Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje. Kwanza kabisa napenda kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa alizoweka za kubeba ajenda ya diplomasia ya uchumi na tayari tumeona matokeo chanya katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nitajikita eneo hili la diplomasia ya uchumi. Tunaposema na diplomasia ya uchumi ina maeneo mengi na mimi kwa muktadha wa mchango huu nitagusia maeneo matano. Eneo la kwanza ni ziara za viongozi wetu wa Kitaifa kwenda nje ya nchi. Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziara hizi zimeleta mafanikio makubwa ambayo tumekuwa tukiyaona, jambo ambalo bado linahitaji litiliwe mkazo na liimarishwe ni namna gani Wizara ya Mambo ya Nje, itatupa taarifa ya utekelezaji wa yale mambo makubwa na mafanikio yanayotokana na ziara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni uwekezaji kutoka nje ya nchi. Kupitia diplomasia ya uchumi Tanzania imefunguka na tumekuwa tukiona wawekezaji wengi wakija Tanzania, lakini jambo ambalo bado linahitaji kutiliwa mkazo ni kituo chetu cha uwekezaji - TIC bado hakina mamlaka ya kutoa huduama ya one stop center, kwa muktadha huo wawekezaji wanakuwa wanakuja ndani ya nchi wakiwa na matarajio ya yale ambayo yalikubaliana katika aidha TIC au kupitia ziara za viongozi wetu, lakini wanapokuja hapa nchini kunakuwa na mkanganyiko baina ya yale yaliyokubaliwa pamoja na utekelezaji aidha ngazi ya Tawala za Mikoa au Serikali za Mitaa kwa maana ya Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa tunahitaji kuweka jitihada za maksudi kabisa ili kuhakikisha kwamba uwekezaji wa kutoka nje ya nchi wanapokuja hapa nchini mambo yawe mororo kusiwe kuna vikwazo au mkwamo wa aina mabalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni biashara kati ya Tanzania na nchi zingine. Nawapongeza sana Wizara ya Mambo ya Nje, tumekuwa tukiona kila ziara za Wakuu wetu wa nchi sekta binafsi pia inakuwa inashiriki. Naomba nisisitize ushirikishwaji na ushiriki wa sekta binafsi hautakiwi kuwa tu pale ambapo kuna ziara za viongozi wetu wakuu, bali lazima tuweke jitihada za kuhakikisha kwamba sekta binafsi inatambua fika fursa zilizoko nje ya nchi na sekta binafsi kule nchi za nje na wenyewe wanatambua fursa zilizoko ndani ya Tanzania ili Wizara ya Mambo ya Nje iendelee kuwa kiungo baina ya sekta binafsi nchini Tanzania na sekta binafsi nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Wizara hii ya Mambo ya Nje inaifungulia njia Tanzania duniani, lakini utekelezaji wa mambo mengi yanafanyika kwenye Wizara za kisekta, hapa ndipo iko changamoto bado hakuna mkakati thabiti wa namna gani ambavyo Wizara ya Mambo ya Nje itaendelea kusimamia utekelezaji wa fursa mbalimbali. Utekelezaji wa maazimio mbalimbali katika Wizara zingine za kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni misaada kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Tumekuwa tukiona kupitia ziara za viongozi wetu, Wakuu wa Nchi, pia tumekuwa tukiona kupitia ziara za Wakuu wa Nchi zingine wanapokuja hapa Tanzania. Zinatolewa rasilimali fedha kwa maana ya misaada kwa ajili ya maendeleo ya jamii, lakini jambo ambalo bado linahitaji kutiliwa mkazo ni fedha zile za misaada bado utekelezaji wake zinakabidhiwa katika mashirika yasiyo ya kiserikali kwa maana NGO’s za nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Wizara hii inalo jukumu la kuona namna gani ambavyo wanaweza wakaisemea sekta ya NGOS za Tanzania, ili asilimia kubwa, zile rasilimali fedha zinazoingia Tanzania ziweze kutekelezwa na sekta ya NGOS za Tanzania. Kwa kufanya hivyo ndivyo ambavyo tutajihakikishia kwamba misaada inayoingia nchini inafanya kazi kwa kulinda na kwa kuzingatia misingi ya mila, desturi, tamaduni pamoja na yale ambayo yako kwenye Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili naamini kabisa halipaswi kuachiwa kwenye Wizara za kisekta kwa sababu, Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo inaweza ikajadiliana na nchi nyingine kwa kutumia diplomasia ya uchumi kuona namna gani ambavyo fedha hizi za misaada zinapoingia nchini, basi NGOS za Tanzania ziweze kupata jukumu la kutekeleza ili kulinda; moja, ajira za Tanzania; na pili, fedha hizi ziendelee kuzunguka katika mnyororo wa thamani wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ni suala la masomo na ajira za nje ya nchi. Tumesikia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri pamoja na hotuba ya Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu suala la diaspora. Tunapoongelea diaspora kuna Watanzania wenye uraia wa Tanzania, kuna Watanzania ambao wana asili ya Tanzania, lakini wana uraia wa nchi nyingine na kuna Watanzania ambao wako masomoni nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara, imezindua Diaspora Digital Hub tarehe 22 mwezi wa tano. Hii itatuwezesha kujua idadi halisi ya diaspora tulionao na wana taaluma zipi? Halikadhalika, liko jambo ambalo bado Wizara hii inahitaji kufanya. Nikiongelea kwa upande wa masomo, wapo vijana ambao wanapata fursa za masomo na wanapata fursa za scholarship kwa maana ya ufadhili wa masomo, lakini vijana hawa wanapoomba visa wanapata changamoto na wanajikuta wananyimwa visa. Sasa wanaponyimwa visa wakati wamekidhi vile vigezo vya msingi, kijana huyu anakuwa hana pa kwenda. Napendekeza Wizara hii ione namna gani ambavyo itasaidia vijana ambao wanakidhi vigezo vya msingi wasinyimwe fursa ya kupata masomo nje ya nchi pasipo sababu maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija pia kwenye ajira. Lazima kama Tanzania, maadamu tumeamua kuingia kwenye diplomasia ya uchumi, lazima tuangalie kada zipi ambazo sisi kama Tanzania tuna ujuzi nazo; na ni nchi zipi ambazo zinahitaji kada hizo; ili Wizara hii ya Mambo ya Nje iweze kujadiliana kupitia diplomasia ya kiuchumi, Tanzania itaweza kupata kada zipi katika nchi hizo? Kwa kufanya hivyo, tutaweza kupata diplomasia ya uchumi kwa maana ya kuwa na ajira ya Watanzania wengi zaidi ambao wanafanya nchi za nje, kwa mfano, kwenye kada ya Udaktari, Unesi, Ualimu, na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina zaidi ya wananchi milioni 60. Kwa takwimu ambazo zilitajwa mapema mwaka huu hapa Bungeni, tunao diaspora 1,500,000 tu. Kwa nchi yenye wananchi milioni 60, bado hapa tunahitaji kuweka jitihada za nguvu zaidi ili kuhakikisha tunaongeza tija ya Watanzania ambao wako nje ya nchi, na ziko fursa nyingi katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye ajira, nitilie mkazo umuhimu wa Wizara hii ya Mambo ya Nje ione namna gani ambavyo Watanzania watapata fursa za ajira katika mashirika ya kimataifa. Miaka ya nyuma tulikuwa tuna Watanzania wengi sana kwenye mashirika ya kimataifa, nami naamini kupitia jitihada za makusudi kabisa za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tutaweza kupata fursa hizi za ajira kwenye mashirika ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumteua Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula kuwa mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Hii ni nafasi nyeti sana. Hivyo, naiomba sana Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia balozi zake na machineries nyingine tuweke jitihada kubwa kuhakikisha tunapata fursa hizi za ajira. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu ya kuhitimisha. Naomba niishauri Wizara hii ianzishe kurugenzi ya fursa ili kurugenzi hii itoe fursa kwa Watanzania, Watanzania waweze kuelewa fursa pamoja na sekta binafsi. Wizara hii itoe elimu kwa Watanzania tuweze kuelewa diplomasia ya uchumi maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado suala hili halieleweki ndani ya Serikali, Taasisi za Serikali, katika Halmashauri zetu, sekta binafsi na hata na sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha. Suala hili la hadhi maalum, nawapongeza sana Serikali kwa hatua ambazo wamechukua, lakini naomba sana tulinde kwa wivu mkubwa suala la ushiriki kwenye masuala ya kisiasa pamoja na ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Ajira hizi na ushiriki wa kisiasa lazima ulindwe na uwe ni kwa ajili tu ya Watanzania. Haiwezekani mtu mwenye uraia wa nchi nyingine apate fursa ya kushiriki kwenye shughuli za kisiasa au apate fursa ya kupata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali na Wizara hii, tulinde maeneo haya mawili kwa wivu mkubwa. Masuala ya kushiriki katika siasa, masuala ya ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama, hizi zilindwe ni kwa ajili ya Watanzania na Watanzania pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)