Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza nianze kabisa kuipongeza Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Dkt. Samia Hassan Suluhu ambaye ni mwanadiplomasia namba moja. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri lakini pia nimongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, baba yangu Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

Pia nimpongeze mama yangu Mulamula Mwenyezi Mungu akutangulie ili uweze kupata hiyo nafasi. Mungu akusaidie ili uweze kuipeperusha vyema Tanzania yetu na mimi nikiwa mkubwa nitakuwa kama wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitachangia kwenye diplomasia ya uchumi ambayo ni kipaumbele namba moja kwenye Wizara. Kabla sijaongelea kwenye hilo suala la diplomasia ya uchumi, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba bajeti iliyopita nilichangia kidogo kuhusiana na vikwazo vya wafanyabiashara ambao wanaliendea soko la Zambia, lakini wakifanya shughuli zao Zambia pamoja na kuliendea soko la Kongo kupitia Nchi ya Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatamani Mheshimiwa Waziri aseme neno, je. bado anaendelea kujua kwamba wafanyabiashara hawa wanaendelea kupitia vikwazo? W iki moja iliyopita walimfuata Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Nyongo kwa ajili ya kuendelea kuelezea changamoto zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye diplomasia ya uchumi kama ambavyo Wizara wenyewe wamesema kwamba ndio kipaumbele chao namba moja, lakini na maoni ya kamati wamesema kwamba diplomasia ya uchumi bado haijaeleweka kwa ufasaha kwa wananchi na hata kwa viongozi ambao wanasimamia sekta hizo, wakataja kwa mfano. Nitataka nisimamie zaidi kwenye maoni ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli diplomasia ya uchumi kwa wananchi wetu wa kawaida, bado hawajui diplomasia ya uchumi ni nini. Watu wengi wanafikiria diplomasia ya uchumi ni wale watu ambao wanapita kwenye red carpet na wale wavaa suti za dark blue pamoja na white color, lakini tunaamini kwamba diplomasia ya uchumi hapa ndio kwenye eneo ambalo limebeba ajira nyingi sana na zinaweza zikasaidia kukuza uchumi wetu kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitolee mfano, mwaka jana kama sio mwaka juzi, tulipewa soko kubwa sana kwenye nchi ya China kupeleka soya, lakini unaweza ukashangaa kwamba ilifika wakati sisi hatuwezi kupata soya hapa. Ilipelekea Watanzania wakawa wanachukua soya nyingi kutoka Zambia, yaani pale mpakani Tunduma ilikuwa ndio biashara, kila mtu anatafuta soya kutoka Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nikawa najiuliza sisi hapa kwetu tuna halmashauri 184, nikachukulia mfano tuchukue tu halmashauri 100 tu za wakulima mfano kule kwetu Momba, mia tu. Tungewapa target kwamba wazalishe tani za soya milioni moja halmashauri mia, maana yake kila halmashauri ingeweza kuzalisha soya tani elfu kumi ambayo ni kitu kinawezekana, lakini hatukuwahi kupata hilo soko kabisa na soya nyingi kwa kiwango kikubwa zilikuwa zinatoka Zambia na waliokuwa wanaenda kuchukua Zambia ni Watanzania hawa hawa. Tafsiri yake ni nini? Ni kwamba sisi tunasaidia kuwakuzia uchumi Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maandiko kidogo ambayo nilipata nafasi nikasoma kuhusiana na diplomasia ya uchumi namna ambavyo inaelezea, kwamba watu wenye uwezo wafanyabiashara, lakini na hata watu wa kawaida wa chini ambavyo diplomasia hii ya uchumi inawalenga. Inasema hivi diplomasia ya uchumi ni mbinu na mkakati unaotumiwa na nchi na mashirika ya kimataifa katika kukuza maslahi yao ya kiuchumi nje na mipaka yao. Lengo la diplomasia ya uchumi ni kuimarisha ushirikiano wa uchumi kibiashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiufundi kati ya nchi na kuboresha hali ya uchumi kitaifa. Diplomasia ya uchumi inahusisha shughuli kadhaa ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaendelea: Nchi zinatumia diplomasia ya uchumi kukuza biashara na uwekezaji kwa kuvutia wawekezaji na kujenga mazingira mazuri ya biashara. Hivyo, wafanyabiashara kusaini mikataba ya biashara na makubaliano na wawekezaji kushirikiana katika masuala ya kifedha na kibenki. Aidha, ushirikiano wa kiufundi, diplomasia ya uchumi inahusisha pia kubadilishana maarifa na teknolojia. Nchi zinaweza kuweka mikataba ya ushirikiano wa kiufundi katika maeneo ya kilimo hapa kwenye kilimo ndio tunajiongelea sisi watu wa Momba na halmashauri zingine ambazo wanalima, afya, nishati, miundombinu na teknolojia ya Habari. Kwenye teknolojia ya habari ndio kwenye mambo ya block chain technology na mawasiliano. Hii inaweza kuimarisha teknolojia na ujuzi na inachangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi zinazoshirikiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameendelea wanasema, katika diplomasia ya uchumi nchi zinaweza kutuma wawakilishi wa Serikali kama mabalozi wa uchumi au wajumbe wa biashara kwenye nchi zingine. Hao hufanya mazungumzo na kuwakilisha Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia tu kidogo. Fursa za biashara na ushirikiano wa kiuchumi. Diplomasia ya uchumi kwa kumalizia anasema, malengo ya diplomasia ya uchumi ni pamoja na kuongeza mauzo ya nje na bidhaa na huduma za nchi. Kujenga mtandao wa biashara wa washirika wa kimataifa, kuvutia wawekezaji wa kigeni, kukuza viwanda vya ndani. Sasa tutakuzaje viwanda vya ndani kama hatumshirikishi mwananchi wa kawaida huyu anayefanya shughuli ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, niombe kwamba, Wizara ilikuwa inasema inatoa elimu mbalimbali kwenye mambo ya diplomasia ya uchumi kwenye magazeti, redio na vitu kadha wa kadha. Niombe elimu hii iende kule kwenye Baraza letu la Madiwani. Wizara ya Mambo ya Nje waweke dirisha kwenye Wizara ya TAMISEMI ambao wao wanazijua halmashauri na uwezo wao. Wanajua vipato vya halmashauri ipi ina mapato kidogo, halmashauri ipi inafanya kazi gani.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Tunaomba Wizara ya Mambo ya Nje watusaidie katika hili ili diplomasia ya uchumi iende kwa wanachi wa kawaida kabisa, ahsante sana. (Makofi)