Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Waziri wakati anawasilisha bajeti yake hapa, ameeleza kwamba bajeti kutoka mwaka 2022 mpaka sasa mwaka huu 2023 imeongezeka maradufu. Kwa hiyo, kwa kuongezeka kwa bajeti hii, la kwanza, lazima tumshukuru mama kwa kukuongezea ma-bi na ma-bi na kuwa na ma-ti. Kwa hiyo, tunampongeza sana mama kwa kujali kuongeza bajeti ya Wizara hii ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ameongeza, ni kwa sababu Waziri mwenye dhamana na Naibu Waziri mko vizuri. Ndiyo maana mmeongezewa ma-bi, sasa mmekuwa na ma-ti. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako, pamoja na IGP, Afisa Uhamiaji, Makamishna wote pamoja na Katibu Mkuu, kazi mnayoifanya ni kubwa na nzuri sana. Ndiyo maana umesema uhalifu pia kutoka asilimia fulani ya mwaka 2022 na mwaka huu imepungua, ni kwa sababu ya kazi nzuri unayoifanya kuiongoza Wizara hii. Tunakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi, unajua Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ukitaka kujua kazi ya Jeshi la Polisi na taasisi zake zote wanafanya kazi nzuri, hebu siku moja vituo vya Polisi vifungwe kwa masaa kadhaa, tuone kitakachotokea. Ndiyo maana tunawapongeza, kazi mnayoifanya ni nzuri ya kutulinda sisi na mali zetu. Ongeza jitihada za kuhakikisha unaendelea kutulinda sisi na mali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa, Mheshimiwa Waziri na timu yako, wapo baadhi ya Askari wanaoliharibia sifa Jeshi la Polisi. Ndiyo maana leo umewaonesha pale zaidi ya watu wanne, umewatunuku kwa sababu ya kufanya kazi nzuri. Kwa hiyo, tunakupongeza kwa kuwatunuku wale kuwa mfano kwa Jeshi la Polisi kufanya kazi nzuri. Wengine pia watakaoendelea kufanya kazi nzuri, wape motisha ili waweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi. Kituo cha Polisi cha Makambako kina eneo ambalo wananchi walishalitoa. Nimekuelezea mara nyingi, mwaka 2022 mwezi Agosti alipokuja Rais nilisema, wanahitaji fidia yao kwa sababu hawawezi sasa hivi kufanya kazi ya aina yoyote. Hawawezi kuezeka nyumba zao hata kama mabati yameharibika, walizuiliwa. Fidia yao ni Shilingi milioni 250, sito B, ni milioni 235. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, jambo hili lichukulie maanani, ukiongea na Waziri wa Fedha ili wananchi hawa waweze kulipwa fidia yao na waweze kuondoka katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, Kituo cha Makambako ni kituo kilichopo center ambapo wako wahalifu wanatoka sehemu nyingine; Songea, Mbeya, Iringa nakadhalika, pale ni kama center. Tunaomba kituo hiki kwa sababu ni kituo kamili cha Wilaya ya Kipolisi, tunaomba vitendea kazi kama magari, kituo cha Polisi chenyewe kiimarishwe, kijengwe vizuri ili waweze kudhibiti uhalifu unatokea katika eneo letu pamoja na Mkoa wetu wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ni lazima tulipongeze Jeshi la Uhamiaji kwa kudhibiti wahalifu wanaoingia nchini. Maana bila kusimamia hawa, ndio wanaogeuka kuwa majambazi na ndiyo wanaotuharibia, lakini Jeshi hili limesimamia vizuri na hatimaye kila wakati tunapata taarifa kwamba wamekamatwa wahalifu mahali fulani, wamekamatwa wahamiaji kutoka sehemu fulani. Kwa hiyo, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi upande wa Magereza. Makambako tulitenga eneo kwa ajili ya kujenga eneo la Magereza katika Mji wa Makambako. Tunaomba, katika kutenga bajeti yake, Mheshimiwa Waziri aone sasa umuhimu wa kujenga Magereza Makambako ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo katika Wilaya ya Njombe. Wilaya ya Njombe ni kubwa sana, kwa hiyo, tunaomba sana utenge fedha kwa ajili ya kujenga Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo ambalo wenzangu wamelisema hapa, kwa upande wa NIDA. Vitambulisho hivi vimekuwa tatizo. Baadhi ya watu sasa wanatoka Makambako kwenda kufuata Njombe, na wakifika kule wanaambiwa waje kesho, keshokutwa na nini, kwa hiyo, nadhani tatizo hili inawezekana liko nchi nzima. Tunaomba jambo hili hebu mliwekee umuhimu kuhakikisha raia wa Tanzania wanapata vitambulisho vyao ili wajulikane kama ni raia wetu wa maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza juu ya malimbikizo ya Askari na mengine, pamoja na kwamba mnakwenda vizuri, hebu mwone namna ya kuhakikisha changamoto hizi za Askari wetu mnaziondoa ili kusiwe na tatizo juu ya Askari wetu ambao wanakuwa wamestaafu na wengine wanakuwa wakati fulani wanadai haki zao. (Makofi)

(Hapa Mhe. Deo K. Sanga alinyamaza kwa sekunde chache)

MBUNGE FULANI: Alikuwa anatafuta ma-bi na ma-bi. (Makofi)

MHE. DEO K. SANGA: Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona hapa natafuta ma-B, amount ile ili niweze kuitaja hyapa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiujumla nirudie tena, Waziri kazi yako ni nzuri. Unajua mtu anapofanya kazi vizuri ni lazima tumpongeze. Kabisa, unafanya kazi yako vizuri, pamoja na timu yako ya Makamishna wote pamoja na IGP wako, mnafanya kazi nzuri. Endeleeni. Hawa Askari wachache wanaochafua, mwadhibiti waweze ku…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Sanga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo naunga mkono hoja. Ahsante sana.