Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na hadi kuweza kusimama katika Bunge hili tukufu jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu na kuimarisha majeshi yetu haya kuhakikisha kwamba changamoto wanazokabiliana nazo zimeondoka ili kuimarisha suala la amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote, lakini pia niwapongeze majeshi yetu yote nchini kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba usalama wa raia pamoja na mali zao umepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika Jeshi letu la Polisi lakini kupitia ufinyu wa bajeti, wastaafu wa Jeshi la Polisi, pamoja na mifumo ya kumbukumbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi letu hili tunatambua kwamba limekuwa likifanya kazi kubwa na ya mfano katika Taifa letu na wanafanya kazi usiku na mchana, lakini la kusikitisha wana changamoto kubwa kutokana na ufinyu wa bajeti katika utekelezaji wa majukumu yao. Kitengo cha mafuta kinasuasua, mishahara yao inasuasua, magari mabovu, ofisi hazijulikani, vifaa vya ofisi havijulikani. Tumekuwa tukipitisha bajeti hapa na kuona kwamba angalau kutakuwa na unafuu katika utekelezaji wa majukumu yao katika utekelezaji wa bajeti hiyo, lakini baada ya bajeti ile kupitishwa tu changamoto zile zinaendelea kuwepo siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yetu kwamba katika bajeti hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameiwasilisha hapa, taarifa ya bajeti ni nzuri, imepangika vizuri, ni mategemeo yetu kwamba utekelezaji wa bajeti hii utaweza kwenda kulenga changamoto zote zile zinazowakabili jeshi hili katika maeneo yote Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa juhudi zake ambazo zinaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hadi kuhakikisha kwamba jeshi letu hili au majeshi yetu haya yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na changamoto hizo nilizozitaja, zipo changamoto kadhaa ambazo jeshi hili wamekuwa wakikabiliana nazo. Katika changamoto hizo moja ilikuwa ni magari, tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Kaskazini Pemba tumeweza kupatiwa magari mawili. Gari moja liko pale Makao Makuu ya Mkoa, lakini gari lingine limeelekezwa katika Kituo cha Polisi Mchanga Mdogo. Wanafanya kazi kwa kuhudumia wananchi kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni mafuta, hawana mafuta ya kufanyia kazi, uchakavu wa ofisi pamoja na vifaa vya ofisi, lakini pia majengo chakavu. Majengo yote ya Mkoa wa Kaskazini baadhi tu lakini askari wengi wanakaa uraiani. Si vema Askari Polisi pamoja na kazi zao kukaa uraiani kwa sababu kuna kazi zingine wanazofanya wanarudi usiku lindoni na mambo mengine. Kwa hiyo ni vema tukakarabati zile ofisi hasa pale polisi line, kuna ofisi nzuri tu ambazo majengo yake tumeyarithi kwa kipindi kirefu, kwa hiyo ningeomba yafanyiwe ukarabati mkubwa kwa sababu majengo yale ni mazuri. Pale kuna Mesi na mambo mengine, huduma za afya na mambo mengine. Kwa hiyo yakikarabatiwa majengo yale na majengo mengine yaliyoko Michewene na vituo hasa kituo kingine Matangatuani na Konde kwa hiyo Mkoa wa Kaskazini Pemba tutakuwa tumeondoa changamoto kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wastaafu. Kumekuwa na ukwasi mkubwa kuhusu suala la wastaafu wa Jeshi la Polisi. Mara nyingi unapotegemea kustaafu unategemea kwamba utapata haki ambayo itaweza kukusaidia katika maisha baada ya kustaafu. Askari wetu hawa wamekuwa wakidhalilika katika hali ya umaskini sana na wanaodhalilika sana ni kuanzia cheo cha Kuruta, Koplo, Sajenti, Senior Sajenti mpaka Inspector kidogo kumekuwa kama kuna makundi fulani kati ya huku na huku. Kwa hiyo ningeomba sana changamoto hii iweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna wastaafu ambao wameshalipwa haki zao kupitia mafao yao ambayo PSSSF tayari wameshawalipa, lakini kuna fedha za kusafirisha mizigo pamoja na nauli. Malalamiko ni makubwa, askari ni wengi sana wanaodai hizo haki, ni wengi mno, sasa hivi wanadai haki zao za kusafirisha mizigo ambapo wengine walikuwa wanafanya kazi Morogoro, wengine walikuwa wanafanya kazi mikoa mingine tofauti tofauti, lakini fedha zao hawajalipwa. Kwa hiyo inasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu walipeleka malalamiko maeneo tofauti tofauti ikashindikana, wakapeleka malalamiko kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, mmojawapo katika Wakuu wa Mikoa wangu waliopo, akawatishia kuwapeleka kwa Mheshimiwa Rais. Matokeo yake haki zile waliweza kupatiwa mara moja. Nauliza hizi fedha zilitoka wapi na katika bajeti gani? Walipolalamika tu na kutishiwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, basi waliweza kulipwa hizi haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi utaratibu uliopo jeshini ni kuwa, ndani ya miezi mitatu kabla ya kustaafu, watumishi hawa wanalipwa haki zao za kusafirisha mizigo pamoja na nauli, lakini wale waliostaafu kipindi cha mwaka 2020/2021, haki zao hadi leo hawajapewa. Kwa hiyo hao watawekwa katika bajeti ipi? Nauliza, haki zao zitaingizwa katika bajeti ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mifumo ya kumbukumbu. Kumekuwa na ukwasi mkubwa katika mifumo ya kumbukumbu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wa Wizara tunaomba masuala ya kumbukumbu yaangaliwe upya katika jeshi hili kwa sababu kunakuwa na utofauti sana katika ulipaji wa haki, lakini pia katika suala zima la utekelezaji, yaani tunamfanya mpaka yule askari husika, aweze kutokuwa na imani na jeshi lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna askari naomba baadaye nimkabidhi Mheshimiwa Waziri. Askari huyu ambaye alikuwa anafanya kazi katika kituo cha Morogoro, alikuwa katika cheo cha Senior Sajenti. Askari huyu aliugua akiwa kazini, lakini pia pamoja na kuugua akiwa kazini, jeshi halikuangalia kuugua kwake wala namna ya kujua matibabu yake. Familia ikamsafirisha ikampeleka nyumbani Zanzibar, askari yule kwa bahati mbaya alifariki dunia, lakini alifariki dunia mwaka 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo mwaka mmoja baadaye inakuja barua ya kustaafu askari yule, pamoja na kupeleka vitambulisho na mambo mengine anaambiwa anastaafu kwa umri wa lazima wa miaka 55, lakini pia arejeshe vitambulisho pamoja na sare na mambo mengine, wakati askari yule ameshastaafu, mwaka mmoja baadaye ndio inakuja barua ya kustaafu, wakati amefariki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maida muda wako umekwisha.

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.