Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Wanasema moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote, kwa niaba ya familia ya Mwamoto naomba nitoe shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Spika na Wabunge wote wa Bunge hili la Muungano kwa kutufariji wakati wa msiba. Kwa kweli hatuna cha kuwapa lakini Mwenyezi Mungu awabarika sana na marehemu alikuwa ni Mume wa Askari wa Gereza Kuu la Iringa. Pia, naomba nishukuru sana Mheshimiwa Waziri ulipiga simu na ukatuletea na mchango Mungu akubariki sana lakini naomba pia niwashukuru RPC pamoja na Uongozi mzima wa Magereza Mkoa wa Iringa kwa ushirikiano wao mkubwa ambao waliuonesha wakati wa msiba wa Kaka yetu mpenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu kwa maboresho makubwa sana katika Jeshi hili, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa ushirikiano wao mkubwa katika Wizara hii, wamekuwa watu wa msaada sana wakati wako tayari. Naomba pia niwapongeze Wakuu wote wa Majeshi ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana bila kumsahau Anna Makakala ambaye anatuwakilisha wanawake vizuri katika jeshi hilo. Naomba pia nimpongeze RPC wetu wa Mkoa wa Iringa amekuwa na ushirikiano mzuri sana katika Mkoa wetu wa Iringa na kazi nyingi zinakwenda kwa sababu yuko tayari wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Polisi pale Kihesa tumekuwa tukiongea muda mrefu sana, wameanza angalau kujenga, japokuwa nyumba zile hazitoshi, bado maboresho yanahitajika sana katika nyumba zile za FFU Kihesa. Pia nyumba zilizopo Makao Makuu pale Iringa, kambi zao kwa kweli ni mbovu sana. Wakinamama, watoto ambao wanakaa katika zile kambi wanaishi kwa shida sana, tunaomba kwa kweli pia ziboreshwe ili waweze kuishi vizuri kwa sababu Askari wengi wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu Wilaya ya Kilolo. Wilaya ya Kilolo imeanza siku nyingi sana toka 2022 lakini haijajengewa Makao Makuu ya Polisi katika Wilaya ya Kilolo. Sasa utakuta OCD anakaa Kata ya Lugalo karibu kilometa 70 kutoka yalipo Makao Makuu lakini Serikali inatumia gharama kubwa sana kusafirisha mahabusu kutoka huko Lugalo mpaka katika Mahakama ambayo ni Makao Makuu. Kwa hiyo, ungefanyika utaratibu mzuri kwamba Makao Makuu kwanza ijengwe ili OCD akae na DC sehemu moja, kupunguza hata gharama za Serikali lakini pia hata mahabusu wasiwe wanasafirishwa kwa muda mrefu kwa sababu hata kuna uhaba mkubwa sana wa magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ni kulipia tu lile eneo kwa sababu eneo lipo lakini halijalipiwa, tulisikia Serikali ilishaanza kutenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Polisi Kilolo lakini eneo halijalipiwa, kwa hiyo, ufanyike utaratibu lile eneo walipe fidia kwa wananchi ili waweze kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni kipo mbali sana na Makao Makuu hakina gari lakini kumekuwa na ajali nyingi sana katika ile Barabara, sasa tunaomba Serikali iangalie umuhimu wa kutoa gari katika Kituo cha Polisi cha Ruaha kwa sababu kiko karibu kabisa na Jimbo la Mikumi. Pia, tunaomba Serikali itoe pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Idodi ambacho ni lango kuu la utalii kwa ajili ya kusaidia Mikumi National Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalipongeza pia Jeshi la Magereza linafanya kazi nzuri sana, kuna mashamba makubwa ambayo kwa kweli kama yatafanyiwa kazi nzuri nafikiri Jeshi la Magereza litakuwa na uchumi wa kutosha. Kuna lile Gereza la Isupilo, kuna Gereza la Pawaga, wana mashamba makubwa ambayo yamekaa hayana kitu chochote, sasa kama hawawezi basi waweke hata wawekezaji waweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ritta muda wetu ndio umeisha, unga mkono hoja.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)