Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kidogo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Masauni na Naibu wake Mheshimiwa Sagini na timu yao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuilinda nchi yetu na kulinda mali za wananchi na kwa kuonyesha msimamo wa kutetea wananchi wake hususani nikitolea mfano kwa jinsi alivyochukua hatua za haraka kwenda kupeleka usafiri Sudani Kusini na kuwachukua wanafunzi wa Tanzania ambao walikuwa kule na kuwarudisha nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi pia kwa Trafiki wa Zanzibar, Trafiki wa Zanzibar wamekuwa trafiki marafiki, Trafiki wa Zanzibar unaweza ukamfuata hata kama umepotea njia akakuelekeza, nenda njia fulani. Trafiki wa Zanzibar anaweza akakusimamisha, akakwambia usipite njia hii ina foleni pita njia hii. Trafiki wa Zanzibar anaweza akasimama kwenye zebra akasimamisha magari akatoka mwenyewe kwenda kushika wanafunzi au watoto kuwavusha mpaka upande wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengine tumeona trafiki yuko kwenye zebra lakini haangalii kusimamisha magari ili watu wapite macho yake yako kulia anaangalia daladala linalokuja litafanya nini ili nipige mkono. Kwa hiyo hilo pia Mheshimiwa Waziri aliangalie, kuna baadhi ya matrafiki hawako sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Trafiki wa Chanika, Chanika kuna kiongozi anakaa kule, si vizuri kumtaja kwa nafasi lakini huwa anakwenda, lakini kituo kile hakina raider ya kuongoza misafara, unakuta kwamba wanatumia tu mikono na taa na wakati kiongozi mkubwa sana huwa anaenda kule. Sasa naomba Wizara hii iangalie kupeleka raider kwa Polisi wa Chanika, barabara ile ni kubwa, ina maroli mengi ina mabasi mengi, sasa ni vizuri tuangalie usalama zaidi wa viongozi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe pongezi kwa Jeshi la Magereza kwa sasa hivi wanatumia vizuri nafasi za wafungwa. Zamani tulikuwa na kazi tu ya kuwalisha na kuwavalisha nguo kazi hazionekani, lakini sasa hivi tumeona kwamba maofisi mengi na vituo vingi vya Magereza majengo yanajengwa kuna ma-hall kuna nini, magereza wanafanya kazi unajua kweli huyu sasa akitoka hapa akashajifunza kitu anaenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaniona mtu wa pongezi sana, natoa pongezi sana kwa sababu haya yanayofanyika yanaonekana, nipongeze Jeshi la Uhamiaji katika utaratibu mzima wa utoaji Passport kwa sasa hivi kwa maana hati za kusafiria. Zamani ukitafuta hati ya kusafiria yaani unahangaika kama unatafuta kumtoa mtu figo ukaweke kwako, sasa hivi Passport ukisema dakika mbili unaambiwa baada ya muda fulani njoo uchukue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeliona hilo Dodoma, tumeliona hilo Dar es Salaam japo kuna maeneo mengine yana matatizo kidogo, basi niombe wawasaidie hususani katika masuala ya kompyuta ikitolewa mfano katika Mkoa wa Iringa, kompyuta zao ni za kizamani, wawarekebishie wawape za kisasa na maeneo mengine ambayo bado yana kompyuta za kizamani, ili waweze kufanya kazi zao vizuri, watu wapate Passport mapema. Nasema hivi kwa sababu kuna wakati mwingine Passport unapata kidharura dharura, siyo kwamba kila anayechukua Passport kwa ajili ya sterehe zake. Kwa hiyo niwapongeze kwamba wameboresha kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi vile vile kwa Trafiki wa Makumbusho Dar es Salaam, yule kijana anajituma, ile kazi inaonekana kaipenda na ameingia pale kwa dhati, anaongoza magari kwa mbwembwe, watu wanapita pale wanamtunza, lakini nafikiri kuna wengine wameenda kwenye upolisi hawana jinsi ili mradi tu niende nizibe pengo. Kwa hiyo napenda hao mapolisi kweli wanaoenda huko waangalie, huo upolisi wanautaka au wamekwenda tu kwa sababu hamna kitu kingine cha kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa polisi wetu pamoja na pongezi zote tunazowapa, kuna maeneo ambayo wanatupa kero, unaanza na king’amuzi, basi akimshika mmoja mwenye tisini yatapita magari hata ishirini yote yanaonyesha king’amuzi tisini tu, tisini hiyo hiyo haibadiliki wanaoneshwa hiyohiyo. Kama hivyo ving’amuzi vibovu vikatengenezwe au vinunuliwe vipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wana mchezo wa kujificha hawa, utaona tu ghafla kakurupuka kwenye mihogo, sasa wewe Bwana Shamba? Uko kwenye mihogo ulifuata nini? Kaa barabarani tukuone kama kuna tatizo tusimame tukwambie, bwana tusaidie hapa, kuna mwingine anamtaka trafiki amuulize hivi kutoka Gairo mpaka manyoni ni kilomita ngapi, lakini yeye yuko kwenye mihogo ghafla tu anaingia ili mradi tu uvunje sheria. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, trafiki wana ucheleweshaji usiokuwa na sababu, wanaweza wakasimamisha mabasi ya abiria, malori na kadhalika, halafu mwenyewe anakaa anachati pale anasubiri dereva au konda atoke amfuate pale akamuulize. Sasa wanawatia hasira madereva, wakitoka pale wanatoka spidi, matokeo yake tunasababisha ajali mbele. Ni afadhali anaposimama aongee naye palepale wamalizane palepale kama kuendelea na safari aendelee kama ni kumwandikia amwandikie badala ya kumsimamisha kwa muda mrefu na kumpotezea muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matrafiki wengine ni walevi, asubuhi tu analewa. Mimi nimekutana naye Morogoro, kanisimamisha nimesimama, kaniuliza hii namba ya wapi nikamwambia hii namba ya usajili wa Zanzibar, akauliza nitajuaje kama Zanzibar? Dereva wangu akamjibu akamwambia si umeona bendera hiyo ya Mbunge? Akasema, aah, bendera hata mimi ninayo kiunoni, lakini kutokana na harufu yake nilivyomskia nikajua mlevi nikamwambia achana naye tuondoke. Sasa walevi kama wale Wizara iwaangalie asubuhi asubuhi isiwe inawapangia kazi huko barabarani, wanatuletea vituko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna kazi nyingine ambazo zinakuwa kioo cha jamii wakiwemo Mapolisi, Wanajeshi kwa ujumla kuna Walimu, kuna Madaktari hata Wabunge yaani ni kazi ambazo zinaenda watu wanakuangalia kioo cha jamii. Sasa tunaposikia Polisi yuko katika ule mchezo kwa kweli wanatutia mashaka. Unasikia mtoto kalawitiwa au kabakwa, unamchukua unataka umpeleke polisi, halafu unakuja unasikia polisi mwenyewe ndio walewale, wanatukatisha tamaa na watatugombanisha kwa sababu ukishamchukua mtoto aliyelawitiwa ukampeleka polisi, kumbe polisi mwenyewe ndio yuleyule anakuona mbaya wale waliompeleka huyo mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maadili kwenye Jeshi la Polisi na wengineo liangaliwe kwa kina, kwa sababu licha ya kutia aibu, lakini wanatukatisha tamaa, halafu baadae wanatuambia mbona mnamalizana wenyewe kijamii jamii hukohuko nyumbani, sasa huko polisi tukienda na mambo yenyewe ndio hayo inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote niseme kabisa pongezi nyingine kwa Waziri na Mheshimiwa Rais, nyumba za askari sasa hivi nyingi zimeboreshwa tofauti na zamani. Zamani mpaka tunajiuliza yaani chumba kimoja wanapishana kwa mapazia unajiuliza wanapataje watoto pale, lakini sasa hivi tunashukuru nyumba za maaskari zimekuwa nzuri, zinaheshimika, wamewapa staha. Naomba Wizara waongeze nguvu yale maeneo mengine ambayo hayajapata nyumba, basi wajengewe waendelee kuwa na staha. Pamoja na hayo bado napendekeza vifaa zaidi vinunuliwe vya kisasa kwa ajili ya askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)