Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya, lakini niwashukuru na Wabunge wenzangu wote waliokuwemo katika Bunge hili Bunge Tukufu hii leo na wakaweza kunipigia makofi kwa wingi hivi saa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wangu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji wake mkubwa anaoufanya katika Wizara zake zote. Mheshimiwa Rais Mwenyezi Mungu amjalie huyu bibi amuondolee kila la shari, amjalie heri, amuondolee nakama, husda, ubaya, amuondolee kila aina ya uadui katika kiwiliwili chake na katika safari zake na ampe heri na busara katika uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea niwapongeze Mawaziri wangu wote, Mheshimiwa Masauni nampongeza sana kwa Wizara hii ni Wizara yake, Wizara mama amejaa na hakuna Waziri mwingine katika Wizara hii kama si yeye Masauni. Pia nimpongeze na Naibu wake hivi sasa ambaye ni Mheshimiwa Sagini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Mheshimiwa Sagini, nilimwomba hapa katika swali langu tuende kwenye site zangu za Mkoa wa Kusini Unguja. Mheshimiwa Sagini hakurudi nyuma, alisema nitakwenda na wewe na nitakwenda kufanya kazi moja baada ya moja. Nimshukuru Naibu Waziri Sagini, tulikwenda Kizimkazi na tukazifanya zile kazi za Kizimkazi. Hatimaye leo hii katika utekelezaji wao uliosomwa sasa hivi na Mheshimiwa Waziri nimeona mafanikio ya Wizara yetu tuliyokwenda kule na Mheshimiwa Sagini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sagini tulikwenda kuangalia kwanza Kituo cha Kizimkazi, kilikuwa kinajengwa upya na kituo kile kwa bahati kimeshamalizika na hivi sasa kinaendelea kufanya kazi, isipokuwa tu kituo kile kina wafanyakazi ambao walitolewa katika kituo kingine wakapelekwa kituo kile bado hawajapata mafao yao. Wamepelekwa pale kufanya kazi hawajapata mafao yao na mpaka sasa hivi wanalalamika sana. Hawajapata maposho yao ya kutoka kule na kuja kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wafanyakazi hawa waliokuwa wamepelekwa pale mafao hawajapata na wanataka mafao yao. Kwa hiyo niomba Serikali, wale wafanyakazi waliopelekwa pale wa polisi kwenda kufanya kazi katika Kituo cha Kizimkazi, wapewe mafao yao na wapewe mahitaji yao yanayohusika katika kuhamishwa kule kuja pale ili waweze kufanya kazi vizuri. Naomba sasa hivi Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind hapa, atuambie kwamba lini utawapatia mafao yao ili na sisi wananchi tuweze kufaidika kwamba wale watu tayari tarehe fulani watapewa mafao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kuna kitengo cha wanawake katika Wizara…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwantumu, kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka tu kumpa mama yangu kwamba Mheshimiwa anayechangia kwamba si Kizimkazi tu wanaaskari wanaodai mafao. Kule Hai kuna wanaodai arrears, posho zao ambazo ni stahiki zao za msingi. Kwa hiyo nilikuwa namwongezea tu kwamba Mheshimiwa Waziri akatazame stahiki za askari wa majeshi yetu yote ili wawalipe, wanafanya kazi kubwa na muhimu sana kwa Taifa letu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Mwantumu taarifa unaipokea?

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa mikono miwili mwanangu huyo. Kwa hiyo kadhia zinatoka hizo kwa wengine baadhi ya vituo vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani, kuna Kitengo cha Polisi cha Akinamama, kitengo hiki akinamama wanapokuwa wajawazito wengine wanakuwa wanachukua likizo zao mapema, lakini kabla ya kujifungua bado hawa watu wana likizo zao, mara moja ile likizo inakatwa, ikishakatwa ile likizo anapewa likizo yake ya uzazi siku zake arobaini akimaliza arejeshewe likizo yake ya kawaida? Basi anakuwa harejeshewi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kadhia ipo inayofanyika katika kitengo hiki na kipo hiki kitengo na ndio maana mimi hapa sasa hivi nakizungumzia. Kwa hiyo tunaomba akinamama waliokuwepo katika kitengo hiki wakimaliza likizo zao za uzazi wapewe likzo zao za stahiki zao ili waweze kuwalea watoto wetu vizuri, maana wale tunawategemea keshokutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea, kuna vituo tulivyokwenda na Waziri Sagini kule Makunduchi Zanzibar, tulikwenda kuangalia Kituo cha Polisi daraja C ambacho ni cha Makunduchi kina thamani ya kujengwa milioni mia moja na kumi, lakini pia kuna Kituo cha Polisi cha Dunga C milioni mia moja na kumi, lakini kuna Kituo cha Polisi daraja C Dunga Mitini, Kusini Unguja kina shilingi milioni 48.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo hivi hapa nilikuwa navipigia kelele sana katika Bunge lako hili Tukufu, kwamba hivi vituo vilikuwa vibovu na vichafu na sasa hivi bado hatujapata mustakabali mzima wa vituo hivi kujengwa kwake, isipokuwa nasikia tu Kituo cha Makunduchi kilishaanza kuzungushwa mabati ndio utekelezaji ambao tunautaka, kilishazungushwa mabati ili kwa kuendelea vituo hivi viweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, hivi vituo vitekelezwe vizuri na vijengwe vizuri ili wale polisi na wao wapate vituo vizuri vya kufanyia kazi zao kwa sababu wanaazimaazima vituo wanakaa. Kama kule Makunduchi kuna nyumba nyingine mbovu, zinavuja, nazo zitengenezwe, Kituo cha Dunga wamehamia Dunga huku wanataka na wao wamaliziwe kituo chao ili warudi kule kwa kawaida ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea, kuna milioni 110 na kuna milioni 44 hizi ambazo tutakazokwenda kujengewa vituo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwantumu, malizia mchango wako.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia, kuna vituo vinataka kujengwa ma-hal,l kwa hiyo nashukuru kwamba vimeonekana na pia vitakwenda kujengewa hizo kumbi za kuweza kufanya mikutano yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina zaidi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwa Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Ahsante sana. (Makofi)