Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nami napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Awali ya yote, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Hasna Mwilima baada ya kupata ushindi usiokuwa na shaka na Mahakama imetenda haki. Hii imeonesha jinsi ambavyo kwa kweli, kesi nyingi zinafunguliwa hazina mashiko yoyote ndiyo maana Sheria inaposimama CCM inachanua.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, najua hujasikia na wala hukuona kwa sababu, Wagogo mna sifa ya kutokuona na kusikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwa michango ya wenzangu, wamesema mambo mazuri, wakati mwingine ushauri kama huu lazima Serikali iusikilize. Ushauri ambao unakuwa na tija, ushauri ambao unakuwa na mwelekeo wa kujenga Serikali yetu na nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu ndugu zangu wanaposema yatumbuliwe majibu sijui wapi! MV Dar-es-Salaam na kadhalika. Jamani, msubiri! Mbona mnakuwa na haraka! Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati ya kuweza kusafisha Serikali yake na kuunda nchi hii ili iweze kuwatumikia Watanzania wote, kwa hiyo, msiwe na haraka, kila kitu kitakwenda hatua kwa hatua. Haiwezekani leo hii ukaanza kutembea na ukaanza kukimbia! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini katika Hotuba hii naona Mheshimiwa Waziri hajazungumzia suala la mikoa mipya na wilaya mpya, kwa sababu, wilaya hizi na mikoa mipya ina miundombinu ambayo kwa kweli, ni kama haipo. Sijaona kwenye bajeti mkakati mahususi kwamba, ni kwa vipi barabara hizi zitaimarishwa ili kuifanya mikoa hii na wilaya hizi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Simiyu hata kwenye Hotuba haujaunganishwa na barabara ya kwenda Singida wala Arusha! Ningeomba katika Hotuba hii Mheshimiwa Waziri, hebu tuainishie kwamba, hata usanifu au upembuzi yakinifu ni lini utafanyika kuiunganisha Simiyu na Singida? Leo hii kuna barabara, lakini haijatajwa Mheshimiwa Waziri, ningeomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika barabara ya kutoka Maswa kwenda Bariadi, kilometa 50, hata hazijatajwa Mheshimiwa Waziri hapa, lakini barabara kutoka Maswa kwenda Mwigumbi inawekewa lami na Mkandarasi yupo! Sasa ni kitu cha kushangaza, unaanza kujenga unaacha kipara katikati! Tunafanyaje kazi namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri katika kuhitimisha hotuba yake, ningependa kusikia mkakati kwamba, zile kilometa 50 za kutoka Maswa kwenda Bariadi, Makao Makuu ya Mkoa. Sisi watu wa Simiyu tuliamua wenyewe kwamba, Makao Makuu yawe Bariadi tena kwenye RCC na Mikutano yote ya hadhara, wananchi wakaunga mkono na hatuna ubishi na hilo. Kwa hiyo, ningeomba sana hili liweze kuzungumzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kingine tunataka kuimarisha uchumi wetu. Hivi unaimarisha vipi uchumi kama Dar-es-Salaam Bandari yenyewe imefungamana? Hata namna ya kusafiri kutoka nje ya Dar-es-Salaam haiwezekani! Magari, mlundikano na hata namna ya kupenyeza mizigo inakuwa ni tatizo! Tumepata wawekezaji wako tayari kuwekeza zaidi ya Dola milioni 200 kujenga Bandari Kavu pale katika Kijiji cha Soga, Kibaha.
Mheshimiwa Spika, leo ni miaka miwili na nusu, wanakwenda, wanarudi, Serikali imeshindwa kutoa maamuzi. Hivi kwa nini Mheshimiwa Waziri akiwa mwenye dhamana hii asione kwamba leo Mheshimiwa Rais anatafuta wawekezaji, wawekeze katika nchi hii na Dar es Salaam aweze kuifungua, haya malori ya mizigo hayapaswi kuingia Dar es Salaam, yakwamie huku bandari kavu.
Mheshimiwa Spika, hata barabara Waheshimiwa wamezungumza kwamba barabara ya Chalinze kuelekea Dar es salaam imekuwa kama chapati, ni kwa sababu gani? Kwa sababu mizigo mikubwa inatokea sehemu moja inapita sehemu moja. Lazima tuziokoe barabara zetu, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri anapohitimisha mjadala huu anipe maelezo ni kwa nini tunachelea kupata wawekezaji ambao wako tayari. Kama ni suala la kuzungumza mnaweka terms and condition, mnakubaliana ili tuweze kuifungua Dar es Salaam, mizigo isianzie Bandari ya Dar es Salaam, mizigo ianzie mahali ambapo kuna dry port na tuweze kuokoa uchakavu wa barabara zetu. Katika hili ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atupatie majibu.
Mheshimiwa Spika, kingine, unapokuwa na TRL halafu mwenye assets ni RAHCO, hivi inawezekana namna gani? TRL ha-own any asset zaidi ya zile TRL commutive peke yake. Sasa anakuwa na uwezo gani hata wa kukopa? Hawezi kukopesheka huyu, lakini huyu mwenye RAHCO yeye ndiye mwenye mtandao wote, lakini hana uwezo wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, ningeomba Mheshimiwa Waziri, suala la Reli na RAHCO aunganishe, aache reli asimamie assets zote zile aweze ku-transact vizuri, aweze kukopesheka na tuweze kuona reli. Naomba sana hii ndiyo njia pekee inayoweza kufufua uchumi wetu, tunaimba uchumi hatuwezi kufufua uchumi wetu kama hatuwezi kuwa na fikra za namna hii na naomba majibu ya subiri, tuachane nayo. Mheshimiwa Rais anasema kwamba, hapa ni Kazi tu, naomba na nyie Waheshimiwa Mawaziri sasa muwe hapa kazi tu, mambo ya kuchelewa kufanya maamuzi tuachane na biashara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja katika suala la uwanja wa ndege wa Mwanza, uwanja wa ndege wa Mwanza una kila sababu za kiuchumi, kimaendeleo na hata za Kikanda. Ukisimamia uwanja wa ndege wa Mwanza zaidi ya mikoa 10 umeihusisha na nchi jirani. Naomba upewe kipaumbele, uwanja huu uweze kukamilika, uwe uwanja wenye hadhi ya Kimataifa ili tuweze kuifungua Kanda ya Ziwa na Mikoa pamoja na nchi jirani kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, hii tunazungumzia kuongeza Pato la Taifa. Ukifungua uwanja wa ndege wa Mwanza ukawa wa Kimataifa, ukawa Serengeti International Airport, tayari ile Serengeti corridor yote umeifungua, tayari umeweza kuvutia wawekezaji, watalii na ndiyo maana uchumi ambao tunauhitaji leo kutoka Mwanza kwenda Entebbe ni dakika 30, Kigali dakika 45, Kinshansa masaa matatu, lakini ukitokea Arusha, Dar es Salaam ni mbali zaidi. Kwa sababu hakuna ndege inayotoka Mwanza kwenda huko kwenye nchi nilizozitaja hizi, naomba sana Waziri anapohitimisha mjadala huu atuambie ni lini uwanja wa ndege wa Mwanza sasa utakamilishwa kwa kiwango cha Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Busega, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi, barabara ya Dutwa-Ngasamo-Nyashimo ni kilometa 46, alisema itajengwa kwa kiwango cha lami. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, kwamba barabara hii sasa iwekwe kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais, aliahidi kwamba itajengwa kiwango cha lami na kwa sababu gani?
Mheshimiwa Spika, barabara ile ilikuwa barabara ya mkoa lakini ina-link barabara mbili za TANROAD. Kwa hiyo, ina maana kwamba inaelemewa na uzito wa mizigo ya magari yanayopita pale, kwa hiyo, automatically lazima ipandishwe hadhi iwekwe kwenye kiwango cha TANROADS, barabara kuu.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna kipande cha Mkula, pale Mkula ndiyo mzungumzaji anapotoka. Mheshimiwa Rais alitoa zawadi akasema kwamba kwa sababu barabara imepita pembeni na ule Mji wa Mkula ambapo anatoka mzungumzaji na wenyewe uwekwe lami, kilometa 1.45, alitoa ahadi hiyo. Naomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha aniambie kama ahadi hii ameshairekodi vilevile.
Mheshimiwa Spika, cha mwisho, ni namna ya kuboresha usafiri majini. Kweli wenzetu wa Mkoa wa Kagera, naomba nizungumze, ahadi ya meli imekuwepo kwa muda mrefu, lazima tufike mahali Serikali i-respond.
Haiwezekani tukarudia matukio kama mwaka1996 kwa sababu ya uchakavu wa meli. Leo hii MV Victoria imeshachakaa hakuna usafiri reliable kati ya Mwanza na mikoa jirani kama Mkoa wa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani wenzangu wa Kanda ya Mwanza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.