Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami kuwa mmoja ya wachangiaji katika Bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa, hasa ya Mheshimiwa Rais, ya kuhakikisha wananchi wanalindwa saa 24. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kwa kweli wanafanya kazi kubwa na wanajitahidi sana kusikiliza changamoto za wananchi kupitia wawakilishi wao, hasa Wabunge. Hiyo ndiyo sifa ya viongozi ambao sisi kama wenzao tumewatanguliza mbele kwa niaba ya kwenda kuwasikiliza wananchi waliotutuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana ambayo nataka nichangie. Jambo la kwanza katika Jimbo langu la Igalula, pamoja na ulinzi wa nchi kuwa imara, ambao Mheshimiwa Rais anaendelea kuuimarisha, tuna haja ya kuongeza upatikanaji wa ulinzi zaidi. Katika Jimbo langu la Igalula tuna ujenzi wa vituo vya Polisi ambapo wananchi waligundua kuwa ili waendelee kuwa salama, lazima waanzishe ujenzi wa vituo vya Polisi. Naiomba Serikali, Mheshimiwa Rais amekuwa akisaidia sana ujenzi unapofika katika hatua ya maboma, hata katika zahanati, vituo vya afya na shule, tunaletewa fedha, lakini sasa tuna maboma mengi ya vituo vya Polisi hayaletewi fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, tuna Mfuko wa Tuzo na Tozo, usiwe tu unahusika kwenye mikoa, basi ushuke na kwenye kata na vijiji ili kwenda kuimarisha vituo vya Polisi katika maeneo yetu. Hii itatusaidia kuondoa mitafaruku ambayo inawakumba wananchi wetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata vituo hivyo ambavyo viko katika hatua ya maboma ni Kituo cha Tura na Goweko. Naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri nilishakwambia, na nimeshauliza maswali kadhaa hapa mkaniahidi mtatenga fedha za bajeti ili ziweze kwenda kule, lakini kwenye bajeti hii sijaona fedha hizo zimetengwa. Naomba kupitia Bunge hili, unitengee fedha ili vituo vya Polisi viweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa ya Polisi wetu. Wanafanya kazi kubwa sana. Kazi ya kumlinda binadamu ni kubwa sana. Ninyi wenyewe mnafahamu, binadamu ana mbinu nyingi, lakini Polisi pamoja na uchache wao, wanajitahidi kuwalinda binadamu ili wasifanye madhara katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamekuwa na shida ya mambo mawili; jambo la kwanza, hawalipwi stahiki zao kikamilifu. Leo tunalalamika Polisi wanakula rushwa, lakini rushwa nyingine zinasababishwa na hali duni ya maisha yao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba, waimarishieni Polisi mapato, hasa zile posho zao stahiki zilizopo kwa mujibu wa sheria zikiwemo kodi za nyumba, kulipia bili za maji na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia leo hii Polisi wakienda kuomba bili za umeme wanaambiwa waende na risiti wakati sasa hivi mtandao umekuwa mkubwa, luku wananunua kwa kutumia simu zao za mikononi, maji wanalipia kwa kutumia simu zao za mkononi. Sasa unapomwomba risiti ni kwenda kuwadidimiza na kuwanyima haki yao ambayo ipo kwa mujibu wa sheria. Kama mlipanga kuwalipa shilingi 50,000 walipeni fedha zao, wao watajua watafanyaje huko. Kama analala kwenye pagale ambalo halina umeme, ni yeye na maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vitambulisho vya NIDA. Mheshimiwa Waziri hili jambo mimi naomba mfanye assessment ya uhakika, muone kama hili zoezi mnaliweza au tulisimamishe kwa muda ili tujipange upya. Kwa sababu gani nasema hivyo? Tuna changamoto kubwa ya vitambulisho vya Taifa. Leo tumesema kila mwenye laini ya simu lazima asajiliwe kwa kutumia namba ya NIDA, lakini fanya takwimu, simu zipo zaidi ya milioni 50, lakini namba za vitambulisho mmetoa ngapi? Ndiyo maana unakuta namba ya mtu mmoja anasajiliwa mtu mwingine ambalo ni kosa na kinyume cha sheria. Kwa hiyo, mimi namwaomba Mheshimiwa Waziri, hebu angalia hili jambo, kama mnaliweza tuendelee nalo, lakini mwongeze kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitambulisho hivi mmeacha kusajili tangu mwaka 2012. Sasa kuna vijana wamefikisha umri wa miaka 18 mpaka leo hamjaweza kusajili upya. Rudisheni zoezi mkasajili upya tena ili sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Venant, muda wako umeisha. Malizia.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)