Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Kamati pamoja na wajumbe wake na wote waliobahatika kuchangia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi kusikia dosari ambazo zimetajwa hapa pamoja na maazimio. Baada ya kusikiliza yote jambo la kwanza ambalo ninapenda kukariri ni kwamba, ni kweli kwa mujibu wa mgawanyo wa madaraka ya vyombo vyetu mhimili kwa mujibu wa Ibara ya 4. Tunatambua kwamba mamlaka yote ya Serikali yanatoka kwa wananchi kwa mujibu wa Ibara ya 8.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(d) ndiyo linalotunga sheria zetu. Pia tunatambua kuwa ustawi wa wananchi, msingi wake ni ule umewekwa kwenye Ibara ya 146 ambao madhumuni ya kuwepo kwa mamlaka zilizopo, zinazotunga sheria maana yake inafuata ule mlolongo ambao unafuata mamlaka zilizotajwa na mihimili.

Mheshimiwa Naibu Spika, yote ambayo yameelezwa hapa na dosari hizi tunatambua kwamba sheria mama zinapotungwa ndiyo zenye kutamka kuwa nani mwenye dhamana ya kutunga Sheria Ndogo na vilevile ni nani mwenye dhamana ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa imeendelea kufanyika na tunalipongeza sana Bunge hili kwa sababu, kila sheria zinapotungwa kati ya mambo ambayo yamekuwa yakinishughulisha Bunge hili na Waheshimiwa Wabunge ni pale ambapo kuna ugatuaji wa kutugwa kwa Sheria Ndogo au kanuni kufuata masharti ambayo yanakuwa yamezingatia Sheria Mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ilivyotolewa na tukiangalia hata kwa mtiririko wa miaka hii miwili. Kumekuwa na maendeleo makubwa ya kupungua kwa dosari mbalimbali. Pia tunatambua kuendelea kuwepo kwa dosari hizi lakini yapo mengi ambayo yanaendelea kufanyika ambayo tunaungana na Kamati kwamba dosari ambazo zimetajwa ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha kuwa zinatatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Mheshimiwa Mpinga katika mchango wake ameeleza vizuri. Kwamba, tangu mwaka 1920 kanuni ya sheria ndogo ya 4151 zilifungwa lakini kwa sasa kwa zoezi linaloendelea ni kuhakikisha kwamba kuna zoezi la kuhuwisha pamoja na kubaki na zile Sheria Ndogo ambazo zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria mama 446 zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo kwa sasa sheria ndogo hai zilizopo kutoka hiyo 4151 zimebaki 25,000. Dosari ambazo zimekuwa zikitajwa hapa na hatua ambazo tumekuwa tukizichukua, tunatambua uwepo wa upungufu katika ngazi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mwaka jana tarehe 7 Novemba yalitoka maelekezo kwenda kwa watendaji Wakuu wa Halmashauri, Tawala za Mikoa na Watendaji Wakuu Serikalini, kulipo na upungufu wa wanasheria, kuhakikisha kwamba wanasheria waliopo kwenye ofisi zilizo jirani wanatumika kwenye mazoezi ili kuhakikisha kazi za kisheria zinatekelezwa kwa kufuata misingi ya Sheria Mama na matakwa mengine ya kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili limesaidia kuendelea kupunguza dosari ambazo zimekuwepo. Pia imeelezwa hapa, mafunzo na maelekezo mengine ya kiutendaji ambayo yanalenga kuboresha namna ya kuhakikisha sheria zetu zinakuwa hai na zinatekelezwa na kupunguza kero kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua ingawa Mheshimiwa Mariam hajawahi kuongea na mimi, ni kweli. Lakini ninaamini kufikika kwangu na watendaji wa ofisi yangu kumechangia sana kuboresha changamoto mbalimbali zinazopatikana kuanzia ngazi za halmashauri na maeneo mengine ya kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wajibu wetu kuwajibika. Pia siku zote Mheshimiwa Chief Whip siku zote ameendelea kuratibu changamoto zinazopatikana na kuzisambaza kwa wadau wetu. Kwa hiyo, hizi ni hatua ambazo zitaendelea kuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizidi kuomba katika hatua hii, nimeelewa kama nilivyo mimi na Waheshimiwa Wabunge kama nyinyi mlivyo na uhusika wenu kwenye mabaraza ya ngazi ya madiwani. Tuendelee kushirikiana wote kuhakikisha kwamba dosari hizi zilizosalia zinapungua kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na Wakurugenzi, Wasimamizi wa Mamlaka katika ngazi mbalimbali na mamlaka nyingine kuhakikisha tunaendelea kuboresha mifumo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo mipango mingine mingi ambayo Serikali inaendelea kuifanya, maana Mheshimiwa Kenani ameuliza ofisi yetu tunafanya nini? Kwa sasa tumeendelea sana kuboresha ile division ya uandishi wa sheria. Maboresho ya sheria yanakuja ili iweze kuwa na mfumo ambao utawezesha kusimamia vizuri kazi za kisheria hasa kwenye eneo la uandishi, kutoka ngazi za chini hadi ngazi za juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itaendana na kile ambacho Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria ameeleza, mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba Law Reform Commission na yenyewe inahusika kikamilifu kuhakikisha sheria zetu zinakuwa zinaongozwa na tafiti na zinakuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya yote sisi tutaendelea kuhuwisha sheria zetu na kufanya urekebu na kuhakikisha tunakuwa na sheria kwa lugha ya Kiswahili. Kama nilivyosema katika sheria mama 446 tayari sheria 258 tumeshazitafsiri kwa lugha ya Kiswahili. Sheria zote mpya zinazotungwa sasa zinatungwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo nayo hii ni nyenzo muhimu sana kuwafanya wananchi wetu kuelewa hizi sheria na maana zake pamoja na madiwani wetu na watu wote wanaotumika katika mchakato wa kutugwa kwa Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba tunaipongeza sana Kamati pamoja na mapendekezo haya. Faraja yetu ni kwamba muda umetolewa kufikia Tarehe 2 Oktoba, basi hatua mbalimbali ziwe zimechukuliwa. Nitaendelea kufikika na nafikiri ambaye hajanifikia basi atakuwa yeye labda sababu zake. Kila mmoja hapa naamini katika kumbukumbu zangu sijawahi kufikiwa na mtu alafu nisimpatie jibu au nisimpatie huduma inayostahili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ahsante. (Makofi)