Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini pia nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuwa muumini mzuri hususan kwenye masuala mazima ya uhifadhi, lakini na utunzaji wa mazingira, lakini ni dhahiri kwamba uhai wetu kwa ujumla unategemea sana vyanzo vya maji, lakini pia viumbehai wakiwemo wanyamapori na mimea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango ya Wabunge imeelekeza zaidi katika Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini pia na Wizara ya Ardhi. Sisi ni wadau wakubwa kabisa kwenye maeneo mengi yenye migogoro hususan maeneo ya hifadhi na tunatambua changamoto hizi zipo na ndiyo maana ilimpelekea Mheshimiwa Rais kuunda Kamati ya Mawaziri nane kwenda uwandani kuchunguza kina na kadhia wanayoipata wananchi hususan kwenye migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niendelee kuwapongeza Wabunge kwa namna ambavyo wameendelea kuwa wavumilivu. Nimejaribu kuongea hapa kwamba chimbuko la migogoro hii ni la muda mrefu. Tunakumbuka tangu Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwa inaongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kulikuwa kuna migogoro hii na aliweza kuunda Kamati ya Mawaziri nane wakaenda uwandani wakaanza kuchunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeenda uwandani kwa ajili ya kutekeleza na ninyi mtatambua mwaka jana tumezunguka Mawaziri, tumepita kila sehemu kuangalia hizi changamoto. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge changamoto hizi ni za muda mrefu na utatuzi wake unahitaji sana busara, lakini na hekima lakini na tuvumiliane kwa sababu unapoenda unakuta mwenzio kaingia huku inahitaji busara sana kutatua changamoto hiyo na ndiyo maana Mheshimiwa Rais alielekeza kabisa kwamba hahitaji kuona taharuki inatokea katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumeenda hatua kwa hatua na pale ambapo kuna kuwa kuna mabishano, Serikali inaangalia, kama kuna umuhimu sana wa kung’ang’ania hili eneo basi kuna maslahi mapana ya Taifa letu, lakini pale ambapo tunaona tunaweza kuachia, basi tunakaa tunazungumza na Mheshimiwa Rais ameweza kuachia takribani vijiji 975 vilivyokuwa vimesajiliwa ndani ya hifadhi vyote ameviachia. Tumpongeze sana na tuendelee kumtia moyo kwa sababu migogoro hii ni mingi, lakini tunaenda kuimaliza kabisa na Mheshimiwa Waziri wangu ameahidi kabisa kabla ya bajeti ya Maliasili tutakaa na Waheshimiwa Wabunge wote wenye migogoro tutajadiliana eneo kwa eneo ili tufikie mahali migogoro hii tuimalize maana lengo la Serikali ni tutembee pamoja na siyo tena kuendelea na migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuzungumzia suala la Mbarali ambalo lilijitokeza jana na suala kubwa hapa ni kwamba mchakato mzima wa kuainisha hii mipaka tayari umeshakamilika isipokuwa tunachotarajia sasa hivi ni kuleta kwenye Bunge lako hili tukufu ili liweze kuridhia marekebisho ya Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kabla ya kuisha Bunge hili tayari azimio hili litaletwa katika Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuwaondoe shaka Wanambarali, tuwaondoe shaka Wanambeya ambao wamekuwa wakishughulika na hizi shughuli za kilimo hususan katika maeneo ambayo yanazunguka Bonde la Usangu kwamba tutakamilisha na kila mtu ataelewa mipaka yake na wale ambao wameainishwa kwamba wataainishiwa mipaka yao basi wataweza kuiona kwa uharaka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumejitokeza kwenye suala hili la Nyatwali. Suala la Nyatwali malengo ya Serikali ilikuwa ni kupunguza migogoro ya wanyama wakali na waharibifu. Kama ambavyo umekuwa ukisikia, tumekuwa na changamoto kubwa sana ya wanyama wakali na waharibifu kwa hiyo, tunajaribu kuongoa zile shoroba ambazo tunaweza angalau tukaruhusu wanyama pia nao wakaweza kupita katika maeneo ambayo kusiwe na mgogoro kati ya jamii pamoja na wanyama wakali na tukitambua kwamba Serengeti ni hifadhi maarufu na imekuwa ya kwanza inaongoza kimataifa kwa maana ya uhifadhi bora na ni chanzo kikubwa cha mapato katika sekta ya utalii. Hivyo tunaendelea kuwaomba Wananyatwali kwamba Serikali imeendelea kusikia maombi yao, lakini tunashukuru kwa sababu wamekubali kwa hiari kwa maana tulienda kuzungumza nao na tukawaeleza kwa nini tunaenda kufanya hivyo. Lengo kubwa ni kuokoa maisha ya wananchi. Hakuna mtu anayefurahi kusikia kila siku kilio cha wananchi wanakufa kwa sababu ya wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda wangu umeisha naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)