Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kuendelea kutulinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la mipaka katika eneo letu la bahari, tuna changamoto kule Mkinga kwenye mpaka wetu na Kenya na changamoto hii ni ya miaka mingi. Mheshimiwa Waziri nafurahi uliwahi kuja Mkinga tukatembelea mipaka yetu kwenye ukanda wa ardhi, lakini tukaenda vilevile Kijiji cha Jasini kwenye ukanda ule wa baharini, uliziona changamoto zetu, nakumbuka ulifika kwenye nyumba ile upande mmoja ni Kenya na upande mmoja ni Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto yetu kubwa, hili la watu kujenga mpakani kabisa tunalisema kiutani utani hivi, lakini athari yake ni kubwa. Niliwahi kusema hapa kwamba wenzetu wa vyombo vya ulinzi vya Kenya wanafika mpaka ndani ya maeneo ya kijiji chetu wakiwa na silaha. Nikasema ni hekima tu za viongozi wa Serikali wakati ule vilisaidia tusiingie kwenye mgogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja tena leo kwa unyenyeku mkubwa naiomba Serikali yangu itusikie. Mwaka 1972 kilifanyika kikao cha kujadili jambo hili la mgogoro wa mpaka, tarehe 8 Mei kikao kilifanyika pale Mombasa; tarehe 4 Septemba, 1975 tulifanya kikao Dar es Salaam; tarehe 9 Julai, 1976 Mawaziri wetu wa nchi mbili hizi aliyekuwa Waziri wetu wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Ibrahim Kaduma na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Dkt. Munyua Waiyaki walisaini document ya makubaliano inayoonesha mambo kadhaa na document ile niliwahi kuileta Wizara na leo tena nitaiweka mezani ili iwe rejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na makubaliano yale kupitia document hii bado kumekuwa na chokochoko hizo. Vyombo vya ulinzi vya Kenya vikiingia kwenye eneo letu, wananchi wetu wa Jasini wanapoenda kuvua wakikamatwa baharini wakapelekwa Kenya kwenda kufunguliwa kesi, mali zao zikataifishwa. Sisi kama Taifa lazima jambo hili tulichukulie kwa uzito mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa mwneyekiti, maboya tuliyoweka ya mipaka kule baharini yameharibiwa, sitaki kusema ni makusudi, lakini nasema yameharibiwa. Wakati hali ikiwa hivi nataka niikumbushe tu au niiambie tu Serikali kwamba kwenye ukanda huu tuna leseni ya utafiti wa mafuta, kwenye ukanda huu tuna leseni ya utafiti wa madini, madini ya kimkakati baharini, lakini wakati hali ikiwa hivi kwenye mpaka wa Kenya na Somalia ambapo kuna dalili zote za kupatikana mafuta kuna mgogoro sasa hivi kule, sijui naeleweka? Tusingoje utafiti utuambie tuna mafuta halafu tushindwe kuyachimba. Tusiache kuchukua hatua watu wetu badala ya kwenda kuhukumiwa Kenya ikafika mahali vyombo vyao vikazamishwa baharini tukapoteza maisha ya watu wetu, nawaomba tuchukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili Mheshimiwa Waziri ni jambo ambalo nimelizungumza katika kipindi chote cha Ubunge wangu ni shamba la kwa Mtili, zaidi ya miaka kumi nalizungumza jambo hili. Miaka kumi na zaidi nalizungumza jambo hili, kuna shamba pale limetelekezwa na anayejiita mwekezaji, zaidi ya miaka 25 limetelekezwa. Huyo mwekezaji hayupo, wameshafariki, wapo tu watu wanasimamia kiujanja ujanja pale wakiwakodisha wananchi wetu kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilituagiza mwaka 2012 ikatumwa ilani ya kufuta shamba lile, lakini ikaonekana ina makosa mwaka 2017 ikatumwa ilani nyingine, mlipotupa shamba lile la kule kwenye kata kule ambapo kipo Kijiji cha Jasini, Kata ya Mahemboni kule nikawaambiwa kuna shamba lingine, tunaomba na hili mlishughulikie, aliyekuwa Waziri wakati ule Mheshimiwa Lukuvi akatuma timu kwenda kufanya uhakiki. Ikaonekana ni kweli, imetumwa ilani, baadaye ikaonekana imetumwa kimakosa kwa sababu kalitumwa kaeneo kadogo, ikatumwa timu nyingine kutoka Wizara ikaja kufanya tathmini, mkajiridhisha kwamba shamba lile limetelekezwa. Ikatumwa ilani nyingine, lakini baadaye ikaambiwa eti huyu jamaa miaka ya 1960 alichukua mkopo mahali huko nje, kwa hiyo tukatuma ilani nyingine kwenye hizo benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilani hizi zimepita zaidi ya miezi saba sasa au nane Waziri unalijua jambo hili,…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Nimekuja kwako ukaniambia watu wa mkoani wamechelesha, watu wa mkoani wamekamilisha kazi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kitandula naomba upokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mnzava.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kaka yangu mzungumzaji anayezungumza, pamoja na mchango wake mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kumpa taarifa kwamba jambo hili la kupeleka ilani, lakini utekelezaji hauonekani na tunakaa kwa muda mrefu kusubiri sio tu kwa yale mashamba ya Mkinga, hata Korogwe, shamba la Mwakinyumbi zaidi ya miaka saba kila siku ilani zinatengenezwa, utaratibu unakamilika, lakini ufutaji au ubatilishwaji wa miliki mpaka leo haujafanyika. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dunstan Kitandula unapokea taarifa?

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa sababu katika mkoa ambao una changamoto ya ardhi ya mashamba makubwa ya mkonge na mengine yaliyotelekezwa, Korogwe, Mkinga, Muheza tuna changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwneyekiti, ndugu zenu tunapowaambia tusaidieni, kwa hiyo nimeambiwa kwamba taratibu zote zimekamilika jambo hili lipo Wizarani, Wizara naomba mchukue hatua. Wapo watu kule wanazunguka zunguka wanakuja kutafuta fursa tuwaunge mkono kwa sababu yule mmiliki amejua hana ujanja, anataka kuuza eneo lile, tunaomba mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, ni lile ambalo kila mmoja wetu analisema, nimeisikiliza taarifa ya Kamati, wote tunajua Kamati ndio inafanya kazi kwa niaba ya Bunge. Kamati inaposema kwamba leteni hayo maamuzi kwenye Kamati tuyajadili wanasema kiustarabu tu kwamba hawaridhishwi kuna jambo linakwenda sivyo. (Makofi)

Naomba muisikie Kamati, tulijadili jambo hili, sisi sote ni viongozi tumeaminiwa na wananchi tusikilizane. Tukifanya maamuzi tuyafanye maamuzi kwa manufaa ya Taifa letu. Mheshimiwa Waziri ushirikishwaji unaujua ulivyo na tatizo, unajua timu ile ya Mawaziri ilipokuja Tanga mimi nilishiriki kikao kile kwa namna gani unajua. Sitaki niseme nilivamia, lakini unajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nasikia kuna timu huko Mkinga inaendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Naomba tuwashirikishe wananchi, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)