Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama hapa na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ningependa niipongeze Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri sana ambayo wameiwasilisha katika Bunge hili na nipende kusema jambo moja Wabunge tunapochangia tuangalie Kamati yetu imetuelekeza wapi kwa sababu hawa wenzetu ndio wanaojua mambo yote yanayoendelea katika wizara hii kwa sababu ndio wanaofanya nao kazi wakati wote. Kwa hiyo, tunavyotaka kuishauri na kuisimamia Serikali tujaribu kuangalia wenzetu wamesema nini? Kamati ndio Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kupitia taarifa ya Kamati ya Bunge na nimeona ni kwa namna gani ambavyo Wabunge wenzetu wameweza kuchanganua na kufafanua yale yote ambayo waliyoyasema katika hotuba aliyosoma Mwenyekiti. Nikupongeze sana Mwenyekiti wa Kamati hii ndugu yangu Mnzava kwa kazi nzuri na kubwa uliyoifanya na wajumbe wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa kwenye Kamati hii kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ninaijua vizuri sana, na ninaamini yale uliyoyaandika siyo majungu ndio ukweli uliopo na uhalisia na unachofanya ni kuisaidia Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake, ili iweze kuondoa migogoro inayowasumbua Watanzania kwenye maeneo yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za ardhi katika nchi yetu ni nyingi sana na kila siku ni afadhali ya jana, unapomuona Mbunge anasimama anazungumza kwa uchungu anajua ni namna gani wananchi wake wanapata adha na shida kubwa ya ardhi. Tunapozungumzia suala la kupanga matumizi bora ya ardhi siyo kwa sababu tuna kitu tunachokitaka zaidi ya kwamba tuondoe migogoro kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inayo Tume na nimwambie Mheshimiwa Waziri ana Tume nzuri sana, ina watendaji wazuri kweli kweli, hawa watu wakipewa mshiko, wakipewa fedha wanaenda kufanya kazi kweli kweli. Mimi hapa leo ninavyozungumza katika Mkoa wangu wa Tabora fedha kidogo walizopewa wameshakwenda kwenye vijiji zaidi ya 16 mpaka sasa ninavyozungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Tume, tulikuwa na mgogoro mkubwa sana wa vijiji katika Jimbo la Igalula, Kata ya Kizenga kuna vijiji viwili mgogoro umedumu pale kwa zaidi ya miaka nane, lakini wamekwenda juzi wamemaliza mgogoro ule kwa sababu ulikuwa kila siku unawafanya watu wanafungwa, unawafanya watu wanapelekwa mahabusu bila sababu zozote. Mimi ninavyozungumza hapa Mwenyekiti wangu wa Kijiji wa wakati huo mwaka 2017 aliwekwa ndani kwa sababu ya mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri na Wizara yake asifikiri Wabunge wanaposimama na kuzungumza masuala ya kupanga matumizi bora ya ardhi tunazungumza tu, lakini tumeona na tunajua faida ya kutoa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yetu tumechoka kufiwa kwa sababu ya migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wanalia kila leo kwa ajili migogoro ya watu wanauana na mimi nafikiri na nilisema hii migogoro huenda inanufaisha Wizara kwa namna moja ama nyingine, kuna manufaa wenzetu ambayo wanayapata kwa sababu haiwezekani kama hakuna manufaa wasisikilize haya ambayo tunasema na wanayaona na wanayajua, lazima wafike mahali wajue kwamba migogoro ya ardhi inachosha na niwaambie niwakumbushe tu...

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Nimemuona Mheshimiwa Waziri.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atajibu anamaliza muda.

MWENYEKITI: Naomba upokee Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, karibu.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hawa siyo kwamba namaliza muda.

Ninakushukuru sana na ninakupongeza kwa kuisifia Tume kwa kumaliza huo mgogoro, ili kusaidia Bunge hili lijue kwamba Wizara ya Ardhi haina manufaa yoyote na migogoro hiyo Tume inafanya kazi chini ya Wizara ya Ardhi, kwa hiyo kama unaona kuna mafanikio yoyote yamepatikana kupitia kwenye hiyo Tume ni kwa sababu Wizara ya Ardhi imeisimamia vizuri Tume, ni kwa sababu ya Serikali imeisimamia vizuri Tume. Kwa hiyo, naomba nikupe tu taarifa kwamba hivyo vitu vyote ni taasisi za Kiserikali na ni Serikali inayofanya hiyo kazi nzuri kwa pamoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwaifunga, unapokea taarifa?

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MWENYEKITI: Mheshimiwa sijakuruhusu.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anhaa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi?

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amenielewa Dada Jenista na anachokisema ina maana anakubaliana na mimi, migogoro ikiondolewa ina maana migogoro ikiondolewa hawa wa Tume wakipewa fedha ina maana hakutakuwa na mazingira yoyote ya watu wetu kufa kwenye maeneo yetu na ndichi hiki ambacho nimekisema kwamba inawezekana kuna baadhi ya migogoro inawanufaisha na hili silifuti ndio ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa baadhi ya Makamishna ambao wako kwenye mikoa yetu mbalimbali. Mimi nimpongeze Kamishna wa Ardhi amefanya kazi kubwa sana, amechukua ushauri vizuri sana wa Kamati, tulimuomba Mheshimiwa Kamishna atusaidie labda kufanya rotation ya hawa Makamishna inaweza ikasaidia kwa kiasi fulani kupunguza migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa na Kamishna katika mkoa wangu wa Tabora tunamshukuru sana amefanya kazi kubwa sana, sasa hivi kuna maeneo kwa kweli husikii migogoro, Wabunge sasa hivi kuna maeneo tumepumzika kusikiliza migogoro Kamishna aliyekuwepo, lakini hata huyu aliyeletwa sasa ninaona anaendeleza kazi ambayo imefanywa na mwenzake aliyetangulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maeneo mengi yana migogoro ukiwepo Mkoa wa Dodoma, Dodoma yaani ni kasheshe. Kwa hiyo mimi nimuombe sana Mheshimiwa Waziri hawa Makamishna mliowafanyia rotation, wapeni muda waweze kufanya kazi, waweze kuonesha kile ambacho mnakitaka sasa, kama mmeamua kupata mabadiliko kwenye Wizara kupitia hawa Makamishna, wapeni muda, wapeni ushirikiano waweze kufanya kazi ili muweze kuona matunda yao, mkiweka au kuhamisha watu bila kuangalia kwa nini mnawahamisha mnaharibu na matokeo yake huyu anamlaumu huyu na huyu anamlaumu huyu, mwisho wa siku migogoro inakuwa haipungui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba na nizungumze kidogo kuhusiana na hili suala la hii fedha ya mkopo na Kamati imefafanua vizuri sana. Mikopo tunapokwenda kukopa Serikali ninyi mnakwenda kwa niaba yetu sisi Watanzania kwa sababu mwisho wa siku hamlipi ninyi hiyo mikopo ni sisi Watanzania tunalipa kupitia kodi zetu. Sasa kama unapewa mkopo una masharti ambayo unayaona hayana manufaa kwa Watanzania una sababu gani ya kuchukua mkopo huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichukua mkopo hapa wa trilioni 1.3; Mheshimiwa Rais alipata huu mkopo na masharti ya mkopo huu ilikuwa tununue barakoa na sanitizer. Trilioni 1.3 Mheshimiwa Rais aliona hivi trilioni 1.3 naenda kununua barakoa na sanitizer wakati kuna watoto wanakaa chini, wakati kuna watoto wanasoma chini ya miti, wakati kuna wanawake wanajifungulia majumbani, wanawake wanajifungua barabarani, kwa nini mkopo usiwe wa kuweza kusaidia Watanzania kule walipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mkopo wa trilioni 1.3 tumeona manufaa yake, kila unapokwenda kwenye majimbo kuna madarasa yamejengwa, kila unapokwenda kwenye majimbo yetu kuna zahanati na vituo vya afya vimejengwa, leo tunapozungumza hapa tunalalamikia vitu vidogo vidogo, siyo majengo tena, je, mama angechukua huu mkopo akaenda kununua sanitizer na barakoa tungekuwa tunagaragara nazo tu hapa Bungeni kwa sababu hazina kazi, corona imeshakwisha au kama bado ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkopo wa trilioni 1.3 fedha ya uratibu iliyotumika, monitoring and evaluation hawa walitumia bilioni tano tu, katika trilioni 1.3 walitumia bilioni tano peke yake, lakini wenzetu wamechukua bilioni 345 uratibu peke yake wanatumia zaidi ya bilioni 47, hatukatai kwamba wanaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Watanzania wanauana kwa sababu ya ardhi nani atakwenda kwenye Ofisi za Ardhi hizo ambazo mnataka kuzijenga? Leo mnachukua fedha eti mnaenda kununua furniture, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge niwambie leo tunapokaa tunazungumza hapa Watanzania wanatuangalia na wanatuona, mwaka 2025 is around the corner, hakuna mtu atakayekuja kukusaidia kwenye jimbo lako utapambana mwenyewe. Mheshimiwa Jenista kakaa pale ataenda Peramiho, mimi nitakuwa Tabora hakuna atakaye kuja kunisaidia lazima nipambane na hali yangu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema huu mkopo lazima uangaliwe ili uendane na tija kwa ajili ya Watanzania na si vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)