Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kweli, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama mbele ya Bunge hili na kuweza kuichangia Wizara hii. Sina budi kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyoifanya pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na wote wa Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, kwa kazi zake nzuri. Ameiweka Tanzania katika ramani iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi pia, kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi yake nzuri anayoifanya Zanzibar na tunajiringia Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka niipongeze Wizara kwa pesa walizozipata safari hii, Shilingi bilioni 17.8 ambazo ni fedha za maendeleo. Wizara hii inakwama, kwani kwa miaka mitatu mfululizo pesa za maendeleo wanazopatiwa ni ndogo; na hiyo ndogo wanayopewa, pia haifanyi kazi. Wanaweza wakapewa robo yake, hata nusu haifiki. Sasa tunalaumu kwamba balozi zetu hazijengwi, vitega uchumi havijengwi, na mambo mengi tu kwamba Wizara hii haiwezi kutekeleza. Tatizo siyo Wizara, tatizo pesa za kutekeleza miradi ambayo wanajipangia, hawapewi kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Wizara ya Fedha itupie jicho Wizara hii ya kimataifa. Wizara hii ni jicho, Wizara hii inafika mbali, Wizara hii ina mambo mengi. Sasa hii Wizara tuiangalie, pesa wanazotengewa wapewe kwa mujibu wa taratibu, waweze kujenga vitega uchumi katika balozi zetu ambapo tunakwenda kwenye Sera ya Uchumi wa Diplomasia. Bila mtu kumpa pesa, hataweza kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija na suala la Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika, ya Haki za Binadamu, ambayo ilikuwa ijengwe kipindi kirefu; ina maana kuna miaka 16 mfululizo toka tumeridhia hatujafanya chochote. Tumeridhia, tumekubali, lakini hakuna kilichokuwa. Sasa tunajiuliza, tunakwenda kwenye diplomasia ya kiuchumi, ni ambayo ni ya kubana matumizi! Kwa sababu, hatuwapi pesa. Mtu haumpi pesa, hawezi kutekeleza. Tanzania tunaiweka katika picha gani au ramani gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeahidi nyie kujenga. Miaka 16 hatujajenga, tunailaumu Wizara! Hatuilaumu Wizara, tunalaumu hawapewi fedha kulifanya hili tukio walilotakiwa wafanye. Nashukuru safari hii angalau wametengewa Shilingi bilioni 5.4, naiomba Wizara iweke alama, ifanye kitu na kazi iendelee na waweze kujenga. Isiwe sababu hampati pesa. Pesa mmeshapewa, mnatakiwa muanze jukumu la kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija na hii Royal Tour. Mheshimiwa Dkt. Samia aliondoka ofisini kwake, akatembea kwenye mbuga na nyika; kwenye vielelezo vyote vya utalii; na akafanya kuipaisha Tanzania katika ramani ya utalii, lakini watalii wanakuja kwa wingi Zanzibar, wanakuja kwa wingi Tanzania Bara, na wanaotakiwa wafanye kazi kubwa ya kuhamasisha ni Wizara hii. Sasa na mtu hawezi kuhamasisha kitu kama hana pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea pale pale. Kazi ya mama haikuwa ya bure, kazi ya mama kajituma, inatakiwa ienziwe. Tumuenzi Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kazi yake nzuri aliyoifanya ambayo inatuletea mapato Tanzania. Sasa ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake, lazima iwe na pesa za kutosha za kufanya kazi zake. Nampa pongezi Mheshimiwa Dkt. Samia Hassan Suluhu kwa ari yake, kwa kubuni hii ziara akaweza kuipaisha Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera ya Mambo ya Nchi za Nje, kwanza naiomba Wizara, muda ulikuwa mrefu na ninategemea hii 2023/2024 inawezekana sera hii ikatoka maana iko katika hatua za mwisho za utendaji kutokana na maelezo yako Mheshimiwa Waziri. Nami naunga mkono itoke, aweke alama kwamba kile kitu umekisimamia na kimekuwa na kimetoka. Kwa sababu hii pia ndiyo itakayotusaidia katika diplomaisa ya uchumi, au diaspora, hii ndiyo itakayoleta ari na mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hili suala la uraia pacha kwa Tanzania bado mapema. Tuikamate hii hii hadhi maalum. Hadhi maalum unapata kila kitu; tatizo liko wapi? Kwa sababu unatambulika, familia inakujua, Taifa linakujua, nyumbani wanakujua; tunataka nini tena? Kwanza hata ukisema unataka uraia pacha itakusiadia nini? Muhimu ujulikane kwenu na ufanye mambo ya kisheria ya kwenu, na sheria inakutambua kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aendelee na mchakato wake. Sera inatoka na hadhi maalum inatoka zinakwenda sambamba, Tanzania oyee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, diplomasia ya uchumi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, maana yake kengele imelia, malizia hiyo moja.

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika diplomasia ya uchumi – nazungumza dogo tu – kwamba sekta mtambuka za Tanzania zishirikiane na mambo ya nje zitoe elimu kwa wananchi, kama biashara, sehemu za masoko, investment, kwa sababu kuna watu hawaielewi, wanakosa kujua maadili ya hilo jambo linavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)