Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara kwa hotuba, lakini pia kwa ushirikishwaji, tulipata semina kama Bunge, lakini mimi binafsi kama mmoja wa Wabunge ambao Halmashauri zetu zitanufaika na Mradi wa Kuboresha Umiliki wa Ardhi maarufu kama hakimiliki salama, nilishiriki pia katika semina ya kujengewa uwezo kuhusu mradi huu. Napongeza pia uwepo wa banda la Wizara hapa Bungeni, imekuwa ni fursa nzuri kupata huduma binafsi lakini pia kupata huduma kwa niaba ya wananchi na hata ndugu, jamaa na marafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala machache ya kuchangia kama ifuatavyo; kwanza ni kuhusu Mradi wa Miliki Salama; nilipohudhuria semina ya kwanza kuhusu mradi huu, niliona hoja kutoka kwa Wajumbe wa Kamati kwamba fedha nyingi inaenda kwenye masuala ambayo it is more of administrative badala ya kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mengi zaidi, kwamba ujenzi wa majengo, uimarishaji wa mifumo na kadhalika sio masuala ya muhimu kuliko kupima vijiji vingi zaidi na kutoa hati nyingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo napongeza kwamba sasa vijiji vimeongezeka kutoka 250 hadi 500 na pia hati na leseni za makazi kutoka laki tano hadi milioni moja kwa kila kipengele. Kwa hiyo, yapo maeneo ambayo mawazo yamezingatiwa. Hata hivyo bado kuna maoni na malalamiko kwamba ilibidi tuongeze zaidi eneo la kupimwa, maoni ni kwamba kwa nini fedha nyingi ziende kwenye majengo na kuimarisha mifumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, suala hili ni muhimu sana, ujenzi wa ofisi na kuimarisha mifumo utakuwa ni jambo la kudumu, itatumika kwa ajili ya mradi na pia hata baada ya mradi kukamilika majengo kwa maana ya ofisi na mifumo itaendelea kutumika, kwa hiyo ni wajibu wa Serikali kufanya ushirikishwaji kuanzia ngazi za Mitaa/Vijiji, Kata na Halmashauri ili kuleta uelewa wa pamoja na ownership ya mradi. Nafahamu kwamba kutafanyika vikao kuanzia ngazi ya CMT katika Halmashauri, lakini nashauri kuwashirikisha Waheshimiwa Madiwani katika kila ngazi. Vikao vya ngazi za chini katika Mitaa/Vijiji, ni muhimu ushiriki wa Madiwani uwepo. Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo pamoja na kuwa jambo hili ni la Serikali, nashauri ushirikishwaji wa viongozi wa CCM kama observers, kwa mfano katika vikao vya ngazi ya Halmashauri kwa maana ya Madiwani ni muhimu Mwenyekiti na Katibu wa Chama katika Wilaya/Halmashauri husika wakaalikwa kama watazamaji ili tu kujua from the horses mouth maana na faida ya mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kupunguza upotoshwaji katika level zote. Kuhusu gharama za ujenzi wa majengo ya ofisi na kuimarisha mifumo, nadhani ni suala ambalo Wizara inabidi ifafanue kwamba huu ni msingi imara katika kuboresha na kuimarisha sekta ya ardhi kama sehemu ya kufikia hatua sio tu ya kumaliza migogoro, lakini pia kuhakikisha mipango ya matumizi bora ya ardhi inakuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango kabambe katika Mji wa Mafinga/industrial park; kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 37, Mji wa Mafinga uko katika hatua za mwisho kukamilishwa, nashauri na kupendekeza jambo hili ambalo mimi binafsi nimelisukuma sana toka nilipochaguliwa mara ya kwanza mwaka 2015 wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Mipango Miji Profesa Lupala, kwa kushirikiana na Ndugu Mahenge na Dean of Students wa Chuo Kikuu cha Ardhi tulianza kushirikiana na Wizara katika hatua za mwanzo za kukusanya data. Ninaomba Wizara itusaidie tukamilishe suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili ninaomba Wizara kama ambavyo imekuwa ikiniahidi katika mazungumzo ya siyo rasmi na viongozi wa Wizara, tusaidiwe kukamilisha ndoto ya Wana-Mafinga kuwa na industrial park, tayari tuna eneo tumetenga ekari 750 kwa ajili ya industrial park na mara kadhaa tumezungumza na Kamishna Mathew juu ya jambo hili. Namshukuru Kamishna Mtui tulianza naye lakini pia hata alipokuja Kamishna Minja amelipokea vizuri sana. Ushauri wangu, kama ni kwa utaratibu wa revolving fund au kwa namna Wizara itakavyoona inafaa basi tulitekeleze suala hili kwa kuzingatia kuwa kuna potential kubwa ya viwanda vya mazao ya misitu, na kama sehemu ya jitihada za kufanikisha suala hili, wenzetu wa EPZA walitembelea kuona potential hiyo na hasa kwa kuzingatia pia kuwa tupo kando ya highway ya TANZAM ambayo ni kiungo muhimu sana katika biashara kati ya Tanzania na nchi za SADC na hasa DRC, hivyo industrial park inaweza pia ikatumika kama logistics center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Wizara tulipe suala hili uzito. Huko kwingine mnakosema kuwa fedha za revolving fund zimetumika sivyo, it won't be in Mafinga.

Kuhusu Baraza la Ardhi Mufindi, wanasema haki iliyocheleshwa ni sawa na haki iliyokoseshwa, wananchi wa Mafinga/Mufindi kilio chao ni huduma ya Baraza la Ardhi, issue ilikuwa ni majengo na sasa issue naambiwa wajumbe wameshapatikana, tatizo ni Mwenyekiti. Kwa hiyo, wananchi wanalazimika kwenda Iringa Mjini, naomba na nashauri tupate Baraza la Ardhi kwa ajili ya wananchi wa Mafinga/Mufindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.