Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa ningependa kuipongeza sana Serikali kupitia Mheshimiwa Rais, Doctor Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao Serikali inaendelea kufanya kwenye Jeshi la Zimamoto. Tarehe 22 Mwezi wa Tano nikiwa pale Bukoba tulipata ajali la moto kwenye Soko letu la Bukoba na kipekee niwapongeze sana Wanabukoba wenzangu pamoja na Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha ya kwamba moto ule unazimwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yote yaliwezekana kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umeendelea kufanyika kwenye Jeshi la Zimamoto. Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, maana Serikali imeshatuma shilingi milioni 600 ambazo zinalenga kujenga kituo cha zimamoto kwa pale Bukoba na kituo hiki kitajengwa katika Kata ya Miembeni pale Bukoba Mjini. Kwa hiyo nami kama Mjumbe wa Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama naendelea kuafarijika sana kwamba yale ambayo tunayashahuri yanafanyiwa kazi na uwekezaji mkubwa unaendelea kufanyika kwenye Jeshi letu la Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika bajeti hii utakuwa katika maeneo matatu na nitaanza kwanza katika eneo la idadi ya mahabusu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano kwenye magereza yetu ikiwemo; moja, kutoa maelekezo kwamba mtu asipelekwe mahabusu mpaka upelelezi uwe umekamilika lakini pili, kuunda Tume ya Haki Jinai. Pamoja na hayo hivi sasa kwa takwimu za jana idadi ya mahabusu ni 12,012 na Serikali inatumia takribani milioni 640 kulisha mahabusu hawa kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni 640 kila mwezi zinaenda kulisha mahabusu hao ambao hawafanyi kazi hivyo hawawezi kuzalisha chakula ambacho wanakula. Asilimia kubwa kati ya hawa ni petty offenders kwa maana ya kwamba ni wale wenye makosa madogo madogo yenye dhamana lakini dhamana hiyo inakuwa haipatikani. Ili tuweze kuhakikisha kwamba tunaweza kupunguza msongamano kwenye magereza yetu, mimi napenda kupendekeza mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napendekeza, Wizara itupe taarifa tokea Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyotoa maelekezo kwamba mtu asiende mahabusu mpaka upelelezi umekamilika. Je jambo hilo limefanyika kwa kiwango gani? Ni muhimu sana tupate taarifa kamili ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Jeshi la Magereza lifanye tathmini wale mahabusu ambao wako nao 12,012 kati yao ni asilimia ngapi ya mahabusu hao wana makosa yale madogo madogo yenye dhamana kwa maana ya petty offenders.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa tatu ni kwamba kumekuwa na changamoto kubwa kwamba mtu anakaa mahabusu kwa miaka mingi takribani miaka miwili, mitatu, mwaka na kadhalika lakini pale ambapo hukumu yake inatolewa ule muda aliokaa mahabusu hauhesabiki kama sehemu ya kifungu. Jambo hilo badala yake limeachiwa utashi wa Jaji ama yule ambaye anatoa hukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitarejea hivi karibuni Mfalme Zumaridi kule Mwanza, Jaji alivyotoa hukumu yake alitoa maelekezo kwamba sehemu ambayo ameshakaa mahabusu iwe ni sehemu ya kifungo na baada ya kauli hiyo kilichofanyika yule Mfalme Zumaridi alikaa magereza mwezi mmoja tu, kwa sababu ule muda ambao alishakaa mahabusu ulihesabika lakini jambo hili haliko uniform. Jambo hili linategemea wengine wanapata wengine hawapati, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi yetu, kwa sababu inaweza ikaleta vurugu na wale ambao wako mahabusu wakajiona kwamba kuna wengine wanahaki zaidi kuliko wenzao. Kwa hiyo, mimi napendekeza kuwe kuna uniformity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni hapo kwenye suala la kupunguza msongamano wa magereza, napendekeza ya kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ije na Mswada wa Sheria ya Dhamana (Bail Act). Kwa sababu hivi sasa masuala ya dhamana ni kifungu kimoja tu katika sheria ya Mwenendo ya Mashauri ya Jinai (The Criminal Procedures Act) na ni kutokana na hivyo kumekuwa na mkanganyiko na loop holes nyingi ambazo zinapelekea kuchelewesha haki ya dhamana na haki jinai kwa ujumla wake. Kwa hiyo, mimi napendekeza Wizara hii ituletee Muswada wa Sheria ya Dhamana kwa maana ya Bail’s Act.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa eneo langu la pili nitaongelea suala zima pale Mkoani kwetu Kagera kwenye Magereza ya Bukoba. Tuseme mahabusu au magereza ambao wanaumwa ambao wanapata rufaa ya kuja hospitali ya Mkoa wanawekwa kwenye lile Gereza la Bukoba na wengine wanapata Rufaa kwenye Bugando, lakini Gereza la Bukoba halina gari la kuwasafirisha wafungwa hawa na mahabusu pale ambapo wanaenda kupata matibabu, badala yake wanawasafirisha kwenye magari mengine, magari ya kawaida pamoja na raia. Kwa kipekee sana naomba Wizara ione namna gani ambavyo itapatia Magereza ya Bukoba Mjini iweze kupata gari ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho kutokana na miundombinu ya Mkoa wetu wa Kagera na hali ya hewa naomba sana Mkoa wa Kagera uangaliwe kwa jicho la kipekee, ili tuweze kupata magodoro, blanketi na sweta za kutosha. Maana hivi sasa katika magereza zetu nane za mkoa wa Kagera tuna takribani wafungwa na mahabusu zaidi ya 1900 na lakini tuna upungufu wa magodoro masweta na mablanketi kwa zaidi ya 15,000. Kwa hiyo, naamini sana kupitia ombi hili Magereza za Mkoa wa Kagera zitapata kipaumbele pale ambapo Jeshi la Magereza litaweza kutoa vifaa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na naipongeza sana Wizara, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Hamad Masauni, Mheshimiwa Naibu Waziri Sagini kwa kazi kubwa ambayo wanafanya na Viongozi wote wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)