Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa rehema kwa kuturuzuku uhai na afya njema na kutuwezesha kujadili hotuba hii siku ya leo. Aidha, nichukue fursa hii ya kipekee kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na kuhudumu katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri na maelekezo yao katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na wewe binafsi pamoja na wenyeviti wote kwa namna mnavyoliongoza Bunge letu kwa hekima, busara na umahiri mkubwa. Aidha, naomba kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, ulinzi na usalama kwa maoni na ushauri wao ambao wamekuwa wakitupatia na pia kupitia taarifa iliyowasilishwa asubuhi hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Kamati makini sana na Wajumbe wake wana uelewa mkubwa wa masuala ya Kidiplomasia na hivyo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa ambao umeendelea kusaidia na kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara yetu na diplomasia ya nchi yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax, Mbunge, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa uongozi wake mahiri na ushirikiano mkubwa anaonipatia mimi binafsi na wenzangu ndani ya Wizara. Kwa hakika uongozi wake, miongozo yake na michango yake kwa kweli inatufanya kwenda katika direction nzuri zaidi na kuwa chachu ya ufanisi wa Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yetu kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwao, bila kuwasahau Mabalozi wetu wote ambao wanatuwakilisha sehemu mbalimbali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapenda kuishukuru familia yangu kwa upendo na uvumilivu wao kwa kuendelea kuniunga mkono wakati nikitekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, lakini kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na kutoa maoni yao katika hoja ambayo imeletwa na Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki. Vilevile, ninashukuru kwa pongezi nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamezitoa kwa Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, tunawaahdi Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tunapokea pongezi hizi na kutekeleza majukumu yetu kwa bidii na ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi wa hoja iliyoelezwa hapa kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Kwanza naomba nieleze kwamba pamoja na kuchelewa huko Tanzania muda wote huo imekuwa ikitekeleza wajibu wake kama Host Country Agreement kwa kuipatia Mahakama hiyo Ofisi za Mahakama, nyumba ya Rais wa Mahakama na nyumba ya Msajili wa Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ili Mahakama hii iwe na majengo yake ya kudumu katika mwaka huu wa fehda kiasi cha shilingi bilioni Nne tayari zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo ambazo zitakuwa katika eneo la Laki Laki huko Arusha. Hivi sasa Wizara inakamilisha malipo ya awali kwa Mkandarasi na tarehe Mosi Juni, 2023 ambapo ni kesho kutwa tu, Wizara itakabidhi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi ili aweze kuanza maandalizi ya awali ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna hoja hapa ilizungumzwa kuhusiana na changamoto za visa hasa kwa vijana wetu wanaokwenda masomoni nje ya nchi. Naomba nikiri kwamba ni kweli baadhi ya muda kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya vijana wetu ambao wanakwenda kusoma huko nje. Hata hivyo, Wizara imekuwa ikisaidia kwa kadri inavyoweza ili wanafunzi hao wapate VISA na hivyo kupata fursa ya kwenda kusoma. Aidha, ililetwa rai hapa kwamba Wizara ianzishe Idara ya Fursa lakini naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna Idara ya Diplomasia ya Uchumi na kwa hiyo tunachukua huo ushauri wake ili hizo fursa hizo ziwe katika Idara ya Diplomasia ya Uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nieleze kuhusu Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyoko Zanzibar. Kwanza, tunashukuru sana kwa Mheshimiwa Mbunge Soud kutambua juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba tuko katika maeneo mazuri ya kufanyia kazi. Pia, naomba kulifahamisha Bunge lako kwamba, suala la wafanyakazi hivi sasa liko katika hatua za mwisho la kulipatia ufumbuzi na hivi karibuni kuna Maafisa kama wanne hivi wataajiriwa hapo. Pia kuhusu suala la samani tayari Wizara imekwishaweka samani nzuri za kisasa katika Jengo la Ofisi zetu huko Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la usafiri wa gari, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari mwezi uliopita gari aina ya landcruiser tayari lilishapelekwa Zanzibar kwa ajili ya Ofisi zetu.

Mwisho kuhusu kujenga Ofisi zetu za kudumu, naomba kulieleza Bunge lako tukufu kwamba, hivi sasa tuko na majadiliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili waweze kutupatia eneo hilo na tayari eneo hilo linaweza kupatikana eneo la Tunguru kwa ajili ya ujenzi huo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda umekwisha. Kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)