Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Francis Leonard Mtega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayofanya kwa watanzania wote hasa hasa ile ziara ya Royal Tour kwa kweli imeleta watalii wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka tulifika Arusha, Mkuu wa Mkoa alikiri kwamba changamoto kubwa sasa ni namna ya ku-manage magari yanavyomiminika kule Ngorongoro. Ukizingatia kwamba tulitoka kwenye Covid-19 basi hayo yalikuwa mafanikio ya hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa shukrani za dhati kwa viongozi wakuu, Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Phillip Mpango, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri wanazofanya lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Nimpongeze Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja. Niwapongeze watendaji wakuu wa Wizara Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, watendaji wote na wafanyakazi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya kuhifadhi, kulinda uhifadhi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kutatua migogoro baina ya TANAPA na wakulima, TANAPA na wafugaji lakini wanyama dhidi ya wananchi. Kabla sijaanza mchango wangu nina salamu za pekee kutoka kwa wana Mbarali kwa Mheshimiwa Rais. Wanamshukuru sana kwa uamuzi wake thabiti wa kumaliza mgogoro wa DN Na. 28. Ni mgogoro uliodumu kwa miaka mingi sana, umesumbua sana wananchi wa Mbarali wamesita kuendeleza kuwekeza kwenye maeno yenye mgogoro hivyo kurudisha nyuma maendeleo yao, lakini Serikali ya Awamu ya Sita wanakwenda kuumaliza kabisa wanasema ahsante sana mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jumla ya vijiji 29 vinaenda kurudishwa kwa wananchi ambalo ni eneo lenye ukubwa wa hekta 74,000 kwa hiyo wananchi wa Mbarali kwa kweli wanashukuru sana kupewa eneo hili. Pia wanashukuru kwa uthamini unaoenda kufanywa kwa vijiji vitano tuna baadhi ya vitongoji ambavyo vitabakia kwenye hifadhi na process nzima inavyoendelea na wanafurahi kwamba watalipwa fidia na kuoneshwa maeneo mengine ambayo watayatumia kwa kilimo na ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo sasa nianze mchango wangu kwa kumsihi Mheshimiwa Waziri kwamba namwamini sana. Kama walivyosema wenzangu ameonesha maajabu makubwa kwenye Wizara ya Michezo tuko juu sana. Pia ameenda Serengeti kule ametatua vizuri mgogoro na mimi namwomba tuongozane Mbarali ili akajionee mwenyewe vizuri tushirikiane kutatua migogoro ya Mbarali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa kwanza unasababishwa na vijana wale walioaminiwa kwenda kufanya doria kwenye mipaka na uhifadhi. Badala ya kufanya kazi waliyotumwa wanaenda kuingia kwenye maeneo ya wananchi na kufanya vitendo visivyokubalika. Wengi wao wanaswaga mifugo na kuiingiza hifadhini, sasa hii inachochewa na taratibu au Sheria iliyowekwa ya kutaifisha mifugo ya wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri hebu angalia utaratibu huu vizuri kama unatija kweli kwa sababu inawezekana wale ambao sio waadilifu wanatumia mwanya huu kupora mifugo makusudi pengine wajinufaishe wao wenyewe badala ya kuingiza fedha Serikalini. Hivyo nakuomba sana tuongozane ukachunguze mwenyewe nikuoneshe wahusika walifanyiwa vitendo vile. Muda ule ambao ulivyokuwa mfupi ikauzwa haraka haraka wanunuzi wenyewe kwa kweli inatia shaka nakuomba tuongozane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa pili, vijana wale huwa wanakuja mitaani na kufanya vitu ambavyo havistahili, kupiga watu kwa tuhuma ndogo ndogo ambazo hazina uhakika. Wakiona mtu amebeba kuni barabarani wanamkamata wanampiga eti umetoa hifadhini kitu ambacho sio kweli lakini pia huwa wanaweza wakafika wakaizuia mifugo sehemu na kuiingiza mashambani wanasimamia ili ile mpunga wa watu kitu ambacho kwa kweli kinatia huzuni sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kwa hiyo, nakuamini sana, ni mchapakazi, ni hodari, ni mbunifu twende Mbarali ukatatue hii migogoro naamini itaisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimefurahi sana kuona kwamba kuna azimio linaletwa Bungeni la kuridhia mipaka mipya baina ya Hifadhi ya Ruaha na wananchi wa Mbarali kwa kweli ni jambo la kheri. Tunaamini ikifikia hatua hii migogoro yote itakua imeisha Mbarali sasa tutalala na usingizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha niombe kwamba baada ya kufika Mbarali baada ya kujiridhisha mwenyewe, niko tayari kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwako na kwa Serikali yangu yote. Nipo tayari kujitolea kutetea, kulinda maslahi ya Serikali lakini pia maslahi ya wananchi wa Mbarali kama walivyonituma mwakilishi wao. Nikizingatia kiapo cha uaminifu na kiapo cha kulinda na kutetea Katiba ya Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru Mheshimiwa Waziri na timu yako yote nina Imani kubwa sasa na wewe kwamba tutaenda Mbarali. Tutaenda kumaliza migogoro yote ya wana Mbarali.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)