Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii, jambo la kwanza nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kuhakikisha masuala kwenye Wizara ya Ardhi inakwenda vizuri, lakini pili nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na kwa moyo wa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri nakushukuru pamoja na Wizara ya Maliasili, tulikuwa na mgogoro uliochukua takribani miaka karibu kumi pale Kata ya Mfumbi, Wilaya ya Makete ulikuwa na changamoto kati ya Mpanga Kipengele na wananchi wa Mfumbi. Tunapozungumza haya ni kabisa wananchi wangu wanawashukuru sana kwa sababu mgogoro ule umeenda kutatuliwa katika ekari milioni 2.3 ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa kwa wananchi na sisi Wanamakete tumenufaika kwenye eneo lile, wananchi wale wanawashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Makete tunawashukuru kwa haya yanayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nipende kumshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara hii Engineer Anthony Sanga kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kwa kweli kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati hii tunafahamu Engineer Anthony Sanga saa hivi yuko na jukumu la kuhakikisha kwamba mifumo ya ulipaji wa kodi kwenye Wizara hii yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Katibu Mkuu na tunategemea kwamba suala la kwamba mfumo uko chini, watu wanashindwa kupata hati kwa wakati, litakuwa limeisha kwa sababu kote alikopita Anthony Sanga ameacha rekodi nzuri ya utendaji, kwa hiyo tiunaamini kabisa kwamba atatusaidia kwenye Wizara hii na mimi niamini kabisa kwamba kwa sisi Wanamakete tunajivunia kuwa na mtumishi ambaye anafanya kazi vizuri kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kumpongeza Mkurugenzi wa National Housing, Ndugu Hamad Abdallah, unajua Watanzania hawafahamu sasa hivi umekuja mfumo mpya wa PPP kwenye ujenzi wa hizi nyumba za National Housing na Mkurugenzi ameshatuonesha kwamba kuna viwanja kadha wa kadha kwenye Taifa letu na vipo kwenye eneo potential kama Kariakoo na maeneo mengine ambapo Watanzania wanaweza kushiriki kujenga nyumba hizi ambazo zinaweza kusaidia kwenye ukuaji wa sekta binafsi, lakini pia kwenye Shirika letu la Nyumba, kwa hiyo nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo yangu mawili, la kwanza ni tuna migogoro mingine Mheshimiwa Waziri ndani ya Wilaya ya Makete, tuna mgogoro kati ya Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya kwenye eneo la Mbarali kwa maana Kata ya Mfumbi. Watu wako kutoka Wizarani walifika kwenye eneo husika wakaainisha eneo la mipaka, lakini changamoto iliyopo ni kwamba hamjaweka beacon.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuweka beacon kumesababisha bado mgogoro uendelee kuwepo na hili ilitupa changamoto kubwa Mheshimiwa Waziri kwenye anuani na makazi, tuna vijiji zile anuani za makazi hazijawekwa kwa sababu ya mgogoro wa mpaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba mgogoro kati ya Mbeya na Njombe eneo la Chimala, eneo la Mbarali uweze kukamilishwa kwa kuweka beacon ili wananchi wa Makete wajue mpaka wao ni upi na wananchi wa Mbarali wajue mpaka ni upi ili tuondoe changamoto ya migogoro ambayo sisi Wanamakete tumeanza kuipata ya wafugaji kutoka Mbarali kuingia kwenye Jimbo letu la Makete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mgogoro mwingine upo kati ya Njombe na Mbeya kwenye eneo la Kikondo ambapo huko nyuma ilikuwa ni kati ya eneo la Hifadhi ya Kitulo na baadae tukawaondoa wananchi likabaki kuwa eneo la Makete, lakini kuna changamoto pale kati ya wananchi wa Makete na wananchi wa Mbeya Vijijini, tunaomba mtusaidie kwa ajili ya kutatua mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mkitusaidia sisi Wanamakete tutashukuru sana ili shughuli zetu za kiuchumi ziweze kwenda vizuri na shughuli zetu za kiuchumi kwa wananchi wetu ziweze kwenda vizuri na niseme wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri suala la ardhi ndio suala mtambuka kwenye Taifa letu ambalo linaweza likatatua migogoro mingi sana. Sisi hatukuwepo na migogoro hii ya wafugaji na wakulima, sasa imeanza kujitokeza kutokana na kwamba matumizi bora ya ardhi yamekuwa ni changamoto na hayajafanyika katika Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili ni kwenye suala la huu mkopo wa bilioni 350; Mheshimiwa Waziri na hii is for the good na ni kwa maslahi mapana ya Taifa letu, Taifa la Tanzania, Mheshimiwa Waziri tusaidie jambo moja tu hizi bilioni 350 Watanzania wanatusikiliza huko nje unapozungumza kwamba kwenye bilioni 350 kwenye uendeshaji tumekwenda kuweka bilioni 2.4, kwenye uratibu tumeweka bilioni 29 na kwenye dharura tumekwenda kuweka bilioni 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hata kwenye vikao vya harusi siku hizi wameacha kuweka kitu kinaitwa contiguous kwa maana ya fedha ya dharura kwa sababu unapoweka fedha ya dharura kwenye eneo lolote lile una-rise doubts kwa sababu unapoweka hela ya dharura wakati kuna uhitaji wa fedha kwenye Tume ya Mipango kuhakikisha maeneo yetu ya ardhi mengi yanapimwa nchini, lakini unafedha ya dharura ya bilioni 17; hii dharura ni dharura ipi ambayo inaweza kwenda kutokea na ikatumia fedha zote hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposhauri Mheshimiwa Waziri tunashauri for good, kwa sababu Watanzania wanatusikiliza na sisi ni Wajumbe wa Kamati, hizi bilioni 17 tungeweza kuwapa Tume ya Mipango wakatusaidia kupima ardhi kwenye maeneo mengi zaidi kuliko haya ambayo mmeyaainisha na Mheshimiwa Waziri wanapozungumzia bilioni 47 kwamba ziko kwenye uratibu, kwenye udharura na kwenye uendeshaji; trilioni 1.3 ya Mheshimiwa Rais tulitumia bilioni tano tu kwenye kuratibu mkopo mzima wa trilioni 1.3 kwenye mkopo wa Covid.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni jambo jema kama mtachukua hatua kuhakikisha kwamba fedha hizi bilioni 17 au bilioni 47 zinaenda kufanya kazi iliyokusudiwa. Mheshimiwa Waziri haileti tija na haina mantiki kwa mwananchi yeyote yule awe ameenda shule au hajaenda shule katika mkoa wa bilioni 350 tunaenda kutumia bilioni kumi tu kupima ardhi ni sahihi? (Makofi)

Ni sahihi Mheshimiwa Waziri? Unaweza ukazungumza kwamba tunakwenda kusimika mitambo, tunaenda kujenga nyumba, si tunataka tuangalie kipaumbele chetu kama nchi ni kipi? Ni kutatua migogoro ya ardhi au ni kujenga nyumba? Kwa sababu nchi hii ina majengo ya halmashauri sehemu zote ambapo tunaweza tukatumia ofisi za halmashauri tukafanyia kazi hii, tukapima ardhi yetu hizo nyumba zikafuata baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna uhitaji mkubwa wa kutumia hela nyingi kwenye…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna haja ya kutumia fedha nyingi sana kwenye kujenga nyumba na hivi vitu vingine ambavyo mmevizungumza tukaacha kupima ardhi yetu.

Mheshimiwa Waziri kipaumbele cha Taifa na cha Mheshimiwa Rais ni kuona migogoro ya ardhi kwenye Taifa letu inaisha na sio kuhakikisha kwamba kila ofisi au kila mkoa au kila wilaya imejenga ofisi ya ardhi. Hiyo sio kipaumbele chetu, kwa sababu gani Mheshimiwa Waziri? Sitaki kuamini kwamba hadi dakika hii Maafisa Ardhi wa Wilaya wanafanya kazi chini ya miti maana yake wanamaeneo yenye ofisi. Kwa hiyo, huu mkopo ungekuwa na tija endapo ungeelekezwa kwa kiwango kikubwa kwenda kupima ardhi. Mheshimiwa Waziri tulikuwa wote pale Arumeru Mashariki… (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga pokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe Mheshimiwa Sanga taarifa kwamba kwa maneno ya msingi anayoyazungumza na kwa uzalendo ninaoujua kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Ardhi, nina imani kabisa kwa uzalendo nimeshafanya naye kazi, ninajua ushauri wa Mheshimiwa Sanga ataupokea Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga unapokea taarifa hiyo aliyokupatia Mheshimiwa Kingu?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea kwa moyo mzuri kabisa, kwa nini kwa sababu in their records wanajua kwamba Kamati ya Bajeti iliwashauri kuhusu mradi, Kamati ya Maliasili na Ardhi tunawashauri kuhusu mradi na sisi ni Bunge na sisi ndio Watanzania walioko nje tunasimama kwa niaba yao. (Makofi)

Kwa hiyo, tunachokizungumza hapa hatuzungumzi for bad, tunazungumza kwa jambo jema tu. Ngoja nikupe mfano kwenye Halmashauri ya Arumeru Serikali ilikopesha bilioni 1.6, Halmashauri ya Arumeru inaenda kuzalisha bilioni nane na imeshalipa na deni lote. Maana yake tukipima ardhi kwa kiwango kikubwa tutaingiza fedha nyingi kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ni Wizara mtambuka, hii Wizara inafanya parallel na Wizara ya Kilimo, hii Wizara inafanya parallel na Wizara ya Maliasili na Utalii. Leo hii Mheshimiwa Rais ameshusha mikopo ya kilimo kuja kwenye single digit kwa maana kwa asilimia tisa. Ukienda NMB, ukienda CRDB mikopo imeshuka, sasa mkulima hawezi kukopesheka kwa sababu ardhi yake haijapimwa. Kwa hiyo, hatuwezi kuwekeza bilioni 350 kwenye eneo ambalo linaenda kwa ajili ya kujenga ofisi, kusafiri, kununua nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi si kwamba haina magari, ina magari, ina ofisi, inavyo vyote. Nimuombe Mheshimiwa Waziri this is for good, this is for your record, utaondoka kwenye Wizara hii, utaandika kitabu chako kama Mzee Mwinyi alivyosema cha kwamba ulifanya jambo kubwa la kupima ardhi kwenye Taifa letu, kutoka kwenye asilimia 23 zilizopimwa kwa sasa ukafika zaidi ya asilimia 50 kwa kutekeleza Ilani ya CCM na kwa kuokoa mauaji yanayoendelea Tanzania kutokana na migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri tunaamini wewe ni mtu rahim, wewe ni mtu mwema, wewe ni msikivu, wewe ni mtu ambaye hutashupaza lolote kwamba sisi labda tuna nia mbaya kwa ajili ya hili, no this is our money, ni mkopo ambao wananchi wa Makete, mwananchi wa Bulongwa, mwananchi wa Iwawa, mwananchi wa Karagwe, mwananchi wa Mpanda, mwananchi wa wapi atalipa fedha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunasimama kwa niaba yao ili bilioni 350 zikapime ardhi na sio bilioni 47 ziende kwa ajili ya kusimika mitambo ya ofisi wakati nchi yetu ina ofisi kila kona.

Mheshmiwa Mwenyekiti, ahsante, naamini Mheshimiwa Waziri ametusikiliza, naamini kabisa nimewawakilisha wananchi, mawazo ya wananchi wa Makete na mawazo ya Watanzania kwamba ….

(Hapa kengele ililia kiashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FESTO R. SANGA: Kwa maslahi yao. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Festo.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.