Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa ubunifuu alioufanya kwenye Filamu yake ya Royal Tour. Na huo ni mfano mzuri, kwamba unapoandaa kitu kizuri lazima usemwe, lakini ukisemwa usikate tamaa ili mafanikio yaje yatokee badaye.

Mheshimiwa Spika, la pili, nikushukuru sana Mheshimiwa Mchengerwa, na ninakupongeza sana. Nimpongeze pia Rais kuwahamisha kama pair wewe pamoja na Dkt. Abbasi. Mimi kama mdau wa michezo nakumbuka kazi kubwa nzuri mliyoifanya kwenye Wizara ya Michezo. Mpaka leo tunaona Yanga inacheza fainali; hiyo ni kazi yako nzuri sana. naamini system uliyoondoka nayo kule tunakukumbuka mpaka leo. Sasa tunaomba na huku kwenye utalii uache alama ileile, na ninakuamini utafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, nitazungumza mambo machache. Mheshimiwa Waziri, kwanza katika kipindi ambacho Watanzania tunaoishi pembeni mwa hifadhi tulikuwa na bahati na raha ilikuwa ni kipindi cha mama huyu mwenye huruma, mama Samia. Alipounda timu ya Mawaziri Nane hakuwawekea mipaka, aliwaambia nendeni mkalete changamoto halafu mnishauri.

Mheshimiwa Spika, lakini mlichokwenda kukifanya kule kiukweli si sahihi. Na mimi nataka kujiuliza, hivi kweli ninyi mnaamini kwamba mtu mpaka anakwenda kukaa yale mazingira, ujue kumemshinda huku, hakununuliki. amekwenda kukaa pale kwa sababu ya shida zake. Mtu anayevumilia kukaa jirani na simba na tembo maana yake hana namna nyingine ya kufanya, na mwingine amekaa zaidi ya miaka 30. Ukienda leo na plan ya kumwondoa hii ni kutengeneza migogoro isiyoisha na Serikali. Na wewe Mheshimiwa Mchengerwa umekuta sisi Tanzania tuna timu za mwendawazimu lakini umetutengeneza mpaka tumekwenda fainali, achana na hayo mambo ya ku-create migogoro ya ujirani mwema.

Mheshimiwa Spika, siku moja nilimwona Mheshimiwa Waitara analia hapa na nikaona watu wanasema Mkurya ametudhalilisha; na mimi nina asili hiyo. Kwanza, ni kwa sababu humu labda viti vimefungwa na hizi mic, hasira ikikupanda Kikurya unachukua kitu chochote unasukuma mbele ili hasira yako ipumue. Kwa hiyo alipolia alilia kabisa akiwa anapumua ili hasira zake ziishe.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri, hebu utafute namna. Labda tulikosea, unajua tukikosea si vibaya kujikosoa. Hili Jeshi la Wanyamapori tangu tumelitengeneza hebu jaribu kuangalia kabla ya Jeshi Usu na sasa, migogoro iko wapi? Kwa sababu siamini huo utaalamu mnaoutumia kutengeneza hilo jeshi kweli mnawatuma kwenda kupiga watu? Mimi sielewi; mbona majeshi mengine hayako hivyo, yana taratibu zake? Yaani hawa imekuwa ni tatizo. Mnatengeneza Jeshi la kwenda kuwabaka dada zetu, kweli? Hii haiwezekani. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa usiponiambia mpango mkakati kama hili jeshi lilitengenezwa kimakosa utakuwa Waziri mzuri sana ukilifumua na kutengeneza jeshi jipya na la kisasa. Haiwezekani tukawa na watu wanapiga watu tu, kila siku kupiga watu; haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, mimi nakaa kwenye maeneo hayo yanayopakana na mapori ya hifadhi; ni tatizo. Ukitaka kujua njoo ukae, usije na magari, ukae siku moja tukuweke kwenye familia kama wiki halafu ufanye kosa kidogo uone utakavyopata mpite mpite. Kwa hiyo tukilalamika humu mtusikilize; nadhnai kuna makosa tumefanya kwenye uundaji wa Jeshi Usu. Lazima uje na mpango wa kulirekebisha, wale wabovu ondoa, baki na watu walio na nia ya kulinda maliasili, siyo kutengeneza migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kujiuliza; Maliasili mnatukamatia ng’ombe, sawa, tuna makosa, mnawapiga mnada, rundo la ng’ombe mnauza kwa bei mnazotaka wenyewe. Na nimejifunza, kwa sababu niliwahi kuongea – kuna Mawaziri sijui kama wako humu au wametoka – kwamba minada inakuwa kama dili, lakini mkifukuzwa tunaanza kusikia mnafuga ng’ombe. Kwa hiyo mnawafuata kiujanja ujanja, mnanunua ndani kwa ndani mnawafuga. Hizo ni laana! Na mtakufa vibaya, lazima niwaambie.

Mheshimiwa Spika, hebu jifikirie umenikamatia ng’ombe wangu 100, yaani naona wanakwenda sina uwezo wa kwenda polisi kwa sababu kuna bunduki. Haya, nina kosa, unawachukua ng’ombe wangu unawauza, mimi narudi maskini. Halafu baada ya miezi sita unaanza kunihudumia na hela ya TASAF. Hiyo ni akili ya design gani jamani? Kwani ni chanzo cha mapato?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, na makosa mengine tengenezeni utaratibu wa kutuonya. Unamkuta mtu ameingia mita 100, mita 200 ng’ombe wanachungwa au wanakunywa maji, unazoa ng’ombe wangu wote nirudi tu nyumbani nainze kusema maliasili; mtakufa vibaya. Lazima niwaloge; hiyo lazima tuambizane ukweli.

Mheshimiwa Spika, maana nikienda polisi utanishinda, mahakamani sina hela ya kwenda, mtalogwa mtakufa vibaya, lazima Mheshimiwa Waziri. Hebu rudisha moyo, tengeneza ujirani mwema ule wa maana. Kama huna maafisa mahusiano kwenye Jeshi Usu lako tafuta maafisa mahusiano watengeneze mahusiano. Mtatuchonganisha bure na Mawaziri, mara mkienda kule mnashika hasira mnasema na matusi, lazima. Kwa sababu sisi tunalia.

Mheshimiwa Spika, mimi ukinichukulia ng’ombe wangu ambao nategemea mtoto wangu wangu yuko chuo kikuu, mwingine anasoma sekondari. Haya, wamekwenda, ukienda kule kuna bunduki; nakaa tu kimya kweli? Na hii Serikali kweli tumekosa chanzo cha mapato mpaka chanzo cha mapato kiwe kuuza ng’ombe?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mchengerwa, hiki kitu jamani kwa kweli hakiwezekani. Fikirieni namna, makosa mengine muonye, mbona ninyi mnakosea na tembo akija huku hatuwashitaki, tunawaambia tu mambo yanaisha? Ninyi kosa lenu ni kuchukua tu na kupiga faini. Mheshimiwa Mchengerwa, mimi sitaki kuamini kama na wewe utaendelea kuwa Waziri wa mafaini; haiwezekani. Nikuombe uwe Waziri utakayetengeneza hifadhi tuzione kama mali zetu, siyo za Wizara.

Mheshimiwa Spika, sisi wote ni Watanzania, na mimi nilipongeze sana aliposimama ndugu yetu hapa wa Kiteto, tulimwambia, na ndugu yangu wa Monduli. Tulikuwa tunamshauri mpaka canteen, huyu hapa, kwamba kwa staili Serikali ilivyoamua kuwahamisha, yaani kutoa mpaka na gari ng’ombe wa Kimasai mara ya ya kwanza amepanda fuso, halafu unapiga kelele, nyumba, maji, shule. Tumemshauri sana Mheshimiwa humu, na akina Mheshimiwa Ole-Sendeka mpaka yakaisha.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka kuuliza; kule Nyatwali ni Tanzania, wale ni wananchi. Halafu mimi nataka kujiuliza Mheshimiwa Waziri ukipanda hapo uniambie ni hifadhi gani ambayo labda umekwenda kuangalia huko duniani, maana sisi tunatembea, nikishindwa kutembea na-google; kwamba unatoka mbugani unakatiza lami unakwenda moja kwa moja ziwani, pembeni kuna kijiji kinaitwa Lamadi, huku kuna Bunda. Kule ziwani sisi tunatega samaki, kule ziwani tunanywesha ng’ombe wetu, halafu na simba tukutane nao kulekule. Mna mpango gani ndugu zangu? Yaani mmefikiria kitu gani, au mtaweka fensi kuzia sasa simba wasiende?

Mheshimiwa Spika, mimi najuiliza mara mbilimbili, hizi ni research za design gani? Ndiyo maana wakati mwingine mimi najiuliza, siyo kwamba napingana sana na degrees za darasani, yaani matendo yenu huwa yananichanganya mpaka nafika mahli najiuliza mara mbili.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana jana nilikuwa nasikiliza kwenye nishati, watu wanasema tumnyang’anye TBS turudishe tena aliyekuwepo, wakati Bunge hilihili tulijadili, na ninyi ni wasomi, tukapitisha, TBS hatujampa uwezo, anategemea kukopakopa kama Musukuma hapa.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi najiuliza hiyo research kweli mnadhani itatufikisha? Kwani kimepungua nini; mmeambiwa kwamba wanyama wamebanana Serengeti mpaka mfukuze kile kijiji wale wanyama wawe wanakwenda? Je, kule kwenye ziwa ukikutana na wavuvi nani anawalinda? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule kwenye ziwa tukikutana sisi tunaonywesha ng’ombe wetu maji nani anawalinda? Wale wanyama miaka yote toka mbuga imeanza wanajua huku wanaishi binadamu, sasa mkiwaambia wapite mpaka kule huku pembeni Lamadi na huku Bunda, nani anaweka ulinzi? Mnataka kutuletea matatizo, na ninajua hamtafaulu.

Mheshimiwa Spika, hivi kweli mnataka ku-achieve kitu gani kufukuza wale wananchi halafu unamlipa mtu milioni mbili? Halafu walewale wanawaangalia Wamasai wamebebewa ng’ombe kwenye fuso; hapana bwana, hii keki ni yetu sote Mheshimiwa Mchengerwa. Maeneo mnayo mengi, kama mmepungukiwa, kama wanyama wamejaa beba leta hata Geita kule tuna mbuga haina wanyama. Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; mimi nina Hifadhi inaitwa Rubondo, ni kisiwa. Ile kata inahesabika kata ya Musukuma, kata ya Geita Vijijini, lakini langu kuu limewekwa Chato, sina tatizo. Sasa, historia ya ile hifadhi ni kwamba ina matambiko yetu ya Kizinza, mlango mkuu ulikuwa Nkome, na upo, na ofisi zipo, lakini yaliyopita si ndwele, turudishe lile geti la Nkome. Kama kule meli sisi bado tunahitaji tu kuwa na boti kwa sababu hata ukiingilia kule Mganza inabidi uje mpaka hifadhi, halafu halafu vile vivutio vyote viko karibu kabisa na jimbo langu. Kwa hiyo nikuombe, ile ni kata yangu. Mimi sitaki kufunga geti la Chato, lakini ninachotaka tuwe na geti la pili, ule utalii wa magari uanzie kwenye jimbo langu ili na sisi tuone Wazungu, siyo tuwe tuna-google tu ndiyo tunaona Wazungu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nina imani kwamba Mheshimiwa Mchengerwa utakapokuja hapa kikubwa kwangu, Nyatwali iwe sawa na…

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, Ahsante sana.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: … Loliondo; pili, utaratibu wa kulitengeneza Jeshi Usu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)