Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara kwa uwasilisho mzuri wa bajeti pamoja na mikakati ambayo wameiweka katika bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maeneo matatu na kama muda utatosha nitaongeza moja la nne haraka haraka katika michango yangu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake ya kule Zanzibar kwa kuweza kuifanyia marekebisho makubwa Ofisi ya Zanzibar ya Mambo ya Nchi za Nje ambayo kwa sasa angalau ina mwonekano wa kweli wa Ofisi ya Mambo za Nchi za Nje. Ni tofauti na ilivyokuwa zamani, miaka mitano iliyopita, kwa kweli ilikuwa inatia aibu kama ni ofisi ya mambo ya nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu, kwamba pamoja na marekebisho tuliyofanya kwenye ofisi hii, naomba sasa twende kwenye changamoto ambazo zinakabili hiyo ofisi. Changamoto ya kwanza hiyo ofisi ina upungufu mkubwa wa watendaji. Kwa hiyo ningeomba tukaongeza idadi ya watendaji katika Ofisi ya Mambo ya Nchi za Nje ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala zima la vifaa na usafiri. Kwa kweli ni aibu Ofisi ya Zanzibar ukienda suala la usafiri ni gumu katika Ofisi ya Mambo ya Nchi za Nje ya Zanzibar na halikadhalika vitendea kazi. Kwa hiyo ni tegemeo langu kwamba Mheshimiwa Waziri na timu yake wataionea huruma Ofisi ya Zanzibar kwa kuipatia vifaa na usafiri ili iweze kuonekana kuwa na hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ningeomba pia kama kuna uwezekano tukatenga eneo hasa, sababu tumefanya marekebisho, lakini tutenge eneo tujenge Ofisi ya Zanzibar katika maeneo mengine sio katika eneo lile ambalo kidogo limejikunja hata parking za magari ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, wenzangu wameongelea kuhusu sera hapa na mimi vile vile niweke mkazo kwenye marekebisho ya sera, tuyafanye kwa haraka kwa sababu sera ya mwaka 2011, ni kipindi karibu miaka 23 sasa toka sera hii imetayarishwa. Sasa naomba tu kwamba tuweke mkazo kwenda kuitayarisha na kuitengeneza Sera ya Mambo ya Nchi za Nje ili kuweza kuakisi hii diplomasia ya uchumi ambayo tunaizungumza hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni suala zima la mambo ya royal tour. Mheshimiwa Waziri amefanya kazi nzuri kuzihamasisha baadhi ya balozi zetu nchi za nje na zimefanya kazi nzuri, lakini ombi langu sasa ni vyema tukawa tuna mkakati wa pamoja na miongozo ambayo itazitaka balozi zote ziwe na target ziwe na miongozo maalum ya kuweza kuifanyia kazi hii ripoti au hii video ya royal tour ili kuweza kutangaza na kufikia ile target au lengo la kufikia watalii elfu tano ifikapo mwaka 2025, kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyozungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niongelee suala zima la ushiriki wa Tanzania katika taasisi na mikutano ya kikanda na ya nchi za nje au ya kimataifa kwa ujumla. Kama unavyojua kwamba ili kuweza kupata hizi fursa kusema vizuri za mambo ya nchi za nje, ni lazima tuwe na watendaji wazuri ambao wameandaliwa, lakini pia tuandae mazingira ya Tanzania kwa ajili ya kupata hizi fursa ambazo ziko katika taasisi pamoja na mikutano ya kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano hapa, kuna mikutano ya kikanda ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kuna fursa nyingi za kiuchumi, lakini ukienda hivi sasa kuna tatizo kubwa kwamba hizi fursa hatujajiandaa vizuri kwa sababu kama ukiangalia, kuna accreditation institution moja tu Tanzania ambayo ni Bank ya CRDB, lakini bado wenzetu kuna baadhi ya nchi wana institutions ambazo zimesajiliwa zaidi ya nne, zaidi ya tano ambazo zinaweza zikatafuta hizi fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na sisi Tanzania tuandae watendaji, tuandae na hizi institutions zetu ziweze kuchangamkia hizi fursa za kifedha na shughuli nyingine mbalimbali katika hizi Jumuiya za Kikanda pamoja na mikutano ya umoja wa kimataifa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)