Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu yeye ndio ameitengenezea njia Wizara ya Maliasili na Utalii ikafanya vizuri sana kwenye suala la ukuaji wa utalii nchini kupitia the royal tour. Kwa maana ya filamu yetu ambayo imetangaza vyanzo vingi ambavyo tunavyo nchini na hifadhi zetu na baadaye tukafanya vizuri na kwa East Africa na ikiwezekana kwa Afrika nzima tukawa tunaongoza kwa idadi kubwa ya watalii ambao wamekuja kutokana na hii filamu ambayo Mheshimiwa Rais ameitengeneza. Kwa hiyo nipongeze sana hilo ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili niweze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mchengerwa ulikotoka umeacha miguu yako salama sana kwa sababu unafahamu na Wabunge wanafahamu na Watanzania wanafahamu kwamba kati ya Wizara ambazo zilikuwa kidogo tuseme ziko kwenye utulivu ilikuwa ni Wizara ya Michezo lakini ulivyopita wewe umeonesha kwamba Wizara ya michezo inaweza kuwa ni Wizara ambayo Watanzania wote wakajivunia lakini kelele zote zikawa zimeisha lakini pia business as usual ikawa imeondoka kwenye Wizara ya Michezo na hatimaye kila mmoja anakumbuka miguu uliyoikanyaga kwa Wizara ya Michezo. Wewe pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Abbas ambaye mnashirikiana kwa ukaribu sana. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya kwetu ni matarajio kwamba hata kwenye Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ambayo kwa kweli kwa historia Mawaziri wengi sana hawajadumu kwa muda mrefu kutokana na changamoto ambazo zipo kwenye Wizara hii lakini tunaamini wewe utakwenda kuwa mwarobaini kwa ajili ya kutusaidia kutatua changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, la kwanza nitazungumzia ongezeko la wageni. Ongezeko la wageni, tunaona kabisa takwimu zinaonesha kwamba tumetoka kwenye 1,700,000 na baadaye tumefika 3,800,000 kwa maana wageni wameongezeka kwa wingi sana. Mheshimiwa Waziri sasa ninaushauri kwenye jambo hili. Ushauri wangu wa kwanza tengeneza chain, mnyororo wa jinsi gani mgeni ameingia, amehudumiwa, amefika hifadhini, amelala, ametoka kwenye nchi yetu na in your record ujue mtalii huyu je, alirudi au hakurudi? Kwa sababu takwimu zinaonesha pia tuna changamoto ya watalii kutokurudi, sasa je, sababu ni nini? Mheshimiwa Waziri kwa hiyo, ninakuomba kwa sababu unataka kuifanya hii wizara iwe ni ya kiutofauti na watalii waongezeke zaidi naomba usaidie kujua chain. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimejifunza watu wanaokaa muda mrefu na watalii ni pamoja na madereva kwa maana kwenye tour guides wanajua mambo mengi sana ambayo watalii wanayazungumza. Usi-base sana kuzungumza na hawa ambao ni stakeholders wa sekta ya utalii kwa maana ya hawa wakubwa lakini nenda kwa hawa wa chini ambao ni madereva na hata tour guides wale wadogo, wapagazi pia. Jifunze watalii wanazungumnza nini kuhusu utalii wetu ndani ya nchi. Mheshimiwa Waziri kwa hiyo unaweza ukajifunza mambo mengi sana ambayo yanaweza kusaidia sekta yetu ya utalii kukua.

Mheshimiwa Spika, pia hifadhi za utalii zimekuwa ni zile zile kwa muda mrefu ambazo zinatamkwa. Mheshimiwa Rais kwa sasa amekuwa na mpango wa the hidden Tanzania, ni muda mwafaka sasa na nyie kwenda kuionesha dunia kwamba Tanzania kuna vivutio tofauti na hivi vya Serengeti na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, mojawapo ikiwa ni hifadhini kwetu Kitulo ambapo ni Jimbo la Wilaya ya Makete. Pale Kitulo ni moja kati ya hifadhi ya tofauti kabisa barani Afrika. Utofauti wake ni kwamba ni hifadhi ya maua ni bustani ya Mungu, ambayo Mheshimiwa Waziri nadhani mnaweza mkatumia pia hifadhi hii ikaweza kutusaidia na Mheshimiwa Rais ametupatia barabara ya lami ya kutoka Mbeya kwenda Makete, sasa hivi tunapita katikati ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muda mwafaka mradi wa re-grow unaweza ukaenda kuisaidia hifadhi ile ikakua na ikawa na manufaa kwa ajili ya wananchi wetu wa Jimbo la Makete lakini na Watanzania wenzetu wote. Mheshimiwa Waziri pia nikuombe kuongeza idadi ya wanayama, mlitupatia pundamilia, mmetupatia wanyama wengine swala. Tunaomba muongeze idadi ya wanyama kwenye hifadhi hii kwa ajili ya kuendelea kukuza hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwenye hili jambo pia la kukua kwa maana ya ongezeko la wageni. Nikuombe sana flow imekuwa ni kubwa sana ya wageni kwenye Taifa letu. Jambo ambalo tumepata changamoto ni malazi. Tulienda Karatu na unakumbuka tulivyokuwa kule, tumeona flow ya watalii ni kubwa na vyumba vya malazi vimeisha kabisa. Sasa sekta za kibenki zimelekea sana kwenye sekta ya kilimo na sekta nyingine. Ni muda mwafaka sasa wa kukaka katikati na benki ukazungumza nazo ikiwemo benki ambayo Serikali ina hisa nyingi Azania Benki ikaweza kusaidia na ikaweza kutangaza fursa za watanzania kukopa na kujenga na kuwekeza kwenye sekta ya utalii ili utalii wetu uweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni jambo la reforms. Mheshimiwa Waziri lazima ufanye reforms. Hili niseme kwa sekta yako ya utalii hatuwezi kuendelea na business as usual kwenye suala la uendeshaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Watakukasirikia, watakuchukia, watafanya kila kitu lakini ni lazima ufanye reforms. Reforms ya kwanza ni namna jinsi gani tunaweza kuutangaza utalii wetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ukumbuke kwamba sisi tuko kwenye namba moja Barani Afrika kati ya Taifa lenye vivutio vya asili. Tanzania tunaongoza Barani Afrika, sasa haiwezekani kwenye mataifa madogo kuliko Tanzania yanafanya vizuri kwenye sekta ya utalii tena wana kivutio kimoja tu yawezekana ni Nyani lakini sisi tuna vivutio vingi tumeshindwa kufanya vizuri kwenye utangazaji wa utalii wetu.

Mheshimiwa Spika, sasa niombe kupitia bodi ya utalii Tanzania nina Imani kubwa sana Mkurugenzi wa Bodi ukimsikiliza mawazo yake ni makubwa sana muweze kwenda kutangaza utalii zaidi kuliko hapa ambapo Mheshimiwa Rais ametangaza.

Mheshimiwa Spika, nimeona una mpango wa kutangaza kupitia kwenye timu za mipira kwa maana kwenye michezo mbalimbali. Sasa Mheshimiwa Waziri tusirudi kwenye mkenge ule ule. Wakati ule tulitangaza utalii wetu kupitia Sunderland ikaenda ikazama, ikazama na utalii wetu. Ni muda mwafaka sasa kwenda kutafuta timu ambayo ina consistency nzuri kwenye performance ambazo zitaenda kutufanya tusikike na tufanye vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sababu nina records nimekuwa ni mdau wa michezo na wewe umekuwa mwanasheria kwenye mpira wetu Tanzania. Unajua kabisa timu inayofanya vizuri na watu wanaongezeka kwenye kui-support na inapofanya vibaya watu wanatoweka. Mnavyoenda kutafuta hizi timu kama mnatafuta ni Manchester, kama ni Real Madrid kama ni PSG ni nini, ninaomba Mheshimiwa Waziri usiingie mkenge wa kutafuta timu ndogo ndogo zikazama na utalii wetu. kwa sababu gani? Mheshimiwa Waziri nimejifunza hilo sana kupitia Sunderland ambavyo jinsi iliweza kutoweka.

Mheshimiwa Spika, pili Mheshimiwa Waziri lazima kwenye kuongeza Watalii tuwe na neno moja la kuitangaza Taifa letu. Tutambulike kwa neno moja leo hii ukienda huyu anasema visit Tanzania, ukitoka hivi anasema Tanzania ni forgettable sijui mwingine anaenda hivi. Lazima tuwe na slogan moja ya kufanya utalii wetu utambulike kwa namna moja kwenye Taifa letu. Kwa hiyo, reforms zingine utaendelea kuzifanya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la Ngorongoro. Tumehamisha watanzania wenzetu pale wameelekea kule Handeni kwa maana ya kupisha uotoasili wa Ngorongoro. Mheshimiwa Waziri lile jambo lazima mchakato uende haraka sana. Kumbuka kwamba maadui zetu na marafiki zetu wa karibu hawatutakii mema kuona sisi tunafanya hili jambo. Tulijitanabaisha, tulijionesha kwamba tuna uwezo wa kufanya hilo jambo na tumeweza kwa kiwango kikubwa na nipongeze Mheshimiwa Rais lakini kuendelea ku-delay wale watu unaweza kuona wanaanza kurudi sasa. Wanarudi kwa njia tofauti, tofauti kupitia makongamano kuhamasisha vitu kama hivi. Acha huu mchakato tuumalize kwa haraka andika historia Mheshimiwa Waziri kwamba uikamilishe hii safari kwa haraka ili wananchi wetu wa Ngorongoro wapate eneo salama na mchakato wa Ngorongoro uishe. Majirani wanatumia hawa watu kutugombanisha, majirani wanatumia hawa watu kuhakikisha kwamba utalii haukui, majirani wanatumia hawa watu kuhakikisha kwamba tunakwama. Kwa hiyo, mchakato wa Ngorongoro uweze kukamilika vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo langu lingine ni kwenye suala la migogoro. Kwanza nikupongeze umeshaanza ziara ya kuzunguka kwenye Mikoa tofauti tofauti. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana changamoto ya Mawaziri nane ambao walikuwa wanazunguka, lazima tukubali changamoto ilikuwepo. Mara nyingi walikuwa wanafika muda mwingine Mkoani hawafiki kwenye kiini kabisa cha migogoro kule chini.

Mheshimiwa Waziri sasa tumia fursa hiyo, nikuombe sana nenda kwenye maeneo yale kwa sababu migogoro yetu mingi Tanzania ni kwa sababu ya kukosa ushirikishwaji. Ukiwasikiliza wale wananchi ambao walikuwa wanakupongeza juzi kwamba toka waisikie Serikali wewe ndio Waziri wa kwanza umegusa kufika kule Serengeti na ukawasikiliza. Lile jambo sisi kama Wabunge tunajifunza kumbe wananchi wako tayari kupokea maelekezo ya Serikali lakini changamoto ni kwamba Serikali haiwafikii wanafika pale wanawamrisha wananchi, hawawashirikishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokuwashirikisha wananchi ndio kunasababisha migogoro mikubwa zaidi. Ni vema mkafika pale mkakutana na wazee wa eneo lile, mkakutana na wenyeviti wa vijiji wa eneo lile kwenye maeneo tofauti. Mheshimiwa Waziri na utakapokuja hapa nikuombe utupe umeainisha migogoro mingapi mikubwa nchini ambayo unampango mkakati nayo ya kwenda kuitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukuteua kitendo cha kufika kule Serengeti kimetupa majibu ya kwamba sehemu kubwa ya viongozi hawafiki chini kwenye migogoro. Wananchi hawana changamoto kabisa, kwa mfano kule Makete sasa hivi tumeanza tena migogoro na hifadhi ya TANAPA kwa sababu wananchi hawakushirikishwa. Mheshimiwa Waziri kwa hiyo, nikuombe sana, nakupongeza kwa sababu umenisaidia kumaliza migogoro kwenye Mpanga, Kipengele na wananchi wa Makete nawashukuru sana watu wa Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro kati ya TANAPA-Kituro na wananchi wangu wa vijiji vya Makwaranga, Isapurano na maeneo ya Igenge maeneo mengine kama Makwaranga, maeneo kama Kigara yanatokana kwa sababu TANAPA wakifika wanachomeka bikoni wanaondoka. Huu sio utaratibu mzuri. Taifa letu halina shida sana, migogoro inatengenezwa na sisi viongozi. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kusema hayo niseme jambo moja tu kwamba ninamtakia kila lakheri Mheshimiwa Waziri ulifanya vizuri kwenye Wizara uliyopita ya Michezo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imegonga.

MHE.FESTO R. SANGA: Naam.

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana, nimtakie kila lakheri Mheshimiwa Waziri. Wewe ndio Ronaldo wetu, Messi wetu tumekuachia mchezo huu cheza sana. Ahsante sana. (Makofi)