Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika mwaka wa fedha huu 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipongeze Wizara hii kwa hotuba nzuri ambayo naamini kwamba kama ikitekelezwa kikamilifu italeta matunda chanya. Lakini pia niseme kwamba, kama wenzangu waliotangulia walivyosema, kuwapongeza Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, pamoja na Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, kwa kupatiwa nafasi na Serikali yetu kugombea nafasi hizi za IPU na kuwa Katibu Mkuu katika Jumuiya ya Madola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi; nafasi hizi ni very competitive, watu wanao-compete ni wengi sana, tusije tukafurahi kwamba tumepeleka majina kwa hiyo automatically watapata. Mimi nafikiri ni vyema Serikali yetu ikajipanga vizuri, hasa ikiongozwa na Wizara yetu hii ya Mambo ya Nje kuhakikisha tunafanya kampeni ya kufa mtu ili nafasi hizi tuzipate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za Afrika Magharibi zimeweka watu wao kwenye nafasi hizi za kimataifa kiasi kwamba wame-benefit a lot kutokana na kwamba wale wafanyakazi wao wanarudisha nini nyumbani. Kwa hiyo ninaomba sana Serikali tusilichukulie lelemama bali tuweke nguvu tukiona kwamba tumekuwa na Katibu Mkuu katika Jumuiya ya Madola, nafasi hii itatupa nafasi kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania kupata mambo mengi, maana mimi nilishapata experience kidogo, nimefanya kazi kidogo kule, kwa hiyo najua kuna nafasi gani kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nizungumzie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wetu aliyoileta kuhusu kwamba yeye anaweka mkazo katika diplomasia ya kiuchumi. Tukumbuke kwamba Hayati Benjamin Mkapa hii ndiyo ilikuwa area yake ya kipaumbele miaka 28 iliyopita. Miaka 28 iliyopita aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu alisema diplomasia ya kiuchumi ndiyo itakayoongoza Taifa letu katika kutuletea maendeleo ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni miaka 28, hebu tujiulize, katika miaka 28 hii inaendana na yale ambayo tumeyafanya tangu wakati ule mpaka leo? Ni wazi kwamba tuko nyuma sana katika diplomasia ya kiuchumi. Tukiangalia yale ambayo yamefanyika kwa kipindi hicho mpaka leo, hakika utajua kwamba tuko nyuma sana kwa yale yaliyotakiwa yafanyike hadi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwamba ameunda tume ya kuangalia utendaji wa Wizara hii ya Mambo ya Nje. Ina maana kwamba kuna mapungufu makubwa ameyaona katika Wizara hii. Na hii pia inanipa picha kwamba kumekuwa na mapungufu makubwa. Nikiangalia kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano hii ya mwisho, maafisa masuuli wamebadilishwa badilishwa sana, takriban kila mwaka unapata Katibu Mkuu mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaashiria kwamba kuna tatizo kubwa mahali; ama wale wanaomshauri Rais, kwamba huyu anafaa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, au yale yaliyotegemewa siyo wanayoyafanya. Kwa hiyo hapo tuliangalie sana. Naamini kwamba tume hiyo itaweza kumshauri vizuri ili tuwe na watendaji wazuri katika Wizara hii na katika Mabalozi ambao wataweza kufanya haya tunayoyapanga hapa yatekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ambayo bado haijakamilika. Na hii ndiyo itakua kioo chetu, hii ndiyo itaweza kutufanya tujipime, kwamba tunakwenda wapi. Kama sera haijakamilika itakuwa pia shida kwamba tunashika lipi na tunakwenda wapi. Kwa hiyo ninashauri kwamba Mheshimiwa Dkt. Tax, uhakikishe kwamba sera hii inapita, ambayo ndiyo itatusaidia katika kuhakikisha kwamba haya yote ambayo tunataka kupitisha leo yanafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika Ripoti ya CAG kuhusu majengo yetu kwenye balozi zetu. Majengo yetu haya yamekuwa ni ya kutia aibu sana. Kwanza, tukumbuke kwamba takriban miaka 50 tulipata viwanja kama kumi hivi kule Zambia tulivyopewa na Hayati Kenneth Kaunda. Viwanja hivyo hata ukifika leo ni mapori. Inatia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati zetu nne; PAC, PIC, LAAC na Bajeti; tulitembelea maeneo yale. Tumeona ni aibu kubwa, maana wale wenye majengo yao, nyumba zao karibu na viwanja vile, kwa kweli wanasikitika sana na wanachukia sana kwamba tumewaachia mapori katika viwanja vile, kwa sababu haviendelezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hayati Kaunda alikuwa ameona kwamba hii itatusaidia kama vitega uchumi. Na tulipotembelea kule wakati huo aliyekuwa Balozi alituambia kwamba viwanja vyetu kama vingejengwa inavyotakiwa, ni wazi vingesaidia kulipa kodi takriban Balozi zote zilizoko katika Bara la Afrika. Lakini mpaka leo ndiyo tunaambiwa bado bajeti ndiyo inapangwa viwanja hivyo vikajengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kusikitisha zaidi ni pale ambapo jengo letu lililopo kule Washington limepoteza kinga ya kidiplomasia kwa kuwa ni chakavu mno, na kwa hiyo wakasema kule wenzetu hatuwezi kuendelea kukaa na uchafu huu, na hatutambui kama ni jengo la Balozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo tukatakiwa tulipe kodi, na imelipwa kodi kiasi cha milioni 283.3 kwa ajili ya kulipia jengo bovu. Sasa haya ndiyo kati ya mambo ya kujitathmini; hivi kweli tuko serious na tunayoyafanya? Tumeacha kukarabati majengo yetu, tangu miaka 29 Hayati Mkapa alivyosema uchumi wa diplomasia ndiyo utaongoza nchi yetu. Leo majengo tumeyaacha na majengo yale ndiyo ya kututambulisha, kwamba hawa ndio Watanzania. Leo majengo yale yamekuwa ni aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia tuna Balozi 34 ambazo hazina majengo yao. Pamoja na kwamba wamesema 14, angalia hiyo aya 20 yatajengwa lini. Kutokana na hivyo, mwaka 2021/2022 Tanzania ililipa bilioni 15.47 kwa kodi ya mapango haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo unaangalia kwamba hivi kweli diplomasia ya uchumi tunayoongelea maana yake ni nini? Maana yake ni kukuza uchumi. Lakini angalia uone kwamba uchumi wako unaukuzaje wakati una gharama nyingi kuliko ambavyo unaweza ku-sustain hiyo diplomasia ya uchumi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kaboyoka.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda la mwisho, tuna uhaba mkubwa wa uwakilishi wa heshima katika balozi zenye nchi zaidi ya moja. Hilo nalo naomba Wizara iliangalie, ahsante sana. (Makofi)