivyosema awali zinaleta usumbufu mkubwa katika utekelezaji wake. Nitatoa mifano ya majedwali mawili, kwanza nitaanzia kanuni za usafirishaji wa mazao ya misitu kuingia ndani ya nchi na kutoka nje ya nchi, ambazo ni tangazo la Serikali Namba 266 iliyotolewa tarehe 31 Machi, mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kanuni hizi ilikuwa ni utekelezaji wa Sheria za Misitu, Sura Namba 323 ambayo katika hizo tunapatia mapato ambayo yanachangia katika uendeshaji wa kila siku wa Serikali na Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali hilo kuna vituo vya kuingia na kutoka nchini kwa mazao ya misitu, ukiangalia njia mbalimbali za kutokea nje ya nchi ambazo ni njia za usafiri utaona kila aina ya usafiri, aidha imewekewa au kuna nyingine hazikuwekewa. Nitapitia moja moja, tukianza na barabara, katika njia ya barabara kanuni hizi zimetoa vituo vya kutosha ambavyo vinaweza kutumika katika kukagua bidhaa hizo. Tukienda kwenye usafiri kwa njia ya reli, vituo vilivyotolewa ni Moshi, Arusha, Tunduma na Kahe junction tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unaona dhahiri kwamba kuna vituo vingine ambavyo vinahusisha mazao kutoka nje ya nchi ambavyo havikuwekwa, hivyo kutokuwemo katika vituo hivyo, aidha kutaleta usumbufu kwa wananchi kwamba wakifika katika vituo hivyo itabidi wasafiri umbali mkubwa kwenda kwenye vituo vingine ambavyo vinaweza kusababisha ukaguzi wa mazao hayo kitu ambacho ni usumbufu. Kwa hiyo, hili limebidi Kamati yetu imeshauri lirekebishwe na tungeomba Wabunge mtuunge mkono ili dosari hiyo iweze kusahihishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika usafiri wa njia ya maji ambao unahusisha bandari, katika Bahari ya Hindi vituo vimewekwa vya kutosha kutoka kaskazini hadi kusini. Vilevile katika Ziwa Tanganyika ambapo ni mpaka kati ya nchi yetu na nchi zingine vituo vimewekwa. Ukiangalia Ziwa Victoria ambalo tunapakana nalo katika nchi mbili, hakuna kituo ambacho kimewekwa kwa kusafirisha mazao hayo. Hivyo basi inamaana wananchi wakitaka kusafirisha mazao yao ya misitu nje ya nchi kwa njia ya maji usafiri ambao unajulikana ulimwenguni kwamba ndiyo usafiri wa rahisi kabisa hakuna vituo. Kwa hiyo, inabidi huyo mwananchi asafiri kwenda katika vituo ambavyo vinaruhusiwa kitu ambacho ni usumbufu mkubwa wakati ambapo vingeweza kuwekwa vituo katika njia hizo za usafiri wa maji katika Ziwa Victoria na ikaweza kurahisisha jukumu hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Ziwa Nyasa hakuna kituo ambacho kimewekwa na wakati Ziwa hilo ni mpaka kati yetu na nchi ya jirani. Kwa hiyo, kukosekana kwa vituo hivyo mazao ya miti kuingia au kutoka kupitia Ziwa hilo ni usumbufu au inamuongezea gharama huyo mtumiaji wa usafiri huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usafiri wa anga. Vilevile katika usafiri wa anga ambao husafirisha kupitia viwanja vya ndege hakuna kituo hata kimoja ambacho kimewekwa kwa ukaguzi wa mazao hayo. Hiyo nayo inaleta usumbufu kwani ina maana kwamba, unaweza kupata usumbufu mkubwa ukiwa pale wakati ambapo ukaguzi huo ungeweza kufanyika pale kwani inafahamika kabisa kwamba ule ni mpaka ambao unaweza kutumika katatika kusafirishia mazao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine unatokana na majedwali ambayo yametengenezwa katika Kanuni ya The Law School of Tanzania Admission Fee and Conduct of Practical Legal Training Kanuni za mwaka 2022. Katika kanuni hizo ukiangalia majedwali pale hakuna form maaalum itakayotumika katika maombi kulingana na kanuni ambayo imetengenezwa, Kanuni Namba Nne. Huu ni usumbufu mkubwa kwani unaweza ukakuta kwamba katika maombi yale muombaji akashindwa kuweka vitu ambavyo vinavyotakiwa ambayo italeta usumbufu katika udahili wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kanuni hizohizo ukiangalia jedwali la ada limetumia maneno ambayo hawakutoa maana yake ambayo yanaweza kuleta mkanganyiko mkubwa. Kwa mfano, wametumia neno Tanzanian students bila kueleza maana yake. Katika uchambuzi wetu tumeona hili neno linaweza kuleta usumbufu kidogo, kwamba je, linamaanisha ni raia wa Tanzania au linamaanisha mtu aliyesomea Tanzania au vinginevyo? Sasa hiyo ili isiweze kuleta huo mkanganyiko katika hayo mambo tulikuwa tumeazimia kwamba maneno ambayo yanaweza kuleta utata katika matumizi yake yaweze kutolewa tafsiri katika kanuni ili kuwafanya watumiaji waweze kuyatumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ikiambatana na hiyo vilevile kuna neno non-Tanzanian student ambayo katika uchambuzi wetu tuliona kwamba linaweza kutafsiriwa kwamba ni mwanafunzi ambaye hakusomea Tanzania. Anaweza kuwa mtanzania ndiyo lakini hakusomea Tanzania na akaambiwa wewe ni non-Tanzanian student kwa hiyo, tukasema hii tafsiri zitolewe ili mkanganyiko huu usiwepo kabisa katika kanuni hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali la kwanza vilevile za kanuni hizo ziliwekwa ada mbalimbali ambazo zinatumika katika chuo hicho, lakini unaona ada ya maombi ya kujiunga haina form wakati ambapo imeainishwa kule ndani na inaweza kuleta usumbufu. Katika jedwali hilo hilo vilevile imeoneshwa changamoto ya kuomba ada kwa Wanasheria Wasaidizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Sheria Mama ambayo ni The Law School of Tanzania Act, Sura ya 425 katika kifungu cha pili, kinatamka waziwazi kwamba sheria hiyo inatumika kwa wanasheria tu, sasa ukikuta kwenye jedwali wameweka ada za Wanasheria Wasaidizi wakati sheria mama inadai sheria hiyo itumike kwa Wanasheria tu wenye shahada ina maana kwamba Kanuni hizi zimevuka mipaka yake na kufanya kitu ambacho hakiruhusiwi, hivyo inabidi ifanyiwe marekebisho ya kuweza kuondoa kasoro hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumeliona waziwazi ni kutohuishwa kwa majedwali kwa wakati. Katika jedwali hilohilo ambalo lilikuwa linahusu ada, kuna ada ya mapitio yanayofanywa na NACTE, taasisi ambayo haipo kisheria sasa hivi na imebadilishwa, hivyo uhuishwaji wa Majedwali haya ni muhimu kwa wakati ili yasilete usumbufu katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mchango huu wa majedwali, tumeazimia kwamba majedwali haya yarekebishwe kwa wakati ili tuweze kupata utekelezaji mzuri wa sheria hizi kama ambavyo Bunge liliazimia kwenye kutunga sheria mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)