Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuitangaza nchi yetu katika eneo hili la utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alifanya vizuri sana kwenye michezo, lakini kwa historia ya zile Wizara tano ngumu (mifupa migumu) ni pamoja na Maliasili na Utalii. Sisi tunakutakia kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nianze na janga la moto kwenye Mlima Kilimanjaro ambalo linatokea mara kwa mara. Kwanza, sasa niwape Wizara habari njema kwamba Mheshimiwa Rais ameleta fedha za kukarabati Uwanja wa Ndege wa Moshi, kazi inaendelea, utakuwa ni uwanja wa Kisasa. Sasa ni jukumu lenu kuona ni namna gani mnaweza kuweka huduma za zimamoto kwa kutumia ndege mkishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kupambana na janga lile la moto linapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri pia mfanye juhudi ya kujua ni nini huwa kinasababisha na ni namna gani mnaweza kuwa mnazuia moto huo kutokea mara kwa mara? Ni muhimu sana mfanye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii unahitaji investment na ukiangalia nchi kumi bora ambazo zinafanya vizuri sana kwenye utalii, sisi tuko hapo katikati. Ukiangalia gap kati ya nchi ya kwanza inayoongoza kwa watalii wengi ambayo ni Egypt, ukija ya pili ni Morocco ,halafu South Africa na Tunisia ambazo mapato yake yanaanzia dola milioni 13 mpaka Nane hapo kwa Tunisia. Uwekezaji wao kwenye tourism ni mkubwa sana. Tunahitaji katika miaka hii ya Bunge hili Mheshimiwa Waziri uje na mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna mchangiaji asubuhi alisema kuweka matangazo kwenye timu za mpira. Mimi nadhani wakati mwingine siyo lazima tu-copy kila kitu. Kwa mfano, hapa nchini nafikiri kuna tangazo ukiliweka kwenye jezi ya Yanga unapoteza hata baadhi ya washabiki wa Simba. Tutafute njia ambayo ni inclusive itakayoleta watu wengi kwenye matangazo yetu ambayo tutafanya. Siyo lazima kwenye timu za mpira kwa maana ya jezi lakini angalau uwanjani ili tuvute watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji hauishii kwenye kutangaza. Hapo kwenye kutangaza nitakuja na mawazo mbadala hapo baadaye. Kuna suala la miundombinu, hili sisi tunafeli sana. Barabara ya kutoka Ngorongoro kwenda Serengeti kupitia geti la Nabi, barabara ile hata kama mzungu amekuja hapa kwa ajili ya adventure, pale utakwenda kumvunjavunja, magari yanaumia na fedha hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna project ya kuweka lami kwenye ile barabara ilisimamishwa kipindi cha nyuma, siamini Wazungu wanakuja ili waishi kwenye maisha ya barabara ngumu ya kutingishika na kuumiza magari kama ile ya kutoka Ngorongoro kwenda Serengeti. Hebu liangalieni upya kwa sasa. Wakati mwingine siyo lazima msikilize watu. Hata watu waliosema tusijenge bwawa letu hili walisema ni kwa sababu za kimazingira, lakini hatuwezi kufa kwa njaa kwa sababu eti tunasubiri mbunga ambayo ni world heritage.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ile barabara tuangalie, tunaweza kuitengeneza vizuri hata kama siyo kwa lami, bali kwa teknolojia nyingine ambayo haitaleta shida na usumbufu mkubwa. Kwa barabara ilivyo ni hasara kwa magari na kwa wageni wale wanaokwenda pale. Kwa hiyo, kwenye miundombinu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye Mlima Kilimanjaro miundombinu ni pamoja na zile camp. Camp zile ziboreshwe bila kuharibu mazingira, ziwe na mazingira mazuri. Siyo lazima mtu akipanda mlima basi vyoo anavyotumia vionekane ni vyoo vya hali hafifu, hapana. Tuboreshe mazingira ya Mlima Kilimanjaro kwenye zile camp na tuhakikishe kwamba tunapata wateja wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miundombinu mliongelea suala la vitanda kwenye presentation yenu kwenye semina. Mheshimiwa Waziri, mimi nina ushahidi. Kuna baadhi ya watu wanataka kuwekeza kule kwenye mbuga, kuweka hivyo vitanda tena vya gharama kubwa, lakini kuna baadhi ya makampuni yameshika maeneo miaka mitatu, minne kwa ajili ya kuwekeza na hawajawekeza na hayo maeneo ni potential. Kwa nini msiwafutie hao walioshikilia hata kama ni matajiri ili tuwape hao wawekezaji ambao wapo tayari kuwekeza hata sasa hivi? Hata ukinifuata, nitakuonesha baadhi ya maeneo na hao watu ambao wako tayari. Wenzetu wanakuja mpaka na coordinates. Ukiuliza unaambiwa hili ni la mwekezaji fulani, miaka mitano hajawekeza. Basi tuangalie namna ya kuwekeza hivyo vitanda ili tuwe na vitanda vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye hoteli, ni moja ya kitu kinachosababisha tuwe hatuna wageni wengi. Ninatoa tu mfano wa jumla, ule mkutano wa wanashheria ule wa (TLS) unafanyika kwenye miji michache sana Tanzania kwa sababu gani? Haufanyiki Dar es Salaam kwa sababu wengi wanaishi pale, unafanyioka Arusha kwa sababu kuna vitanda vingi na accommodation ya kutosha. Wakija hapa Dodoma, tayari tuna ukumbi mzuri wa ku-accommodate watu 2000, 3000 lakini watalala wapi kwa hapa Dodoma? Kwa hiyo, suala la hoteli ni muhimu sana katika uwekezaji au ukuzaji wa utalii kama sehemu ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nafikiri Serikali yetu inatakiwa iwe na macho na maamuzi ambayo yamekwenda mbele zaidi. Kwa mfano, kuna hoteli ile ya Ngurdoto Mountain Lodge ambao ni uwekezaji mkubwa wa mzawa, bahati mbaya ameondoka, biashara imekwenda vibaya, Serikali imeacha pale, ajira za watu zimekufa, eneo lile limekufa. Kwa nini Serikali isi-intervene kwa kununua share au kuingia makubaliano na wawekezaji ili tuwekeze eneo kama lile na tuwe na maeneo haya ya utalii ambayo tunayahitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwenye miundombinu kuna kazi kubwa sana ya kufanya na siyo lazima wafanye Serikali. Wanaweza kuweka mpango mzuri na wa kuwavutia wawekezaji wakawekeza kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la gharama. Moja ya matatizo ambayo yanaukumba utalii wa Tanzania ni kwamba watalii wanasema destination yetu imekuwa ni ghali sana. Mimi najua moja ya maeneo yenye gharama kubwa ni pamoja na landing fees za viwanja vyetu vya ndege. Hebu tuangalie namna ya ku-harmonize. Tunaweza tukatoa hata holiday ya miaka kadhaa, tukaangalia namna ya kupata hayo mapato kupitia sehemu nyingine ili utalii uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye gharama hizi ni pamoja na mikopo. Wakati ule tumepayta janga la UVIKO niliwahi kutoa wazo, nikasema ni vizuri Serikali iongee na mabenki kwa watu wa utalii iwe kama wakulima, wanakopeshwa lakini wanalipa kwa wakati, kwenye kipindi cha high season. Kipindi cha low season, zile interest na principle zisimamishwe ili waweze kujiweka sawa na season inapoanza waende. Kama wakulima wanavyokopeshwa kwamba kipindi cha mavuno kinajulikana ndipo wanaanza kulipa mikopo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuwapunguzia gharama wawekezaji, maana yake tutaweza kuwasaidia sasa nao wawaajiri wale wafanyakazi wadogo kwa muda mrefu na tukakuza ajira kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilishaliongelea mara mbili tatu ni suala la park fees. Haiwezekani tukawa na park fees ambazo ni uniform tu. Mbunga ambazo zinafanya vizuri, hazina tofauti kubwa na mbuga ambzo hazina watu kabisa. Sasa ni nini tutatoa incentives kwa watu kupeleka watalii kwenye mbunga hizi ambazo hazifanyi vizuri? Tuangalie, kuwe na tofauti kubwa kiasi kwamba mtu ataona nita-save ili aende kwenye mbuga hizi ambazo hazifanyi vizuri. Kwa hiyo, nafikiri hayo ni maeneo ambayo tunaweza tukawekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, manpower ni tatizo kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania. Mtu yeyote anaweza akaenda kwenye hoteli zilizopo Zanzibar; asilimia kubwa ya wale wafanyakazi active Zanzibar na porini, ni wale wanaotoka nje kwa nchi jirani. Waswahili unakuja kuwakuta huku chini kwenye kazi ambazo hawa-interact na wageni. Kwa nini tusiwekeze? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, VETA, kwa kweli kwenye kuwaandaa wafanyakazi wa utalii hawafanyi vizuri. Tena kuna mtu aliniambia, Tanzania ndiyo nchi pekee unakuta mpaka mfanyakazi wa ndege ana-attitude, yaani hawezi kukuchekea hata kama ana stress zake. Sasa industry hii inahitaji watu kwanza manpower iende kwenye lugha, wapishi wazuri na hata supporting staff. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Airport zetu na entry point, kwa mfano mtu wa immigration ni vizuri achaguliwe yule mtu ambaye anaweza kuongea lugha vizuri, anawasiliana kwa ukarimu na yuko sharp. Hivyo hivyo, ukienda TRA kwenye entry points kwa maana ya Airport na baadhi ya zile border ambazo zinapitisha watalii. Sasa ukifika kwenye hizi border zetu, watu wenyewe waliopo wana attitude tayari hata kabla hujaingia, hawakaribishi watu vizuri, hawaongei vizuri, lugha inawagonga. Hapo hatujaenda kwa ma-guide, wapishi na hata wahudumu wa hoteli. Kwa hiyo, kwenye manpower ni lazima tuwe na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha tunakuwa na manpower ambayo inaweza ika-support ukuaji wa utalii. Baadhi ya maeneo watu wanakwenda kwa sababu ya manpower tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo mambo ambayo nafikiri yanaweza kusaidia kukuza utalii. Kwenye presentation ya Wizara walisema tuna-deal tu na maliasili, tumeacha uwekezaji. Ni kweli, kwa sababu baadhi ya uwekezaji unahitaji hela, na kama siyo nguvu ya wwekezaji wenyewe, basi Serikali i-intervene. Kuna vitu havihitaji nguvu, vinahitaji advocacy. Kwa mfano, nikimwuliza mtu yeyote hapa ni kwa nini ile cable car ilisimamishwa na nini implication za kusimamishwa na ni namna gani tunaweza kuwa na kitu mbadala pale kwenye Mlima Kilimanjaro ambacho haki-intervene lakini kinaongeza mapato? Hakuna. Hata hivyo, watu wamezuia cable car na wanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo tunaweza kuewekeza. Michezo ya golf, kuna game ilikuwa ifanyike kule Kili Golf, uendeshaji wa baiskeli kama Toure Kilimanjaro tuka-boost kama ilivyo Kilimanjaro Marathon…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)