Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante sana kwa nafasi hii. Nami ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Waziri na Watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani, moja kwa kufahamu kwamba katika dunia tunayoenda sasa ya sayansi na teknolojia ni aibu sana kuendelea kutumia Askari barabarani kuongoza magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika bajeti ya Waziri kwamba mmeanza kufunga taa katika Majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, hii programu ni nzuri sana na ni muhimu ikaendelea katika maeneo mengine kama Morogoro na kwingineko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya sasa haiwezekani hata kidogo kwa kweli tuna upungufu wa Askari karibu asilimia 40 ya nchi yetu halafu tunaendelea kutumia Polisi kwenda kuongoza magari barabarani. Tunaomba hii teknolojia iendelee mbele watu wakae sehemu wachache wa-control computer watazame magari yanaoenda speed. Mtu anakamatwa hata kama mbele ya kilometa 50 anapewa faini kuliko Askari kukaa kila kichochoro, wakati huo wananchi katika vijiji wananchi katika Kata wanalalamikia wapate Askari wa kuwalinda. Kwa hiyo, hili ni jambo zuri na ni jambo kubwa, mpango huu Mheshimiwa Waziri ni vizuri ukawekewa fedha za kutosha ukaenda katika Majiji yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mimi kushika shilingi ya Kaka yangu Mheshimiwa Masauni nitashika kwa mambo mawili. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wote wamefika Jimboni kwangu. Mheshimiwa Waziri tumeenda nae Jimboni mpaka tumepita vichochoroni mpaka kwenye Magereza ya Idete ameenda mpaka Gereza la Kiberege ameenda kule, tumeingia ndani kona zote. Leo Watanzania wa Kilombero wa Ifakara wanaangalia hivi ninavyochangia, ahadi yao ya Wilaya ya Kilombero kukosa Kituo cha Polisi cha Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ni Wilaya kongwe sana, haina Kituo cha Polisi cha Wilaya, tumeshatafuta eneo tumelipata na mimi Mbunge nimepeleka tofali, anapokaa OCD wetu hapafai, wakati wa mafuriko maji yanaingia. Kwa hiyo, kama ni kushika shilingi Mheshimiwa Waziri mimi nitataka ufafanuzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni Kituo cha Polisi Tarafa ya Mwaya Kata ya Mwaya. Mheshimiwa Waziri umefika umekuta kituo cha Polisi cha mbao, katika dunia ya sasa hivi Kata ambayo inaongoza kwa watu wengi, mimi nina tofali za kuchangia pale Wizara inanipa nini? Tujenge Kituo cha Polisi ama tukarabati tuondoe zile mbao katika Kata ya Mwaya Askari wetu wapate Kituo cha Polisi chenye sifa ya kukaa vizuri. Kituo cha Polisi cha Mwaya kila mwaka Waandishi wa Habari wanaenda wanakipiga picha wanakisambaza hizo picha. Kwa hiyo, siyo vizuri jambo hili ni baya sana katika Kata yetu ya Mwaya, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana chondechonde haya mambo mawili makubwa unisaidie Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero na Kituo cha Polisi cha Kata ya Mwaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, NIDA imekuwa usumbufu kama baadhi ya Wabunge walivyosema. Wananchi wetu walishakubali kupata Namba za NIDA achana na haya mambo ya kitambulisho. Namba hizi haziji kwa wakati, sasa kama kweli mmeweka bilioni 42.5 Mheshimiwa Waziri tafauteni utaratibu ambao namba hizi watazi-print kwa wakati. Mimi kila siku napokea meseji hapa 10, 15, 20, nimekwama nimekuja Wilayani nimetafuta NIDA nimekosa. Nikatafuta na mimi operesheni nikaongea na Mkurugenzi wa NIDA na mimi nikatafuta chochote kitu, tukawachukuwa watu wa NIDA wakaanza kuzunguka katika Kata kufanya operesheni ya kuandikisha, haijasaidia kitu bado watu wengi hawajaandikishwa na watu wengi hawajapata namba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana jambo hilo utusaidie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Ifakara inaonekana inaongoza katika utapeli wa kimitandao. Kuna vijana wachache ambao wamekuja kutuharibia Mji wetu wa Ifakara. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa kuniletea OCD mpya na Mkuu wetu wa Wilaya wameanza operesheni maalum ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha kwamba Ifakara inasafishika na tunaondoka katika hiyo rank ya kwanza ya utapeli wa kimitandao kama juzi nilivyomuona Afande RPC wa Morogoro anachukua hatua na tunasafisha Mji wetu na Kilombero inakuwa safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)