Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana, kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Awali ya yote kwanza nitambue mchango mzuri na kazi, ufanisi, tija pamoja na uzalendo unaofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Pia nitambue na nipongeze jitihada za Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye hivi karibuni siku ya Muungano Aprili 26, aliweza kutoa msamaha kwa wafungwa 376. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa na tabia ya kuingia moja kwa moja kwenye kero na kuzitatua. Mimi kwa hilo nampa hongera lakini si kwamba tu aliwaondoa wafungwa na kupunguza msongamano bali aliweza kupunguza gharama za matumizi ambazo kwa mwaka ni bilioni 338 ambazo zinatumiwa na hao tu 376.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tatizo la msongamano wa wafunga magerezani bado halijapatiwa jibu sahihi, ndiyo maana naona Mheshimiwa Rais alielekeza nguvu zake kule ili kuonyesha njia ili na sisi wenye dhamana tuweze kupita huko kuona namna gani tunaweza kwenda kupunguza msongamano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi inayotakiwa kwa wafungwa ni 29,902 lakini iliyopo sasa ni 32,140, tayari tumezidiwa. Tusiende tu kukimbilia kwenye kujenga magereza lakini tutafute mwarobaini. Sisi tuliona kwamba Bodi ya Parole inaweza ikawa mwarobaini lakini zipo Sheria katika Bodi ya Parole ambazo zinakwamisha wasiweze kuchukua hatua. Sheria hizi zinatakiwa bodi ikae iweze kuzichakata ili kuona sheria rafiki zitakazosaidia ili kuweza kupunguza msongamano wa wafunga magerezani. Nikisema hivyo nirejee kipo kifungu ambacho kinaonyesha kwamba lazima aliyemshtaki mtuhumiwa aweze kuridhia na kusaini ndipo mtuhumiwa aweze kupata msamaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mambo mengi, wanaweza kuwa na chuki, anaweza kuwa na hasira na asikubali. Kwa hiyo, wale watu wanabaki magerezani. Kwa hiyo kwa kiipengele hicho niombe Bodi ya Parole itakavyokaa ianze kuchakata sheria ziwe rafiki kwa ajili ya kupunguza msongamano kwa wafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msongamano huu wa magereza unajumlisha Wahamiaji haramu. Bunge liliopita nilisimama kwenye Bunge lako Tukufu nikazungumza ni namna gani Wahamiaji haramu wanakomba pesa za walipa kodi na kwenda kukaa kwenye picnic, kwa sababu watu hawa hawawezi kufanya kazi ya uzalishaji. Tayari wamemaliza vifungo vyao, tuna wahamiaji haramu 2,609 wako wamekaa wanastarehe wanakula chakula, hawa wahamiaji haramu 2,609 wanatumia pesa za walalahoi, pesa za walipa kodi, pesa za watu wadogo wadogo ambao wanalazimishwa kulipa kodi wasipolipa kodi watachukuliwa hatua. Sisi tunachukua hatua gani kuwaondoa wahamiaji haramu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahamiaji hawa haramu kama ilivyosema Kamati, wanatumia pesa nyingi kwa mwaka, wahamiaji hawa haramu wanatumia bilioni 2.3. Bilioni 2.3 ni pesa nyingi, ni pesa nyingi ukilinganisha na maisha yetu ya sasa, fedha hizi zingeweza kuelekezwa kwenye madarasa zingejenga madarasa 117 na watoto wetu wangekaa sehemu salama, zingeweza kuelekezwa magereza huko huko zikaenda kwenye miradi ya maendeleo nao magereza wangeweza kufanya mambo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itumike busara wakati Waziri anakuja ku-wind up aweze kuonyesha dira ya wahamiaji haramu, kwa sababu zipo hapa Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mambo ya Ulinzi, kaeni muone namna gani mnakwenda kutoa hii kansa ambayo imeenea kwenye Nchi yetu. Nikisema hayo naenda ku - reflect kwenye bajeti ya magereza, bajeti yao ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Maendeleo mwaka 2022/2023 wameomba shilingi 21,300,069,000. Hizi zilitengwa na Bunge, lakini fedha walizopata ni shilingi milioni 100. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hee! Loh!

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Magereza wana shughuli za kufanya, wana rasilimali watu, wanaweza kufanya mambo makubwa, wamepewa shilingi milioni 100 sawa na 0.46%. Hatuwezi kwenda hivi. Kama tunawapa wahamiaji haramu shilingi bilioni mbili sawa na 20%, tunaachaje kuwapa hawa wazalishaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zetu tumewekeza, tunalisha watu wanaopita wanakuja kukaa hapa wanapunga hewa, tunaacha kwenda kuzalisha. Watu wa magereza waliweka mikakati 2020 wakasema wana vituo tisa wanaweza kuzalisha mazao mbalimbali, wakapunguza burden ya mafuta ya kula, wakapunguza burden ya mfumuko wa bei. Tungewapa fedha wakalime. Wana ardhi, wameziainisha vituo tisa. Tumeshindwa kuwapa fedha lakini fedha za kulisha wahamiaji haramu, wapita njia tunazo. Kiko wapi cha kumpa mtoto wa kambo chakula ukamwacha mtoto wako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba lichukuliwe kwa u-serious kabisa, wakati Mama yetu anazunguka huku na kule ughaibuni kutafuta fedha, sisi tunakwenda kulisha watoto wa jirani wanashiba sisi tunalala njaa. Naomba fedha inayotengwa na Bunge kwa ajili ya Bajeti za Wizara hii na Wizara nyingine kwa maslahi ya Taifa zikatolewe kwa wakati. Hazitolewi. Ukiwapa shilingi milioni 100, wakanunue nini katika shilingi bilioni 21? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyoongea leo, wako tu wako hapo. Vyombo hivi haviwezi kulalamika kutokana na nature yao ya kazi, lakini sisi tunakuwa midomo yao, tunawasemea. Wanafanya kazi kwa kinyongo, hawafanyi kazi vizuri, wanafanya kwa kinyongo lakini ni kwa sababu wamejawa uzalendo, wanafanya kazi hii na Taifa linaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Magereza ardhi waliyonayo ni ekari 19,770. Iliyotumika ni 3,850 sawa na 19% halafu mnalalamika hawa Magereza wamekuwaje? Wapeni hela tuwapime kwa kazi zao. Tuwape fedha wakafanye kazi. Wana uwezo mkubwa, wana ufanisi mzuri, wana uzalendo wa kutosha, wanaweza kuliletea tija Taifa, lakini wameshindwa kufanya kwa sababu tu hawana fedha za maendeleo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. muda wako umekwisha. Tunashukuru sana kwa mchango wako.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namalizia kwa kusema, Waheshimiwa hawa Jeshi la Magereza wapate stahiki zao, waweze kununua sare zao wenyewe. Wasinunuliwe, wanunue kwa wakati ili wawe smart. Saa nyingine unakutana nao hawaeleweki. Tuwasaidie wakasimame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)