Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya ya kuendelea kutoa ajira mpya ili kuliboresha Jeshi letu na Majeshi yetu nchini. Niwapongeze Mheshimiwa Waziri Naibu pamoja na timu nzima ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa mnayoifanya, ni kazi ya kiuzalendo; pia askari kazi wanayofanya ya kulinda mali na kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naenda kujikita kwa maeneo machache sana, hasa Jeshi la Zimamoto. Wabunge wengi wameongelea masuala ya makazi lakini Jeshi la Zimamoto lisipoanza na kuwa na mfumo wa zimamoto jamii; zimamoto jamii katika maeneo mengi miji inakua hata taarifa za majanga zinapotokea Jeshi la Zimamoto mpaka lifike kuna malalamiko kwamba either maji hamna ama wamechelewa kufika. Kwa hiyo wasipoanzisha zimamoto jamii katika maeneo ambayo ni hatarishi ili wanapopata taarifa ya majanga tayari wanakuwa na taarifa kutoka kwa wale zimamoto jamii kwamba ni vifaa gani vinatakiwa viende katika tukio linalotokea. Kwa sababu sasa hivi wanaweza wakaenda na vifaa ambavyo havifai kwenye tukio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakianzisha sera ya kuwa na zimamoto jamii wataweka coverage kubwa sana ambayo itawapunguzia kazi askari wa zimamoto. Hata ile ajali ya ndege ya Ziwa Victoria tungekuwa na zimamoto jamii maeneo yale wangeweza kuchukua hatua mapema zaidi; kabla ya Jeshi halijafika tayari. Hakungekuwa na hata mgongano wa wananchi kulalamika kuwa hawajafika; wanakwenda kuongezea nguvu tu kwenye zimamoto jamii. Vilevile wanakuwa tayari na taarifa. Kwa hiyo kazi itafanyika vizuri kwa sababu tayari wana taarifa kamili na nini hatua ya kuchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye upande wa NIDA, Wabunge wengi wamechangia, lakini nitoe ushauri kwa upande wa taarifa kwa wananchi wanaoishi vijijini. Wizara waje na mkakati maalum namna ya kuwapelekea taarifa wananchi ambao wanaishi vijijini kwa sababu wanatembea umbali mrefu, wanatumia gharama, hawana taarifa, akifika wanamwambia kitambulisho chako, bado, rudi. Mwananchi anatumia hata nauli elfu 30 mpaka 40, mwisho anakata tamaa anaacha, kwa hiyo watumie local radio, tv, Viongozi wa Serikali, Madiwani na hasa Madiwani wa Chama cha Mapinduzi ndio watapata taarifa kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilitembelea kwenye vyuo vyetu, bado vina hali ngumu ukizingatia Jeshi la Uhamiaji pamoja na Jeshi la Zimamoto tumeuhisha sasa hivi ndio wanaanza kujitegemea kama majeshi, hawana vyuo ndio wanaanza kujenga. Kwa hiyo Wizara itenge fedha, wapewe bajeti ili waweze kumaliza vyuo vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Sheria ya Parole; Sheria hii ndio itapelekea kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na hili Mheshimiwa Rais ameliona na ndio maana amemchagua Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Mheshimiwa Kagasheki kuwa wakatazame walete sheria ya mabadiliko itakayowezesha wafungwa kupata unafuu na kupata msamaha ili waweze kupunguziwa kesi pamoja na kupunguza msongamano magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kata za kimkakati ambayo jiografia imekuwa ni ngumu, uhalifu unapotokea mpaka askari polisi wafike inakuwa ni tatizo hasa katika Jimbo langu la Nkasi Kusini, Kata ya Sintali, Kata ya Kizumbi, Kata ya Myula, pamoja na Kata ya Nyinde. Hizi kata zote ziboreshwe, vituo vya polisi vimechoka, vina hali ngumu pamoja na makazi. Wabunge wengi wamechangia kuhusu makazi ya askari wetu, kwa kweli ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anapokuja kumalizia, kwa kuwa yeye ni msikivu mzuri, safi kabisa, anatenda kazi vizuri, aje na mkakati wa namna ya kuboresha makazi ya askari wetu, yako katika hali ngumu sana pamoja na Ofisi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)