Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ambayo inatupeleka katika uso wa Dunia. Zaidi namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chief Hangaya, kwa namna alivyopata nafasi hii alikwenda moja kwa moja kuifungua nchi kwenye diplomasia ya uchumi ambapo sasa nchi inasonga mbele tunaelekea kwenye kipato cha kati na huenda tukaingia kwenye kipato cha kwanza. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kitu Balozi ni kitu chenye hadhi kubwa sana, nchi yetu ina hadhi kubwa sana nchi za nje tofauti na tunavyoifikiria. Jina Tanzania ni Tanzania kweli. Nchi yenye ufahari, utulivu, mito, mimea na nchi yenye mali kila siku nchi hii inavumbua mali mbalimbali. Sasa, lazima tujitafaharishe na tujifaharishe zaidi kwamba hii ni nchi tamu na nchi ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebatika kutemebea nchi mbalimbali kama Amerika, Bara la Ulaya na nchi mbalimbali, nilipata bahati ya kutembea Marekani katika Mji wa Seattle kwenye ujumbe na Makamu wa Rais wa Zanzibar. Jinsi ya utamu wa nchi hii kuna Mmarekani alitusimamisha aliuliza naomba msimame nikuulizeni maswali, ninyi mnatoka wapi, tukamwambia sisi tunatoka Tanzania akasema na mimi ni Mtanzania na kwa Kichaga akasema yeye alikuwa na Kihamba kwamba ana kijishamba chake cha Tanzania. Kwa hiyo, akasema ninyi mna nchi nzuri, utulivu wenu umefanya nchi ifunguke na nchi yenu imetulia na ina amani. Kwa hiyo, hongereni sana kuja hapa America. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayakuja tu lazma niwampongeze Mheshimiwa Waziri na timu yako Mheshimiwa Dkt. Mbarouk kwa kuisimamia vizuri, mnafanya kazi nzuri, hamlali na hamchoki, Mwenyezi Mungu akupeni afya na muihudumie zaidi nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika diplomasia ya kiuchumi kuna mambo na fursa mbalimbali zinapatikana hasa za uchumi. Mashirika yafuatayo yameweka mkono wazi kwetu Tanzania, kama vile World Bank, IFAD, FAO, UNDP, African Bank, BADEA, Kuwait Fund na mashirika mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapochukuliwa Balozi iwe unapata ripoti ya kila siku kwamba neno gani au jambo gani Tanzania lina manufaa nchi iko wazi. Kwa utundu wangu kuna siku nilikaa mgongoni kidogo World Bank kwenye corridor zile mbili, nikapata na bahati nikakaa kidogo nikachukuliwa nikaona kwamba World Bank corridor mashirika makubwa ya dunia yamekaa yanagojea tuende tukawaombe au tukakape pesa zetu. Kwa mfano, Zanzibar mradi wa PADEP, mradi wa MANCEP hii ni juhudi binafsi za Makatibu Wakuu kwa wakati ule na viongozi, mradi ule leo unawafaa Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi kwa hapo tu naomba Balozi zetu zichangamke fursa zipo, zituletee maendeleo ili nchi iwe na neema kwa hii fursa ya uchumi wa Bluu. (Makofi)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Mwanaisha.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, anayoyazungumza kuhusiana na Balozi zetu kuiendea kwa kasi dhana nzima ya diplomasia ya uchumi, Balozi zinapaswa kukumbuka pia zitafute uwekezekano wa nchi zetu kuanzisha benki katika zile nchi ambazo tunafanya nazo biashara kwa karibu. Kwa sababu tunaingiza intermediate currency ambayo inampotezea Mtanzania fedha nyingi anapokwenda kununua mizigo kama China na nchi za namna hiyo, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Engineer Ulenge kwa mikono yote miwili. Basi mimi taarifa yangu ni hiyo Balozi zichangamke fursa zipo nyingi, nchi iendelee mbele ili lengo la Rais wetu litimie la diplomasia ya uchumi, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)