Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa furasa na mimi leo kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na mimi siku ya leo kuweza kuchangia bajeti hii ya nishati.
Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa kutuwakilisha kwenda kushuhudia uapisho wa Rais wa Nchi ya Nigeria, vivyo hivyo kuendelea kutuwakilisha sana Watanzania katika mambo mbalimbali kimataifa. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara, kaka yangu January Makamba. Kazi kubwa unaendelea kuifanya katika nchi hii kama alivyosema dada yangu Tauhida hapo. Sisi wananchi na hasa wananchi wa Jimbo la Msalala tunakuelewa. Tunakuelewa kwa ukarimu wako, tunakuelewa kwa uchapaji kazi wako; na wananchi wameniagiza kwa wema uliyowatendea baada ya wewe kufika katika Jimbo la Msalala kutuona, kututembelea na kutusikiliza maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo kwenye maeneo yetu ya Msalala. Nimpongeze sana kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya lakini pia nimpongeze Naibu wako Waziri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Mkurugenzi Mkuu wa REA kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii mimi nimesimama hapa kuwawakilisha wananchi wa Msalala kuhusiana na kero mbali mbali zinazohusu suala la umeme. Mheshimiwa Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Cherehani amezungumza asubuhi hapa kupongeza jitihada mbalimbali ambazo zinaendelea kwenye Wilaya yetu ya Kahama na hasa Mradi wa REA ambao unaendelea kutekelezwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikili ni kweli hapo mwanzoni palikuwa pamesuasua sana lakini sasahivi mkandarasi anaenda sawa sina haja ya kurudia kwa sababu Mheshimiwa Mbunge mwenzangu Cherehani amelizungumza jambo hili. Hata hivyo, niongezee hapo tu kidogo katika kumuhakikishia kwamba huyu mkandarasi anaenda ku-perform vizuri Mheshimiwa Waziri sisi wananchi wa Kahama, tunaomba huyu mkandarasi aweze kuongezewa zile kilomita mbili ili awe anamaliza kabisa ili kumuondolea usumbufu baadaye kuwa anarudi kuja kutekeleza zile kilomita mbili ambazo zimebaki. Kwa hiyo nikuombe sana muongezee mkataba. Sambamba na hilo kwa sababu ya vifaa niombe Mheshimiwa Waziri nendeni mkajaribu kuona utaratibu wa kumfungulia LC ili aweze kupata material kwa wakati, aweze kutimiza miradi hii kwa wakati ili wananchi wa Jimbo la Msalala na Wilaya ya Kahama waweze kunufaika na miradi hii ya umme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi amelizungumza Mbunge mwenzangu na mimi naomba nikazie. Wilaya ya Kahama ndiyo Wilaya ambayo inaongoza kwa kukusanya mapato yatokanayo na umeme kwenye Mkoa wa Shinyanga. Utaona makusanyo kwenye Mkoa wa Shinyanga ni takribani bilioni 16, lakini kiasi cha shilingi bilioni 13 zinatoka kwenye Wilaya ya Kahama. Ukitazama hapo utaona Wilaya ya Shinyanga Mjini ni bilioni mbili na Wilaya ya Kishapu ni kama bilioni moja na kitu. Kwa hiyo Wilaya ya Kahama ni eneo muhimu sana katika uwekezaji wa sekta ya umeme. Kwa hiyo nikuombe sana weka jicho lako katika kuwekeza kwenye Wilaya ya Kahama ikiwemo kuanzisha Mkoa wa ki-TANESCO.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia Mkoa wa Dar es salaam wameanzisha mikoa minne ya ki-TANESCO, sasa tunashindwa nini kuanzisha Mkoa wa ki-TANESCO katika Wilaya ya Kahama ili tuweze kuhakikisha ya kwamba tunasogeza huduma hii kwa haraka kwa wananchi wetu lakini pia tuone namna ya kuweza kusaidia watu ambao wanatoka kwenye maeneo mbalimbali kwenye maeneo yetu? Kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri hili jambo la kuanzisha kwenye bajeti hii twende tukaanzishe Mkoa wa ki-TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na nimwambie Mheshimiwa Waziri, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kahama anafanya kazi kubwa sana. Wilaya ya Kahama ina halmashauri tatu, na ule ni sawa sawa na mkoa. Lakini pia kutokana na shughuli nyingi na maeneo mengi inanuwia vigumu meneja huyu kufika kwenye maeneo yale. Kwa hiyo niombe, baada ya kuanzishwa Mkoa wa ki-TANESCO katika maeneo yale, mkianzisha na ofisi kubwa za wilaya katika halmashauri zetu inatusadia sana kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ile huduma kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, wafanye mazungumzo na hawa watu wa TRA. Wananchi wanalalamika kwamba kumekuwa na tabia sasa hivi, hasa ile kodi ya majengo ambayo inakatwa kwenye umeme. Kumekuwa na ulimbikizaji wa kodi ile haikatwi kwa wakati matokeo yake wananchi wetu ambao wana uchumi duni wa kununua umeme unakuta mtu anaenda kununua wa shilingi 10,000 wakati huo huo anadaiwa shilingi 6,000 au 10,000 hiyo, inakatwa na anapata unit ndogo. Kwa hiyo niombe mfanye coordination ya ninyi pamoja na TRA waweze kukata kodi ile mapema iwezekanavyo ili kuondoa mzigo mkubwa kwa wananchi wetu hawa kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimempongeza sana Mheshimiwa Waziri, nisisahau kumpongeza meneja wangu wa mkoa anafanya kazi kubwa sana Mkoa wa Shinyanga, nisisahau kumpongeza meneja wa kanda anafanya kazi kubwa sana. Bila ya hawa maendeleo huko kwetu, hasa katika sekta ya nishati yatashuka. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, siku zote huwa anazungumzia habari ya umeme, kwamba unapozungumzia umeme ni mambo matatu; uzalishaji, sina shaka na uzalishaji kwa sababu mambo mengi yanafanyika, anazindua miradi mingi, na juzi tumemuona Mheshimiwa Rais akiizindua Mradi wa Rusumo kazi kubwa inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu usafilishaji sina shaka na usafilishaji, usambazaji sina shaka na usambazaji. Nataka nimuongezee hapo Mheshimiwa Waziri, aende akaanzishe suala jingine la ukusanyaji, TANESCO waweke mikakati mizuri ya kukusanya mapato kwenye maeneo yetu ili kuiwezesha TANESCO kuweza kusimama na kutengeneza faidi lakini pia kulipa madeni mbalimbali kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba EWURA wametenga fedha kwa ajili ya kukopesha vijana wetu, kuanzisha vituo vya mafuta kwenye maeneo ambayo yana umbali mrefu kwenye vituo hivi vikubwa vya mafuta. Niombe kwenye maeneo hayo Mheshimiwa Waziri watafute namna ya kutoa semina nzuri kwa vijana wetu. Kuona ni namna gani wanaweza kupata taarifa sahihi ya namna gani wanaweza kupata mikopo hii ili na wao waweze kutumia fursa hii ya mikopo ya kuanzisha vituo vidogo vidogo vya mafuta kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo kwa Mheshimiwa Waziri sasa naomba nizungumze suala moja zuri sana. Sitaki kuzungumza leo habari ya mafuta, na nimeona kwenye bajeti yake Mheshimiwa Waziri hapa amezungumzia habari nzuri ya mafuta. Mimi nataka leo nizungumze habari ya lubricant, kwa maana ya vilainishi.
Mheshimiwa Spika, biashara ya vilainishi kwenye nchi hii ni biashara kubwa sana. Kama Wizara hawataweka jicho katika kuhakikisha kwamba wanadhibiti uingizwaji wa lubricants, kwa maana ya vilainishi fake kwenye nchi hii itaendelea kutia hasara kubwa sana wananchi wetu katika maeneo haya. Mimi ni shuhuda nimeweza kuweka oil kwenye gari langu imeharibu engine.
Mheshimiwa Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, wananchi wengi wanaharibikiwa engine zao ni kwa sababu ya uingizwaji wa oil ambazo ni fake kwenye hii. Sasa niombe kwenye Wizara hii na EWURA, kupitia TBS waweke udhibiti mzuri ili kuhakikisha kwamba oil zinazoingia nchini ziwe ni oil ambazo zimethibitishwa na TBS kwa ajili ya kumlinda mtu anayekwenda kutumia. Tunaingia hasara kubwa sana ya gari zetu, tunaingia hasara kubwa sana kununua vilaishi hivi fake.
Mheshimiwa Spika, na hasa utaona kuna viwanda vingi bubu ambavyo vimeanzishwa kwenye maeneo hayo, wananunua oil ambazo ni chafu ni kwenye maeneo yale, wanazisafisha oil zile, wanaofanya package kwenye maeneo yale na matokeo yake tunaenda kuuziwa oil ya Total kumbe ni oil ya Total ambayo ni fake. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri waanzishe utaratibu wa kuwasajili wauza oil na vilainishi kwenye nchi hii ili kuwalinda wawekezaji wetu kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumze suala zima la namna ya kulinda biashara hii katika nchi hii. Katika makubaliano ya Mheshimiwa Waziri na nchi za East Africa, hasa Kenya, katika ushindani wa biashara hii utaona hapa Tanzania na Kenya kumekuwa na competition kubwa. Uanzishwaji wa viwanda vya vilainishi kwenye nchi imekuwa changamoto yake ni kubwa. kwa sababu ya kodi ambayo tunaweka kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, utaona wamekubaliana kwamba import duty ya lubricant katika nchi hii na katika East Africa iwe ni 10 percent, lakini ukienda Kenya utaona kabisa Kenya wameweka 16 percent VAT lakini huku sisi tumeweka 18 percent VAT na kodi mbalimbali zingine. Kwa kufanya hivyo wamefanya viwanda vingi viende vikaanzishwe Kenya na wamefanya sasa iwe kwamba kununua oil Kenya ni rahisi kuliko kununua oil hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, yeye pamoja na Waziri wa Fedha wakae chini waone namna ya kupunguza na kuondoa kodi hizi mbalimbali ambazo zitaweka usawa wa nchi za East Africa ili kuwawezesha wawekezaji kwenye maeneo haya kuja kuwekeza viwanda vikubwa vya kutengeneza oil hapa nchini, oil iliyo na ubora, oil ambayo yenye kiwango kilichothibitishwa na TBS ili kuondoa hili wimbi la kuingiza oil chafu kwenye maeneo ya nchi yetu hii.
Mheshimiwa Spika, mwisho kwa Mheshimiwa Waziri nataka nizungumze habari ya vijana wetu ambao wanasoma masuala ya umeme kwenye vyuo vyetu. Tunao vijana wengi wamesomea umeme, wamehitimu kwenye vyuo vyetu, lakini hii kwa mkakati alionao Mheshimiwa Waziri wa kupeleka umeme kwenye vijiji na vitongojini tunategemea mafundi ambao wanaenda kufanya installation kwenye nyumba za watu wetu kwenye maeneo yale leo hii hawajathibitishwa, hawajapata ithibati, hawajawa registered kwenye CRB. Matokeo yake ni kwamba mtu anakwenda kufunga umeme kwenye nyumba, anatumia kiasi cha shilingi 50,000 mpaka 100,000 kwenda kumuona mkandarasi tu amgongee muhuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sasa nimuombe, ili kutengeneza ajira ya vijana wetu hawa ambao wamemaliza chuo kwenye maeneo hayo muweke utaratibu mzuri wa kuwasajili hao vijana ambao wamemaliza chuo waliyosomea mambo ya umeme, waweze kuwa na uwezo wa kwenda kuhakikisha ya kwamba wanathibisha na kugonga mihuri fomu zile kuondoa usumbufu na kutengeneza ajira kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo niombe sana, gharama, kama alivyosema hapa Mbunge mwenzangu Kenneth Nollo, muangalie na mtuambie ukweli gharama ya shilingi 27,000 inalipa? na kama hailipi mje na mkakati wa kuona namna gani mnaboresha. Kwa sababu utaona wametangaza shilingi 27,000…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa kengle imeishagonga, malizia sentensi. (Makofi)
MHE. IDDI. KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Wao wametangaza shilingi 27,000, lakini ukiangalia mtu unakwenda kuvuta umeme fundi anachaji 100,000 kwa ajili ya kugongewa muhuri, lakini pia kufanya installation kwenye nyumba ni zaidi ya 100,000 mpaka 200,000. Kwa hiyo gharama inarudi kule kule. Kwa hiyo niombe waliangalie suala hili haraka iwezekanavyo na watueleze ukweli wa jambo hili ili tuweze kuwaelewesha wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa unayo endelea kuifanya, ahsante sana. (Makofi)