Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru, halafu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii asubuhi hii ya leo kwa kunipa pumzi ili niweze angalau kuchangia na mimi kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kuhusiana na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mimi leo nachangia kwenye jambo moja tu kubwa ambalo ni mahususi kwangu, linalohusiana hasa na kata ile ya Nyatwali ambayo wananchi wangu pale takribani 13,000 wanahamishwa kutoka katika eneo lile. Lakini wahusika ambao wanatarajia kuwahamisha wananchi hawa ni Wizara mbili, Wizara ya Ardhi ambayo ndio inafanya tathmini na Wizara ya Maliasili ambayo ndio yenye Mbuga ya Serengeti, hawa ndio wahusika wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi imepewa nafasi ya kufanya tathmini na kufanya valuation kwa ajili ya majengo ya wananchi wetu na kuwafanya ili waweze kupata stahiki zao vizuri. Wizara ya Maliasili ndio mlengwa na muhusika ambaye ndio anapaswa kuwalipa hawa wananchi wetu. Nyatwali sasa jambo lile la wananchi wa Nyatwali kuhama kutoka katika kata yao ile ya Nyatwali ni jambo ambalo mimi nimelisikia kwenye mahusiano yangu zaidi ya miaka 20 leo na nimelikuta likiwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa sababu pia jambo hili limekaa muda mrefu sana kwenye vichwa vya wananchi wetu, kwanza lilishawaumiza kisaikolojia, wananchi walishapoteza direction, kwa hiyo, hata leo ukiwauliza wanananchi wa Nyatwali kwamba mnatakiwa kufanya nini? Jibu la ndio wanaweza kusema hapana na jibu la hapana wanaweza kusema ndio kwa sababu lile jambo lilishawaumiza kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili tumeshawahi kukutana na Mawaziri pale walikuja kwenye kata yetu ya Nyatwali, Mawaziri wale nane. Walisikiliza maoni ya wananchi wao wenyewe kwa michango yao. Sasa jana niliona Mheshimiwa mmoja anachangia hapa anatoa taarifa kwamba wale wananchi wa Nyatwali wao walikuwa tayari kuondoka kwenye eneo lao. Mimi nasema hapana wananchi wa Nyatwali hawakuwa tayari kuondoka kwenye eneo lao isipokuwa wametakiwa kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametakiwa kuondoka kwa sababu ya manufaa makubwa ya nchi yetu. Kwa maana ya kuhakikisha kwamba ile Mbuga ya Serengeti imeongezwa kwenye eneo lao hilo ili Wanyama wetu wawe wanaenda kupata maji kwenye Ziwa letu la Victoria. Sasa wananchi wetu walioko pale Nyatwali wengi wameshaumia na sasa hivi akili yao imebaki tu Serikalini kwamba Serikali lazima itumie utu, kwa sababu wale wananchi ni wananchi wake, wanaipisha Serikali pale kwenye eneo lao ili Serikali ifanye uwekezaji wa kutosha pale ndio maana yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali imeenda kununua eneo kwa wananchi, siyo kwamba wananchi walivamia hapana. Inaenda kununua eneo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapokwenda kununua eneo kwa mwananchi ambaye yeye alikuwa hayuko tayari kununua eneo lake, siyo kwamba wewe unayekwenda kulinunua ndio unatakiwa kumpangia bei isipokuwa yeye mwneyewe anayetaka kuuza ndio atapanga bei. Sasa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili inawapangia wananchi wa Nyatwali bei ya kununua eneo lao badala ya wananchi wa Nyatwali wao wenyewe kupanga bei yao kwa yule anayetaka mali yao wamuuzie kwa bei wanayoitaka wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya muda mrefu wananchi wetu wa Kata ya Nyatwali wameridhia kukubali wakaona hakuna sababu ya kuendelea kubishana na Serikali wakasema walitoe eneo lao lile ili waache shughuli za Serikali ziendelee na shughuli za hifadhi zifanyike. Lakini pia ufahamu tu kwamba Halmashauri ya Mji wa Bunda ndio Halmashauri kubwa pia inayopata athari kubwa kupitia Mbuga ya Serengeti kwa wananchi wake, kwa sababu pale wananchi wanalishiwa mashamba yao na fidia yenyewe kutoka katika Wizara ya Maliasili na Utalii inaweza kuchukua miaka mitatu, bei yenyewe anayolipwa heka yake ya shamba ni shilingi 100,000. Lakini hiyo fedha mwananchi ataidai zaidi ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwananchi huyohuyo anayeishi pembezoni mwa Mbuga ya Serengeti, ng’ombe wake wakiingia kwenye Mbuga ya Serengeti kila ng’ombe mmoja atakuwa–charged kwa shilingi 380,000 kila ng’ombe aliyekanyaga kwenye Mbuga ya Serengeti. Huku yeye heka moja ya shamba analipwa shilingi 100,000 tena kwa kuidai kwa muda wa miaka mitatu.

Sasa mimi nilikuwa nawaomba watu wa Wizara ya Ardhi na Maliasili wale wananchi wa Bunda wakihamishwa kwa viwango vyao hivi walivyovipanga, pamoja na umaskini wao walionao watu wa Nyatwali, watazidi kuwaongezea umaskini mara tano Zaidi kuliko vile walivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu wale wanachi wa Nyatwali na wao Mbuga ya Serengeti ni mali yao, wala sio mali ya mtu mwingine, ni mali yao, kwa hiyo wanapisha ili wao wafanye maendelezo kwneye mali yao. Sasa kama wanapisha kwa nini wasilipwe fedha stahiki zinazoweza kuwafanya waridhike kwamba mali wanayoiondokea pale ili wanufaike nayo ni mali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wafanya tathmini wale wa Serikali walioko pale, wanafanya tathmini kwenye majengo ya wananchi wetu. Nyumba zile ni nyumba zimejengwa toka miaka ya 1968, leo wale wananchi wanaambiwa wahame kwenye eneo lile ambalo wamekaa toka mwaka 1968.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mwaka 1968 mpaka leo kwamba yule mwananchi alijenga nyumba yake ya majani. Kipindi hicho majani ya kukata kwa mikono yalikuwepo maeneo hayo, leo hii majani yale hayapo, halafu unamwambia leo huyo mwananchi utamfanyia valuation kwenye nyumba yake ya majani, utamlipa fedha kulingana na nyumba yake ya majani halafu yeye ataenda huko atakapokwenda, ataenda kutafuta majani aezeke nyumba yake kwa majani atayatoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, kila mwananchi, kila raia wa nchi hii sasa hivi kule alikokuwa anataka kutoka ili aende mahali pengine, hivi leo unawezaje kumfanyia valuation mwananchi kwenye nyumba yake ya majani, halafu ukamwambia ukitoka hapa ukajenge nyumba ya majani hiyo hiyo wakati kila mmoja anatakiwa kufanya kila jitihada akajenge nyumba ya bati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, wananchi wa Kata ya Bunda Mjini, wananchi wa Kata ya Nyatwali katika Halmashuri ya Mji wa Bunda, lolote litakalowapata katika haya, machozi yao yatabaki Wizara ya Maliasili na Wizara ya Ardhi. Wale wananchi wameshaumia kwa kiasi kikubwa, ni mategemeo yangu, ni maombi yangu na tumeshazunguka nao mara kadhaa kila sehemu kwenda kupeleka jambo hili kusema ili Serikali iweze kuwasikia, lakini bado jambo halijakaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe watu wa Wizara ya Maliasili na Ardhi wahakikishe kwamba wanawatendea wananchi wa Nyatwari haki yao ili wapate fedha stahiki ambazo zinaweza kuwafanya pale wanapotoka na huko wanakokwenda wakanunue eneo, na kwa sababu katika kuwahamisha kwao pale hawakuwatengea eneo maalum ambalo watakwenda kuishi wao wanawalipa fidia, wanawaambia nenda mtanunua ninyi wenyewe huko mnakokwenda kitu ambacho ukija kuangalia kwa sasa hivi mfano kwa mazingira ya sasa hivi ndoa nyingi baba na mama wanaishi, lakini hawako pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo fedha zile zinaenda zinawekwa kwa baba aidha zinawekwa kwa mama kati ya hawa wawili mmoja anaweza akaondoka nazo halafu wale Watoto wakabaki wanarandaranda pale mjini na hawatapata sehemu nyingine ya kwenda. Hawa watakapokuwa wanaanza kulia watakuwa wanaililia Serikali kwa sababu Serikali ndio ilichukua eneo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna wajane, kuna nini na watu wengi unajua Watanzania wameshaathirika kisaikolojia sana wale wananchi, Serikali ikapata eneo maalum ambalo itawapeleka wale wananchi wa Nyatwali, hautakuja ukaa ukasikia Kata ya Nyatwali na ukajua raia yoyote wa Nyatwali baada ya kuwa wamelipwa walihamia wapi hutakuja kukaa ukapasikia eneo hilo, kwa sababu watakuwa wamepotea katika mazingira ambayo hayawafanyi wao waende kutafuta sehemu nyingine ya kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia wanayopewa ni kidogo sana, nimuombe sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan anaamini kutokana na michango mingi ya Wabunge wenzangu hapa ameliona na amelisikia jambo hili alishike na alifanyie kazi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Robert Chacha Maboto kwa mchango wako. (Makofi)

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)