Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia hotuba hii kwenye siku Tukufu, leo siku yetu ya Ijumaa. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye utalii na nikubaliane kabisa na Mheshimiwa Waziri alivyosema kwamba, Mheshimiwa Rais anastahili kuwa mhifadhi namba moja. Amefanya juhudi kubwa tumeziona katika kuhakikisha kwamba, nchi yetu inafunguka katika suala zima la utalii, pamoja na juhudi nyingine zote alizofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwenye nchi yetu, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili pamoja na timu yake nzima kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tumeona Mheshimiwa Rais amepambana sana kuifungua nchi yetu, kuhakikisha watalii wanaongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Hiyo ndiyo imesababisha kuongeza mapato yetu ya Serikali kwa sababu ya kuona kwamba watalii wetu wanaongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa maana ya Waziri pamoja na msaidizi wake, pamoja na Katibu Mkuu na Menejimenti yao nzima kwa sababu, inaonekana kabisa upele umepata mkunaji. Kwa kweli, wanafanya kazi kubwa sana kwenye suala zima la maliasili, mimi nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watalii tulionao sasa haijawahi kutokea toka tupate uhuru. Ni watalii wengi sana wameingia. Ndivyo hivyo tunavyoenda kupata mapato mengi sana ya Serikali. Mapato yameongezeka kwa kiwango kikubwa, tumemsikia Waziri na Mwenyekiti wa Kamati ameongea hapa, nawapongeza sana. Narudi kumpongeza Rais kwa kufungua nchi yetu kidemokrasia, kiuchumi, na sasa nchi yetu inaaminika kwa kiasi kikubwa. Hii ni kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimefurahi sana na kaulimbiu ya watu wa Maliasili inayosema Wakati ni Sasa. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona wakati anaongea watalii ni wengi, lakini tunajua kabisa vyumba vya hoteli ni vichache. Nawaomba, tumeambiwa Wakati ni Sasa, hii ni fursa, Waheshimiwa Wabunge twendeni tukakope tukajenge hoteli. Huu ni muda sasa wa kuwatangazia Watanzania, wananchi wetu, hizi ni fursa ambazo tunazitaka. Tukajenge hoteli, hoteli ya kitalii unaweza ukaweka tu chumba cha matofali ya kuchoma, ukaezeka manyasi na ukapata Dola 100, Dola 200 kwa siku. Kwa hiyo, hii ni fursa, tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kufanya kazi ya kuweka vivutio vikubwa na hatimaye kupata fursa ya Watanzania. Wakati ndiyo huu, nami nakubali Wakati ni Sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika na ndugu zangu Watanzania, wakati huu ndiyo wakati na sisi kufanya biashara zetu. Mama amefungua nchi. Kwenye nchi yenyewe ameleta maendeleo, lakini anataka na sisi Watanzania tupate maendeleo kupitia sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema kufikia 2025 tunatakiwa tuwe na watalii 5,000. Naamini sana Wizara hii chini ya Mheshimiwa Mchengerwa, kwa kazi kubwa anayoifanya, tunaamini 2025 tutakuwa na watalii zaidi ya 10,000, na hii itabaki kuwa ni sifa yetu Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende moja kwa kwenye suala la changamoto ya vijiji na hifadhi. Tumeona changamoto ni kubwa, wananchi wanalalamika sana kutokana na Sheria ya Ardhi na hifadhi kuingiliana. Niwaombe wataalamu wetu, kama alivyosema Mbunge aliyepita, mdogo wangu, Mheshimiwa Mnzava, mkae hizi taasisi zote kwa pamoja mziangalie sheria zenu upya mziweke vizuri ili kwenda kutoa malalamiko kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunamwona Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amekwenda Mbeya, lakini amekwenda Tarime kulikuwa na shida kubwa, amekaa tena na wale watu vizuri. Kuna watu walikuwa wamesusa wamerudi; Mheshimiwa Mchengerwa tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeangalia mimi mwenyewe kwenye YouTube ukiongea pale Tarime, Mbunge umeongea naye vizuri, Mwenyekiti wa Chama na wale watu waliorudi. Kwa kweli wewe uko kwenye Serikali kama Waziri lakini wewe kweli ni Mjumbe wa NEC, unaangalia Chama chako cha Mapinduzi; nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye mikakati yenu umetutajia mikakati 10, nakupongeza sana kwa mikakati yote hiyo 10 uliyoitaja, pamoja na ununuzi wa helikopta, kuongeza askari, lakini mmesema kuweka mazungumzo na wale watu waliopo kwenye changamoto, lakini kuwapa elimu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri asichoke, yeye hii ni Serikali yake, ni chama chake, asichoke na wataalamu wake kuwapa watu elimu kwa utaratibu, kuongea nao kwa heshima na unyenyekevu, wale ndio wapigakura wetu, lazima tuongee nao vizuri. Hatukatai kwamba wanafanya makosa, lakini waelimishwe kwa utaratibu.
SPIKA: Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninataka nimpe taarifa mchangiaji, ali-quote Ilani ya Chama Cha Mapinduzi akaonesha kwamba imeonesha kwamba kufikia 2025 watalii wawe 5,000. Ninataka tu niwambie asiache hiyo figure ikaenda hivyo, maana kasema 10,000; target ni milioni tano, kwa sababu sasa hivi tuko kwenye million plus, sasa akisema 5,000 inamaana unafupisha zaidi, unaturudisha nyuma zaidi. Kwa hiyo naomba tu arekebishe vizuri kwamba ni milioni tano na kuelekea kwenye milioni kumi, siyo watalii 5,000.
Mheshimiwa Spika, ni hiyo tu taarifa ndogo sana.
SPIKA: Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Esther ni mdogo wangu nimeipokea, kuwa anataka kuonekana tu. Naomba niendelee.
Mheshimiwa Spika, tunajua wazi kazi kubwa inayofanywa na Wizara na tunaendelea kuwapongeza sana. Lakini Mheshimiwa Mchengerwa umekuwa Waziri wa mfano, wewe ni mnyenyekevu na mchapakazi, wala huinui mabega yako juu, ukikuta missed call ya mtu hata uko busy jioni utampigia; tunakupongeza sana.
Mheshimiwa Spika, niongee kuhusu Tabora. Mheshimiwa Waziri naomba uandike na kalamu yako, Katibu Mkuu wewe umeoa Tabora, tena umeoa Ukoo wa Fundikira, tunaomba uandike haya ninayoyaongea. Tabora hakuna watalii hata kidogo ingawa tuna vivutio vingi. Cha kwanza, tuna Mbuga ya Ugalla lakini hakuna hoteli nzuri na wala hakuna barabara ya kutupeleka huko Ugalla, pia hakuna mawasiliano kwa maana ya simu. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo, lakini mtu-link na ofisi za tours za Arusha na wapi, watu watakapokuja waelekezwe maana ta Tabora, Ugalla n.k.
Mheshimiwa Spika, Tabora tuna Ngome ya Jeshi ya Mjerumani ambayo sasa hivi ni Ngome ya Jeshi. Kuna handaki inatoka chini kwenye ngome mpaka railway station, walikuwa wanakamwatwa watumwa wanapelekwa kupandishwa treni chini ya ardhi. Tunaamini huo utakuwa utalii mkubwa kama mkiamua kuutangaza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Waarabu walikuja pale kwa ajili ya kukamata watumwa wakajenga jengo kubwa ambalo alikuja kukaa David Livingstone, na walikuwa watumiwa kutoka Congo, Rwanda, Burundi na Kigoma, wanafikia pale Tabora ndipo wanasafirishwa kupelekwa Bagamoyo, Zanzibar na hatimaye Uarabuni; vyote hivyo ni vivvutio vikubwa sana ambavyo vipo katika Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, 1958 ulifanyika Mkutano Mkuu wa TANU pale Tabora na kujenga Mnara ulioandikwa Uamuzi wa Busara, ndipo palipotokea vuguvugu la kupata Uhuru mwaka 1961. Vuguvugu lile lilitokea Mkoa wa Tabora, tulipiga kura tatu, ya Muasia, ya Mzungu na Mwafrika, Mwafrika alishinda na Baba wa Taifa alihutubia mkutano ule kwa mara ya kwanza, alitoa machozi. Huo ni utalii mkubwa sana Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Spika, tunaomba muendelee kutangaza watu waje waone chimbuko lao la Uhuru wa Tanzania lilitokea wapi. Kuna mnara mkubwa ambao hautengenezwi sasa umebakia. Kuna jengo ulipofanyika Mkutano Mkuu wa TANU 1958 wa kuhakikisha msingi wetu wa kupata uhuru ulitokea pale; vyote hivyo ni vivutio.
Mheshimiwa Spika, tuna mtani wetu anaitwa Fundikira ambako Katibu Mkuu, Dkt. Abbasi ameoa. Pale opposite na nyumba yake kuna mlima, ule mlima kuna siku aliuziwa yule mzee. Sasa anakwenda kwenye ule mlima kwenye matambiko. Kila alipokuwa akikanyaga ardhi alama za nyayo za miguu yake zinabaki. Ni jambo kubwa sana la kufikirisha, unaweza ukafikiri alikuwa binadamu wa namna gani, lakini alikaa chini akapiga ngoma zake za matambiko, makalio yako pale na ile ngoma na fimbo vilitokea pale, havifutiki viko pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo yote hayo ni utalii mkubwa sana. Mimi namshangaa Dkt. Abbasi, tutakunyang’anya mke kwa sababu haututekelezei mambo yetu ya Tabora. Na hapa ni kwao kabisa na mke wake, kwa hiyo tunaomba sana hili ni jambo kubwa la utalii na litekelezwe.
Mheshimiwa Spika, nimesema kuhusu David Livingstone. Hilo jengo walilokuwa wanahifadhia watumwa lipo, wanapelekwa kwenye ngome ya Jeshi la Mjerumani ambayo sasa hivi ni ngome ya Jeshi, kuna njia ya chini kwa chini inakwenda inatokezea railway station, ndiko walikokuwa wanabebwa watumwa na kupelekwa humo. Hiyo njia kwa sasa naambiwa imeharibika; lakini mkiifuatilia ile njia ni kivutio kikubwa sana, Wajerumani wengi watakuja kuona jengo lao la utawala, ngome yao ya Jeshi na njia iliyokuwa ikibeba watumwa kupeleka huko.
Mheshimiwa Spika, kuna njia kuu ya watumwa waliokuwa wanapokelewa kutokea Burundi, Congo, wanapitishwa sehemu inaitwa Utusini. Ilikuwa wakipita wanapanda miembe, ndiyo maana mnaona Tabora kuna miembe mikubwa. Kuna Tabora Boys, alisoma Baba yetu wa Taifa, Mwalimu Nyerere, mpaka leo bweni lake lipo ukienda utaliona, na kitanda alichokuwa analala Mwalimu Nyerere kipo mpaka leo; ni utali mkubwa sana kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kuna Shule ya St. Mary’s, leo inaitwa Mihayo Sekondari, ndiyo alifanya kazi ya kufundisha akiwa mwalimu kwa mara ya kwanza pale. Wote huu ni utalii mkubwa ndani ya Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya yetu ya Kaliua kuna tatizo kubwa la Vijiji vya Usinge na Kakoko. Hivi vijiji vilipitiwa na mawaziri nane, wale mawaziri walisema wananchi wale waongezewe eneo kwa sababu kuna kaya 1,300; lakini kinachotokea sasa wanaambiwa wahame pale. Na nimesikia Mheshimiwa Waziri anasema yale yote yaliyosemwa na Kamati ya Mawaziri Nane yaendelee kuwa vilevile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya, ahsante sana, muda umekwisha, malizia sentensi.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)