Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuendelea kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niendelee kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Wapo watu wachache sana ambao Rais anaposifiwa huko nje wanaumia kweli kweli, ninachotaka kusema tunaosimama hapa na kumsifia Mheshimiwa Rais ndiyo tunaoijua kazi ambayo Serikali inafanya. Kwa mfano, leo ninaposimama hapa kumsifia Rais, ninamsifia kwa kuutoa mradi wa Mwalimu Nyerere kutoka asilimia 37 alizozikuta hadi asilimia 87 leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapomsifia Rais wetu tunamsifia mradi mkubwa wa kusambaza gesi asili katika nchi yetu unapokwenda kupata mwanga chini ya Waziri wake January Yusuf Makamba ndiyo maana tunamsifia Rais. Kwa hiyo, wale wachache wanaoona tunamsifia Rais wanaumia, mimi nashauri tu tunapoanza kuzungumza kama hivi wawe na glasi ya maji wanakunywa huwa inasaidia sana kupooza chuki na hasira. Mtu mwenye chuki, hasira, wivu ukinywa maji inapungua lakini Mama Samia anastahili sifa hizi na tutaendelea kuzitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge wanaohudumu katika Kamati inayosimamia Wizara hii, Kamati ya Nishati na Madini. Kwanza kabisa ningependa niipongeze kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wasaidizi wao wote kwenye taasisi zote hizi Sita zinazosimamiwa ambazo ni TANESCO, TPDC, EWURA, REA, PBPA Na PURA) ambapo taasisi hizi zote ziko chini ya Wizara ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili kwamba, katika mjadala tulikuwa tunatazama na kuishauri Serikali hata taasisi mbili ambazo zinajihusisha na shughuli za nishati na haziko chini ya Wizara ni vizuri sasa Serikali ifikirie kuzichukua taasisi hizo ziwe chini ya Wizara. Taasisi kama vile TIPER na PUMA energy ambazo ziko chini ya Msajili wa Hazina lakini zinafanya kazi za nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano leo hii TIPER ingekuwa inasimamiwa na Wizara ya Nishati moja kwa moja inawezekana kabisa kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi kuliko saa hivi imebaki kama kazi yake ni ku - store mafuta tu yanayowekwa katika matenki ya TIPER. Kwa hiyo, naishauri Serikali hizi taasisi mbili zisimamiwe na Wizara ili Wizara ambayo inasimamia shughuli za maendelo ya nishati izipangie kazi zaidi na kuleta tija zaidi kuliko kusimamiwa na Msajili wa Hazina ambae kazi yake ni kuangalia hisa zetu na faida ambazo zinazozalishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nirudie pongezi zangu kwa Serikali, kwa kazi kubwa iliyofanywa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, hii inakwenda kutusaidia kufanya mambo makubwa katika Taifa letu. Kigoma tumejiandaa kuipokea neema hii, maana tunakwenda kuunganishwa na umeme wa kilovolt 400 kutoka Nyakanazi kuja Kidahwe na Mkoa wetu mzima utaunganishwa na Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi hii unayoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais, endelea kuchapa kazi na sisi tunakuunga mkono. Kupitia nafasi hii nikuombe Mheshimiwa Waziri katika Jimbo langu la kigoma Mjini, eneo la Kagera na Businde, Kata ya Kagera na Businde pamoja na kwamba ziko katika Manispaa ya Kigoma Ujiji lakini haya ni maeneo ya peri urban, mradi wa REA uendelee kuwapa huduma wananchi katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo nataka nizungumze ni suala la bei ya mafuta, nimewahi kulizungumza hapa nalirudia tena. Nalirudia tena nakujua Mheshimiwa January Makamba ulivyo mtu msikivu, mchapakazi mwadilifu na mzalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mafuta inatofautiana kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine katika nchi yetu lakini bei ya umeme ni moja nchi nzima, uwe ni umeme wa mafuta, uwe ni umeme wa gesi, uwe ni umeme wa maji waliounganishwa kwenye grid ya Taifa wanaotumia umeme wa majenereta wote umeweka unit ni bei moja. Kwa nini mafuta ya nishati yasiwe bei moja nchi nzima? Jambo hili naomba ulifanyie kazi linawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza Kigoma lita moja ya mafuta ya diesel na petrol ni shilingi 3,034 lakini Dar es Salaam ni shilingi 2871, ukinunua lita 1,000 tu tofauti yake ni karibu shilingi 180,000 kutoka Dar es Salaam kuja Kigoma, na huku ambako bei inakuwa kubwa ndiko ambako watu wana maisha magumu, ndiko ambako kila kitu ni bei kubwa, hebu kaa na wataalamu wako, unao watu wazuri mtazame jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni lile ambalo limeelezwa na wenzangu kuhusu mafuta, suala la vinasaba. Tulikaa hapa Bungeni tukaishauri Serikali baada ya kuona kwamba kuna baadhi ya mambo hayaendi vizuri katika suala zima la vinasaba kwenye mafuta, suala hili likahamishwa kutoka kusimamiwa na EWURA likapelekwa TBS. Huko sasa ndiyo mambo yanaonekana magumu zaidi. Ndugu zangu tunataka tufahamu kitu kimoja, kujikosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi. Sisi tunaweza tukajikosoa katika mambo ambayo tunaona tumeamua lakini tumekwenda kwenye utekelezaji hayaendi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo yanajitokeza sasa hivi, baadhi ya Vinasaba vinawekwa lakini EWURA wanapokwenda kukagua wanakuta hakuna vinasaba ni kwamba lipo tatizo. Pia chini ya EWURA kabla haijaenda TBS hizi kampuni za SICPA na GFT zilikuwa zinafanya vizuri, hawa SICPA wameendelea kufanya kazi hapa nchini kwa uaminifu na sasa hivi wanafanya kazi na TRA, kwa nini jambo hili tusilirudishe tena EWURA wakalitazama na wakafika mahala wakalifanya vizuri zaidi, TBS wana mlolongo wa vitu vingi sana wanavyoviangalia katika ubora, lakini EWURA ni maji na mafuta peke yake. Kwa hiyo, bado tunaishauri Serikali kurudi nyuma kujitazama si jambo baya katika kujiimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tumepiga hatua kubwa sana chini ya Waziri January Makamba, tunaona mwanga wa kwenda Kumtua Mama Kuni Kichwani, kupata nishati safi. Nilikueleza hata tukiwa kwenye semina, umeme ukiwa na shilingi 1,000 unanunua umeme wa 1000 unawasha taa, ukiwa na shilingi 2000, ukiwa na 3000 lakini gesi kuna mtungi wa chini unaanza sijui shilingi 23,000 unakwenda 50,000, kwa wananchi wa kwetu huko vijijini wanapata shida. Kwa hiyo fikiria kuwa na gesi inaanzia shilingi 1000 mtu anakwenda anajaza gesi yake ya 1000 anatumia. Siku akipata 3000 anajaza 3000 anatumia. Kukusanya shilingi 22,000 kwa baadhi ya familia ni suala la kikao cha familia nzima watu wakae kujadili kupata shilingi 23,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja nawatia moyo sana, endeleeni kuchapa kazi kwenye Wizara hii mnakwenda vizuri sana. Ahsanteni.