Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika mjadala huu muhimu na adhimu. Awali ya yote ningependa kuchukua fursa hii kutoa shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo makubwa sana toka alivyoingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyanja nyingi zimeendelea lakini kama tutakuwa tunachambua, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Sera ya Nje ni miongoni mwa vitu ambavyo Mheshimiwa Rais na timu yake imefanya kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pongezi zangu ziende kwa Waziri Mheshimiwa Tax na aliyemtangulia Mheshimiwa Mulamula kwa kazi kubwa waliyoifanya. Naomba nichukue fursa hii kumtakia Mheshimiwa Mulamula kila la kheri katika nia yake ya kuwania nafasi ya General Secretary wa Commonwealth kila la kheri Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia mambo matatu na nitajitahidi yote niyagusie kwa sababu ya msingi na ya dhati. Nimefarijika mno kumsikia Mheshimiwa Waziri kwamba ameyagusia mambo yote ambayo ningependa kuyachangia. Ningependa kuzungumzia diaspora, Sera ya Diplomasia ya Uchumi na suala la uraia pacha au hadhi maalum yote ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, diaspora maana yake nini? Diaspora ni neno la Kigiriki ambalo maana yake ni kutawanyika ulimwenguni. Watu ambao wametoka sehemu yao ya asili wakatawanyika ulimwenguni, ndio maana ya diaspora. Watu hutawanyika ulimwenguni kwa sababu mbalimbali kuna wengine inawabidi wahame kwa sababu ya vita, mauaji ya kimbali, kwa sababu ya njaa kali (famine), na wengine wanakwenda tu kwenye masomo na wengine tu kuwania maisha na kutafuta riziki zao za kheri na watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ubaya kwa mtu kuhama na kwenda sehemu yoyote kujitafutia riziki yake, yote hiyo ni ruhusa. Tafiti zinaonesha kwamba diaspora inachangia katika nchi ya asili mambo makuu matatu mpaka manne. La kwanza, kijamii; la pili, kisiasa; na la tatu, kiuchumi au kimaendeleo. Hayo ndio maeneo ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijamii, wale ambao wako huko pengine wanajifunza ubunifu na kufanya mambo tofauti, wakirudi makwao wanafanya hivyo na kutuendeleza katika gurudumu la maendeleo. Anaweza mtu akawa Israel akawa mkulima mzuri kule, una teknolojia au njia ya kulima vyema, anarudi kwetu anatusaidia katika hilo. Huo ni mchango chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika kisiasa, kuna nchi ambazo zimeingia kwenye machafuko nyingi tu, mfano Iraq, Libya, Burundi, Somalia hata Kenya katika machafuko ya 2007. Diaspora wa nchi hizo walichangia mchango mkubwa sana katika kupata amani. Sasa nao huo ni mchango vile vile na wanachangia maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na la msingi zaidi ambalo nilitaka kujikita zaidi ni kiuchumi. Kiuchumi, wana-diaspora wanaweza kuchangia nchini mwetu kwa njia kuu mbili ya kwanza ni remittances ambazo zimezungumzwa na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na ya pili ni investment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, remittances ni zile fedha ambazo wana-diaspora wanawapa ndugu zao huku kuwasaidia kujikimu katika maisha yao na hizo zinapimwa. Nimefanya tafiti kidogo kwa nchi nne; Nigeria mwaka 2021/2022 remittances kutoka katika diaspora kwenda Nigeria zilikuwa dola bilioni 20, ndani ya mwaka mmoja. Ni fedha nyingi zaidi kushinda their largest export ya mafuta. Mafuta yanayouzwa nje yana thamani ndogo kushinda Wanaijeria waliopo nje wakileta kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya Wana-diaspora wapo milioni tatu, wamechangia mwaka 2021/2022 dola bilioni nne. Uganda wapo laki sita, wamechangia dola biloni 1.4. Sisi tumechangia mwaka huo huo dola bilioni 1.1 na bilioni 1.1 imeongezeka kwa kasi kubwa sana kulinganisha na mwaka uliopita ilikuwa milioni mia tano na kitu na ukiangalia cha msingi kabisa ni jinsi gani wana-diaspora wanajiona wanathaminika ndani ya nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nitoe pongezi kwa hatua ya kwanza ambayo imetuwezesha sisi kuongeza lakini ukiangalia wana-diaspora wa Uganda wako laki sita sisi tupo milioni 1.5. Wao wanachangia nchini mwao zaidi kuzidi sisi kwa nini? Hilo ndio swali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu inajikita katika Diplomasia ya Uchumi. Diplomasia ya Uchumi shamba lake kubwa ipo kwenye diaspora. Tukiweza kuwapa incentives wana-diaspora, tunaweza tukavuna mabilioni ya fedha mengi zaidi kushinda export yoyote ambayo tutaifanya hapa Tanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumalizia jambo moja tafadhali. Suala la uraia pacha na hadhi maalum. Uraia pacha tunaouzungumzia hapa Mheshimiwa Rais Nyerere kama msingi wa msimamo wetu. Tuna ahadi za Wanachama wa TANU au sasa CCM. Tuna ahadi mbili ambazo ni relevant katika hili ya kwanza binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi huu ulitumika kuwa-nationalize wakimbizi 200,000 wa Burundi Tanzania awamu ya kwanza, wakimbizi hamsini elfu wa Somalia awamu ya pili. Sasa ahadi ya pili ya mwanachama sote sisi tunaijua, nitatumikia nchi yangu na watu wake wote, narudia tena nitatumikia nchi yangu na watu wake wote. Wana-diaspora ni watu wetu, lazima tuwatizame tuwajengee hoja, tuwasaidie, kama sio uraia pacha, hadhi maalum. Tofauti yake ni ndogo, sio tofauti kubwa. Hadhi maalum inategemea unawapa haki gani, uraia pacha unaweza kuzuia mambo makuu mawili masuala ya siasa wasiweze kushiriki katika siasa na wasiweze kufanya kazi katika vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana umeeleweka sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)