Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta’aala aliyenipa satua na nguvu ya kusimama hapa mbele ya Bunge lako tukufu kuchangia hotuba hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyojitahidi kuchukua hatua ya kuifanya Tanzania yetu kupaa katika mizani ya kisiasa. Kazungumzia mambo muhimu sana katika jitihada zake, tumeweza kuona ile diplomasia ya mashirikiano ya kimataifa, kuchochea diplomasia ya kiuchumi, kuvutia wawekezaji, kushamirisha uchumi wa Bluu, kufungua masoko na kuhusiana na kuweka masuala ya tabianchi. Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kweli ameipaisha Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee napongeza sana jitihada za Waziri wetu mahiri na hodari, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax, pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Mbaruok, Makatibu wake Wakuu, watendaji, maofisa na wachocheaji wa protocol na wawakilishi mabalozi wetu wote wa Tanzania duniani kote kwa jitihada zao wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri shughuli za Wizara yetu hii zinakwenda vizuri sana. Serikali imefanya jambo zuri sana la kuhakikisha hadhi maalum hii kutolewa, kwa sababu kilio hiki cha uraia pacha kilikuwa ni cha muda mrefu cha ndugu zetu hawa wa diaspora. Leo Serikali imekuja na hili. Niwashauri tu wana-diaspora wapokee hii, mengine mazuri yatakuja baadaye. Wapokee kwa moyo mkunjufu, wajiandikishe kama walivyoelekezwa. Serikali yetu ina nia nzuri na mambo mema yatapatikana baadaye. Kwa sababu jambo hili wamelitaka siku nyingi. Inawezekana wasifurahie sana kuambiwa wapate hadhi maalum, lakini hadhi maalum ni nzuri kwa sababu bora moja kuliko kukosa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhusiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, tunajua sote Wizara hii ni miongoni mwa Wizara kongwe ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa Taifa letu hasa katika nyanja za kitaifa, kikanda na kimataifa. Sambamba na hilo, Wizara hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu ambapo Maofisa wa Mambo ya Nchi za Nje wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana kuhakikisha wanakusanya taarifa za kiintelijensia, kudumisha ujirani mwema na hata kutoa taarifa za awali (early warning) ambazo zinaisaidia nchi yetu kuepukana vita au majanga mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na unyeti wa kazi ambazo zinafanywa na Maofisa wa Mambo ya Nchi za Nje, kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inapaswa kuangalia upya kuhusu status za maafisa hawa ambapo nahisi wakati umefika sasa kada hii ya Maafisa wa Mambo ya Nje ikapewa hadhi maalum, special recognition na kumtofautisha Ofisa Mambo ya Nchi za Nje na ofisa mwingine wa Serikali. Ni dhahiri hali ya Maafisa wa Mambo ya Nchi za Nje zinakuwa ni bora pale tu ambapo wanakuwa nje ya nchi ambapo hupokea posho maalum (special allowance), lakini wanaporejea ndani ya nchi, maafisa hawa wanakuwa wanyonge kutokana na maslahi duni wanayoyapata licha ya kazi kubwa na ngumu ambazo wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisa Mambo ya Nchi za Nje, haheshimiki kama wenzao wa Idara ya Usalama wa Taifa ama Wizara ya Fedha. Naomba Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ipitie upya kada hii na kutoa maslahi sawasawa na wanayopatiwa Idara ya usalama wa Taifa. Afisa huyu wa Mambo ya Nchi za Nje naye anahusika na masuala ya kiintelijensia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ningependa kugusia ni kuhusu scheme of service hasa inapofika wakati wa kupandishwa vyeo au uteuzi wa mabalozi. Kwa heshima sana, kipekee, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kurejesha hadhi na heshima ndani ya Wizara hii ambayo kwa muda mrefu ilitoweka. Kipekee nampongeza Rais kwa kuendelea kuwaamini vijana waliokulia ndani ya kada na kuwateua Maafisa wa Mambo ya Nchi za Nje kuwa Mabalozi. Hili ni jambo zuri sana na linafaa kupongezwa, kwani linachangia kurudisha morale na imani kwa maafisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwa hatua ya kuona umuhimu wa kuteua kikosi kazi maalum cha jopo la mabalozi wabobezi, ambao wamepewa kazi mahususi ya kuangalia mwenendo na utendaji wa kazi za Wizara hii. Jambo ambalo naamini mwisho wa siku itasaidia kutoa mwelekeo chanya na ufanisi kwa utendaji wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye scheme of service napenda kusisitiza Wizara kuzingatia kikamilifu taratibu za Utumishi wa Umma, kwani eneo hili limekuwa na changamoto kubwa. Maafisa wengi ambao walipaswa kupandishwa vyeo, bado wengi hawajapandishwa, hali hii inawanyima fursa mbalimbali ikiwemo kupata uwezekano wa kuteuliwa kuwa Mabalozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Foreign Service Regulation iliyokuwepo imepitwa na wakati na haiendani kabisa na matakwa ya mazingira ya sasa kwa Maofisa Mambo ya Nchi za Nje. Nashauri Wizara kama bado hawajaanza kuifanyia kazi, mapitio ya regulation hii iliyopo, waanze na wahimize ili kuweza kuendeleza na kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi wa Maafisa wa Mambo ya Nchi za Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Wizara iongeze mashirikiano na kuweka karibu Waziri, Makatibu Wakuu, watendaji, kwa kuandaa retreats angalau mwaka mara mbili, kuandaa masomo mafupi mafupi ili kuwaweka hawa watu in order.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine muhimu sana. Tunazungumzia diplomasia ya uchumi, lakini tunapowachukua wachumi wabobezi ambao wamekuwa kwenye foreign service na wamekuwa ubalozini kwa miaka kadhaa isiyopungua kumi pengine, halafu unamtoa unampeleka ukamfanye Kaimu Katibu Tarafa, ina maana umepoteza ile potential. Huyu ana uzoefu wa ku-deal, ku-lobby na kufanya vitu fulani kwenye foreign service, wewe unampeleka kule. Inakuwa sawa sawa na kumchukua surgeon unamwambia akafanye kazi ya ofisa ugani. Naomba watazamwe wale wote ambao walikuwa displaced, wakapelekwa kwenye sehemu wasizohusika warudishwe kwenye career yao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwapatia fursa hawa foreign service waendelee kwenye career yao ni jambo bora, kwa sababu mtu ameshakaribia kufika awe balozi, wewe unamtoa unampeleka Katibu Tarafa, is that fair jamani! Hii siyo haki. Unampeleka kwenye line nyingine hana uzoefu nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kabisa mimi naunga mkono hili jambo la diaspora na ninaomba tufanye kazi zaidi ili tusije tukajiingia katika jambo ambalo litahatarisha usalama wetu na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi naona kama nimalize mambo yangu hayo. Ah, jambo moja nimesahau, kweli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku nyingi tuliambiwa kama majengo ya ubalozi ya nchi zetu yatakarabatiwa, lakini hii imekuwa ahadi ya siku nyingi, sijui lini itakamilishwa. Bahati nzuri mimi nimebahatika pia, msinione hivi, nimeshakuwa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, tuliwahi kuwa kwenye msafara na Makamu wa Rais, by then Mheshimiwa Dkt. Shein, tukaambiwa kule ubalozini Abuja, kama kiwanja kipo na kila kitu tayari, ubalozi utajengwa; na kwingine hivyo hivyo. Sasa jambo hili lifanyiwe kazi. Kwa sababu tukiwa na majengo yetu tutapata faida nyingi. Tutapangisha, tutafanya shughuli zetu pamoja na makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Chuo cha Diplomasia. Hiki chuo kilikuwa kinaendeshwa kwa ushirikiano baina yetu sisi na Mozambique, lakini inaonekana kama ushirikiano ule umetetereka kidogo. Sasa Serikali imejipangaje kukiendeza chuo hiki ili kiwe na hadhi kubwa na kiwe cha kileo zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Baada ya hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)