Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie kwenye taarifa ya Kamati yangu ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kama ilivyowasilishwa na Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba kipekee nimshukuru Mheshimiwa Spika kwa kunipangia Kamati hii, kwa sababu imepanua wigo wa uelewa wangu wa umuhimu wa Sheria Ndogo katika ustawi wa jamii na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyekiti wa Kamati yetu, Makamu wake, Wajumbe wenzangu wa Kamati na Makatibu kwa ushirikiano mkubwa walionipatia na kuniwezesha kujifunza mengi kama Mjumbe wa Kamati katika kipindi kifupi na kutambua umuhimu wa Sheria Ndogo ambazo zinagusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda, naunga mkono hoja ya Kamati yetu ya Kudumu ya Sheria Ndogo na ninakubaliana na taarifa na mapendekezo kama yalivyowasilishwa. Naomba pia nitumie fursa hii kwanza kuipongeza Serikali kupitia Wizara husika kwa taarifa walizotupatia pamoja na semina zilizotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali katika kutuelimisha, kutuhabarisha kuhusu utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kama zilivyopitishwa na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati tumepata wasaa wa kuchambua Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Bunge lako Tukufu pamoja na uchambuzi wa taarifa za utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, naomba kutoa pongezi kwa Serikali kwa hatua nzuri ya kukamilisha marekebisho ya Sheria Ndogo mbalimbali kutokana na dosari zilizobainishwa katika utekelezaji wa kutangazwa katika Gazeti la Serikali, kama zilivyowasilishwa leo kwenye Bunge lako tukufu kupitia Hati iliyowasilishwa Mezani na Waziri Mkuu. Leo tumeshuhudia kwamba kumekuwa na Matoleo 22 ya Gazeti la Serikali, kuanzia mwezi Aprili mwaka huu 2023 hadi Mwezi huu wa Septemba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kutangaza marekebisho katika Gazeti la Serikali ambayo imefikiwa na Wizara zinazohusika katika kipindi husika, ni mwitikio mzuri wa utekelezaji wa Maazimio ya Bunge yanayolenga kuondoa changamoto zilizobainishwa katika Sheria Ndogo kama ilivyooneshwa kwenye jedwali la utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kwenye taarifa ya Kamati. Hatua hii inastahili kupongezwa kwa kuwa ni hatua ya juu ya uzingatiaji wa Maazimio ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujibu hoja mbalimbali za Kamati, mamlaka zinazohusika zimeweka juhudi ya kusahihisha dosari zilizobainishwa na Kamati. Kwa kufanya hivyo, madhara ya dosari hizi yameondolewa kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, Sheria Ndogo ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mwaka 2022, kifungu cha 14(3) ambacho Mheshimiwa mwanakamati mwenzangu, Mheshimiwa Maryam alikigusia, kinaeleza kwamba iwapo abiria atakayetupa taka nje ya chombo cha usafiri, kilikuwa kimeweka sheria kwamba mmiliki wa gari, dereva au kondakta ndio aweze kulipa faini isiyozidi shilingi 50,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Serikali imelisikia hili na imeweza kutekeleza maagizo au Azimio la Bunge iliyoitaka kufanyiwa marekebisho ili kumtaka mkosaji mwenyewe aweze kuadhibiwa kwa kosa alilolifanya. Kwa hiyo, tumeona leo kwamba marekebisho ya kifungu hicho yamefanyika kwa kufuta kifungu hicho na kukiandika upya kwa kumwondoa mmiliki na dereva katika makosa yanayotendwa na abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo inaakisi misingi ya haki ya mtu kuadhibiwa iwapo ametenda kosa na siyo vinginevyo. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua hiyo, Kamati kama Wajumbe wenzangu walivyosema, imebaini ucheleweshaji katika kurekebisha dosari zilizobainika katika utekelezaji wa Sheria Ndogo. Ucheleweshaji huo unasababisha athari hasi za dosari zilizobainishwa katika Sheria Ndogo mbalimbali na hivyo kushindwa kutatua kero ambazo Bunge lako tukufu lililenga kuziondoa kwa ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, zimetajwa sheria mbalimbali ambazo zinacheleweshwa au hazijatekelezwa kutokana na Maazimio ya Bunge, lakini naomba nitoe mfano tu kuhusu hii Sheria ya Environmental Management Control and Management Carbon Trading Regulation of 2022, hii inahusu maombi ya biashara ya carbon. Tumekuwa tukiongelea hilii hata wakati nikiwa kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara, kwamba hii iweze kutungiwa kanuni ambayo inaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nafurahi kusema kwamba kama Wajumbe wa Kamati, sote tunaelewa umuhimu wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo ambayo imekuwa engine ya Bunge lako katika uthibiti wa Sheria Ndogo na utekelezaji wake ulio na tija kwa kuwa sheria hizo zinazogusa moja kwa moja maisha ya wananchi. Ibara ya 8(b) ya Katiba inaeleza kwamba lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba nirudie kwamba naunga mkono hoja ya Kamati yetu mia kwa mia, ahsante sana. (Makofi)