Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Rose Vicent Busiga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu, Mungu akubariki sana. Pia, ninakuombea sana, umekuwa mwema sana, umekuwa ukiendesha shughuli za Bunge kwa uaminifu mkubwa sana. Sisi kama Wabunge tunakuombea katika mchakato wa uchaguzi. Naweza nikasema neno moja, Wamtumainio Bwana ni kama mlima sayuni hawatatikisika milele na milele. Tuna imani kubwa na wewe na tuna mwamini Mwenyezi Mungu atakwenda kutuvusha katika mchakato huo wa uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unanijua vema mdogo wako, kwamba ukinipa nafasi siichezei. Nafasi hii adhimu ninamuomba Mwenyezi Mungu anisaidie niongee ukweli ulioko moyoni. Unanifahamu mdogo wako ni mkweli tupu. Ilikuwa ni juzi, wakati wa wiki ya nishati, nilipata bahati ya kutemebelea mabanda, nikaenda moja kwa moja kwenye mkoa wangu nikiwa na maswali mengi. Nilipofika kwenye mkoa wangu kuna vijana ambao wamepikwa walinipokea vizuri nikaanza kuuliza maswali ya umeme. Katika Mkoa wangu wa Geita nina takribani vijiji 474 lakini viiji vyenye umeme ni 389 na vijiji 85 viko kwenye mpango wa REA mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba ufikishaji wa umeme kwenye Mkoa wa Geita ni asilimia 82. Kwa hiyo ni asilimia 18 tu ambayo umeme haujafika. Nani kama Mheshimiwa Rais? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo inaendelea kufanya kazi kwa uaminifu hapa ndipo ninapokuja kusema kazi iendelee; na hapa ndipo ninapokuja kusema tena hakuna kilicho simama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si jambo dogo, naomba niwaambie Watanzania si jambo dogo. Nakupongeza sana kaka yangu Mheshimiwa January Makamba, hongera sana kwa kazi ambayo unaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mimi ninaona vyema, ni Dhahiri, pamoja na naibu wako na wizara nzima na Katibu Mkuu kwa jinsi ambavyo mmeweza kufanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Spika, lakini ninarudi kwenye vitongoji, kuna kupeleka umeme katika vitongoji vyetu. Mkoa wangu wa Geita nina takribani ya vitongoji 2,261. Kati ya vitongoji hivyo ambavyo vina umeme ni vitongoji 965, vitongoji 1,296 havijafikiwa na umeme. Kwa heshima hiyo hiyo Kaka yangu January nilipokuwa nimetembelea lile banda, nikafika, wakasema Mheshimiwa Mbunge tunapomaliza kupeleka kwenye vijiji tunashuka mpaka kwenye vitongoji. Ninakuamini kabisa Mheshimiwa January Makamba tunapoenda kumaliza hii bajeti ninaomba vitongoji vya Mkoa wa Geita vikafikiwe na umeme. Sina shaka na wewe, na ninaamini wewe ni mtu mwema sana, ni mtu bingwa sana, hivyo utaenda kufikisha katika vitongoji hivyo 1296 ili wananchi waone Serikali yao jinsi inavyochapa kazi.

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kiukweli niwadhihirishie Watanzania, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kwa nguvu zote. Ninaomba tumuamini Watanzania wenzangu. Kwa nini nasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu ladha ya chakula anaijua mpishi, mimi mwenyewe wakati nikiwa kwenye banda lile nilifika Rufiji nikiwa hapahapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu tu Kanuni za Bunge haziruhusu; lakini nilitama niwe humu humu Bungeni na wananchi wananiangalia waone ambavyo nimefika Rufiji. Mambo ambayo niliyoyaona, mafundi wako kazini wanaendeea na kazi, mambo ambayo niliyoyaona nilipofika pale Rufiji ujazo mkubwa wa maji unaendelea. Jamani Watanzania asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru. Mimi binafsi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ninamshukuru sana Kaka yangu Mheshimiwa January Makamba kwa sababu lile bwawa Mama alilipokea likiwa na asilimia takribani 30 leo tunazungumzia asilimia 88, nani kama Samia Suluhu Hassan?

Mheshimiwa Spika, tukienda mbele zaidi utaona upelekaji wa umeme kwenye migodi. Kaka yangu Mheshimiwa January unanisikia; kule kwetu Geita unajua kabisa sisi ni wachimbaji, ninakuomba kwenye migodi ambayo haijafikiwa na umeme kwa heshima hiyo hiyo kaka yangu ninaomba uweze kufikisha umeme kwenye migodi ya Nyakafuru, Mwabomba na migodi mingine ambayo sijaweze kuitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana sana sana kwa nafasi hii ambayo umenipa. Nina imani wananchi wangu wa Mkoa wa Geita hasa akina mama walionichagua, ninawaambia ya kwamba tuwe na imani kubwa na Serikali yetu. Serikali yetu iko kazini, Serikali yetu si ya mchezomchezo, na Mheshimiwa January Makamba kanifikisha Rufiji nikiwa hapa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninamshukuru sana na kumpongeza Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Geita pamoja timu yake nzima. Lakini kuna kaka mmoja ambaye sasa alikuwa ananipa hiyo elimu nilipotembelea, anaitwa Engineer Seif Abdul amenielewesha vizuri na ndio maana nimeweza kuchangia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja, hongera sana Waziri wangu January Makamba hongera nyingi Naibu Byabato.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)