Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa pili jioni ya leo katika Wizara hii ambayo nina maslahi nayo moja kwa moja. Kwanza, na-declare interest, hii ni Wizara yangu kwa maana nimefanya kazi kwa zaidi ya miaka 11. Nimefundishwa kazi na kulelewa na Wizara hii ambayo ninaipenda sana. Sasa nina machache ya kumshauri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni mgeni, sasa nichukue fursa hii kumshauri. Sina mengi ya kusema, labda mengine tutazungumza wakati mwingine, lakini leo nimshauri tu. Aidha, Bunge la Septemba, Novemba na yanayofuata kama tutaona tunayoshauri hayajafanyiwa kazi, basi tutaona namna ya kuzungumza, lakini kwa sasa nimshauri, sina cha kumlaumu na nimhakikishie leo sitashika Shilingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpitishe kwa mambo machache ambayo yako pending kwenye Wizara yake ambayo yanahusiana na maeneo yetu ya kijimbo na wananchi wetu. Kwanza, kwangu Malinyi na Bonde la Kilombero wanafahamu kuhusu Kijiji chetu cha Ngombo, ilizungungumzwa na Tume ya Mawaziri wanane kwamba Kijiji kile kifutwe kwa sababu ya sensitivity ya uhifadhi na kadhalika, jambo ambalo tulimalizana nao kwenye mkutano wa wananchi, lakini kilichofuata ni kwamba wananchi wanatakiwa wapewe fidia ili waweze kuhama pale Ngombo na kutafuta maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili ni la muda mrefu tangu mwaka 2022, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea au hakuna ambacho Mbunge ana taarifa nacho. Sasa hofu ni kwamba mwezi wa Kumi na Kumi na Moja watu wanaandaa mashamba kulima, watu wa Ngomnbo sijui watalima wapi? Nasema hivi kwa sababu wanapaswa walime wapate chakula, ila wakilima watagombana na watu wa maliasili kwamba wamelima hifadhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini wasitoke mapema wapewe hela yao kama ambavyo tumekubaliana? Sasa muda ukifika tutaanza tena kugombana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili alifanyie kazi haraka. Ilikuwa ni jambo gumu kufikia hatua hii, lakini muda umefika, naomba liishe mapema ili watu wasije wakaonekana ni wakorofi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kulikuwa na biashara ya viumbe pori hai, wale wanyama na wadudu wadogo wanaosafirishwa kwenda nje ya nchi wanafanya watu wa TWEA, ilisimamishwa karibia mwaka 2016 leo miaka mitano au sita. Nilizungumza hapa Bungeni kipindi fulani, Serikali waliahidi watafanyia kazi, lakini juzi nimesikia hapa Mheshimiwa Waziri anatoa maelekezo kwamba huenda jambo hili likaruhusiwa na biashara ika-resume. Ni jambo la heri kabisa na ninawatakia heri na ninatamani kuona hilo linafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la upandishaji hadhi pori la akiba la Kilombero (Kilombero Game Controlled Area) kuwa game reserve. Nimeona imefanyika na GN inatembea mitandaoni kwenye ma-group ya WhatsApp kwamba eneo hili limeshapandishwa hadhi sasa linakuwa ni game reserve na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina tatizo kidogo na hilo kwa maana sina shida na upandishaji hadhi wa maeneo, ndiyo umuhimu wa uhifadhi kulingana na sensitivity yake, lakini procedure yake sina amani nayo sana. Sasa nimesema nisizungumze sana ili tusigombane, Mheshimiwa Waziri ni mgeni. Nadhani wanafahamu kuna utaratibu wanapaswa kushirikisha wananchi tuweze kujadili mambo haya yaweze kwenda vizuri na mwisho wa siku tujue tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo ya Kijiji yanaingia kwenye eneo hilo amablo linatajwa, kuna baadhi ya maeneo ya wananchi wa kawaida yanaingia mle. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili alifanyie kazi au tutazungumza na nitapata mrejesho kutoka ofisini kwenu. Tusijadili sana hapa kwa sababu nina vitu vingine vya kuvisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna suala la wanyama vamizi, (wanyamapori wasumbufu). Kule kwangu Malinyi tuna National Park ya Nyerere, bado kuna Selous na kadhalika. Tembo wamekuwa wakisumbua sana kama ambavyo wanafanya sehemu kubwa ya nchi, lakini bado usaidizi haupo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nimetoa hizi highlights uzichukue. Hata hivyo, bajeti ya mwaka 2022 niliahidiwa hapa kwamba Malinyi itakuwa moja kati ya wilaya kadhaa ambazo zitapata vituo vya kudumu vya Askari wa Wanayamapori. Nadhani TANAPA na TAWA wali-share, sasa natarajia kuona pengine wakati wa kuhitimisha utasema hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nianze kuchangia. Nilikuwa nampitisha tu Waziri nina mambo makubwa mawili ya wizara hii. Kwanza, napenda nimshauri Waziri, natamani abadilishe thinking au approach ya conservation ya nchi hii. Pili, kwenye Jeshi letu la uhifadhi kwa maana ya Conservation Paramilitary, namna muundo wake ulivyokaa kidogo haujashiba na kidogo haujatosheleza. Kwa hiyo, haya ndiyo mambo makubwa mawili ambayo nilisema nataka nianze kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye approach ya uhifadhi ninaozungumzia, mara zote nimekuwa nawaambia wenzangu jambo la ushirikishwaji ndiyo kila kitu kwenye uhifadhi, na ninadhani dunia nzima ndivyo inavyotakiwa kuwa. Wizara yangu ambayo ninaipenda, we have been too militarily, kila jambo ni vurugu, kugombana, hata migogoro mingi ambayo inaendelea kila Mbunge akisimama hapa anazungumzia migogoro ni kwa sababu ya kutoshirikisha wananchi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kushirikisha kwa namna gani? Wananchi, wenzao ni wawakilishi watu wa kuchaguliwa kwa maana ya Mbunge na Waheshimiwa Madiwani kwenye maeneo yetu. Watu wa Serikali na hata ile Tume ya Mawaziri wanane, ukiwauliza wanasema, tumefanya ushirikishaji nchi nzima. Ushirikishaji wenyewe, wanaenda mikoani kuzungumza na Mkuu wa Mkoa, wanaenda Wilayani kuzungumza na DC, Wakurugenzi na vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi kiutaratibu unajua jeshini kiongozi huwezi ukawa unashauriana na watu wa ulinzi, kwa maana ya Polisi, wanajeshi wa kawaida hawa, watu wa uhifadhi ni maelekezo, “ndiyo Afande, jambo limekwisha.” Sasa unakuta Serikali inajadiliana yenyewe. Kwa hiyo, Serikali inatoka Wizarani wanakwenda kujadiliana mkoani ambayo ni Serikali tena. Wanashuka chini wanakwenda wilayani, wanazungumza na DC ambayo Serikali tena na watu wa kuchaguliwa kwa maana ya Wabunge na Madiwani ushirishwaji siyo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nawashauri wenzangu, ili isionekane sisi ni wakorofi, hakuna mtu ambaye anataka mambo yaharibike au uhifadhi uharibike. Sisi Malinyi na Bonde la Kilombero Samaki ilikuwa unaokota bure kama takataka, tunakula hivyo, lakini leo samaki ni gharama kubwa Malinyi, Ulanga na Kilombero kuliko hata Dar es Salaam. Maeneo ni kweli yameharibika na kadhalika ni changamoto kubwa. Hakuna anayependa kuona uhifadhi unakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa nimesimama hapa kueleza, mimi ni mhifadhi na nilishaapa na ni msimamo wangu, siko radhi kushiriki kuharibu uhifadhi kwa sababu ya umashuhuri wa kisiasa, lakini wenzangu hatuelewani kwa sababu hatusikilizani, approach yao siyo sahihi na mimi siwezi kunyamaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninawauliza mara kadhaa, miaka ya nyuma Jeshi la Uhifadhi au niseme zamani maliasili nzima hatukuwa na silaha za kutosha, hatukuwa na magari ya doria ya kutosha, hatukuwa na Askari wa kutosha, lakini sasa hivi kila kitu kimeongezeka. Tuna Askari wengi, silaha za kutosha, tuna magari ya kutosha, lakini je, uhifadhi uko salama? Uhifadhi hauko salama. Sasa jambo hili linapaswa liwafikirishe kwamba they have to change approach ya conservation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tushirikishe sisi tutazungumza vizuri na watu tuwaelekeze na tutakubaliana, mambo yatakwenda, lakini muda mwingi hawashirikishi Madiwani wala Wabunge. Wanasema hawa wanasiasa wakorofi. Wanafanya vikao kama siri. Jambo jema la conservation ni la wote, lakini linafanywa siri kama la magendo, Wabunge na Madiwani wanatengwa hawawashirikishi. Unaona mtandaoni vitu fulani vimeshafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni mgeni kwenye Wizara hii, ni kijana lakini sina mashaka na uzalendo wako, nakupa nafasi, fanyia kazi. Naomba kwa sababu bahati nzuri wewe sio mhifadhi, nadhani ni mwanasheria, hebu tusaidie kubadilisha thinking approach towards conservation. Hatupingi, lakini wenzangu hawaelewi hawashirikishi wanataka waseme bwana hawa wenzetu wanasiasa wakorofi; sisi ni wanasiasa lakini pia wataalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mhifadhi, lakini humu kuna wanasheria na pia kuna Ma-engineer. Kila taaluma iliyoko Serikalini iko Bungeni. Tushirikisheni tutafanya mambo yaende kuwa marahisi, hakuna kiasi chochote cha silaha au Jeshi, uhifadhi na kadhalika ambao kinaweza kusaidia uhifadhi upone bila ushirikishaji. Tusikilizeni, hata nikisema Waheshimiwa Wabunge tufanye vikao tutumie mafuta yetu tutafanya. Lakini wanakuwepo wanaangalia sijui DC, kule kwa Mkurugenzi wanaongea vikao vya ndani, mimi nakaa nawaaangalia, lakini mwisho wa siku utaonekana. Kwa hiyo mimi sisemi kwa sababu Waziri ni mgeni, tutaongea wakati mwingine in case nikiona mambo hayaendi kama ambavyo inapaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu muundo wa Jeshi la Uhifadhi ambao upo sasa hivi. Kuna changamoto kadhaa, Mheshimiwa Waziri naomba uzisikilize. Ya kwanza Jeshi la Uhifadhi halina Mkuu wa Jeshi la Uhifadhi, kwa maana Kamishna Jenerali, kama Jeshi hili ni moja. Lakini ya pili kuna changamoto ya majina kijeshi kwenye vyeo ambavyo maafisa wadogo na wapiganaji wanavyo. Lakini la mwisho ni kuhusu mrundikano wa Makamishna wa Kanda wa Jeshi moja la Uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi hili nadhani mnafahamu, kama Jeshi lingine ambalo tunayo hususani Polisi, Magereza na kadhalika wana Makamishna Jenerali. Kwa hiyo nilitaka nijue kama Jeshi la Uhifadhi tumekubaliana ni moja basi lazima liwe na Kiongozi Mkuu pale juu lakini leo hakuna. Kamishna wa TFS anafanya mwenyewe, wa TAWA the same Kamishna wa Ngorongoro, Kamishna wa TANAPA kila mtu anafanya mwenyewe ndiyo final. Lakini nikawa nimeuliza hata swali siku moja hapa Bungeni, kwamba in case Rais anataka kuongea na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu Jeshi la Uhifadhi mnampeleka nani? Hapa Wizara ikanijibu ikasema Katibu Mkuu ndiye anakaimu. Katibu Mkuu ni mtu mkubwa sana kukaa na hawa Makamishna Jenerali kwenye level. Hata hawa Wizara ya Mambo ya Ndani kuna Wakuu wale Makamishna Jenerali lakini pia kuna Katibu Mkuu wao, hata Jeshi la Wananchi kule kuna CDF Mkuu wa Chombo lakini kuna Katibu Mkuu, Maliasili kuna shida gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi jambo hili na pia nishauri, washauriane jambo hili na ndugu zangu, pengine Makamishna wa Jeshi la Uhifadhi pengine najua wazee wangu labda wana hofa na wanasema mimi nitakuwa nani kukiwa na Bosi juu. Niwatoe hofu tunatengeneza mfumo wa kudumu kwa ajili ya nchi siyo kwa ajili ya kwao. Kesho wao hawatakuwa pale walipo kama ni Makamishna, kesho mimi sitakuwa hapa kama Mbunge. Kwa hiyo tutengeneze kitu ambacho kimekamilika. Mpaka leo hakielezeki kwa nini hakuna, haielezeki. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba nikupe kama changamoto ili ulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu suala la vyeo vile vya kijeshi kwa maafisa wadogo pamoja wale wapiganaji. Mtu mwenye nyota mbili, wanafahamu majeshi yote hususani Magereza, Polisi, anaitwa inspekta, huku Jeshi la Uhifadhi hawatumii majina hayo wanasema huyu ni Conservation Officer One au Two na kadhalika. Yule Koplo au Sargent anaitwa Conservation ranger two and whatever, vitu vya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema hayo ni majina mazuri lakini majina ya kiutumishi ya kiraia, kwa sababu hata Polisi mwenyewe anaitwa Police Officer, Magereza anaitwa Prison Officer, lakini military naming anaitwa Inspector au Assistant Inspector au Mratibu, wherever wherever. Kwa nini Jeshi la Uhifadhi hakuna? Haielezeki. Sasa shida naona ilianzia muda mrefu iliyoundwa kikosi cha raia huko katika Jeshi la Uhifadhi kutengeneza mfumo wa Jeshi labda ni shida ndio ilianzia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri ulichukue hili ulifanyie kazi, ni vitu ambavyo havieleweki. Hawa maafisa wanapokutana na wenzao wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi, wamevaa kiraia anataja cheo gani? Anasema mimi ni Conservation Officer Nyota mbili hizi sawasawa na Luteni unaanza kujieleza kwa nini. Jeshi halina maelezo ukishakiona kimesomeka straight forward; na kwa majeshi hili si jambo jipya. Sasa hawa TANAPA, TAWA, TFS Ngorongoro wanaonekana kama umekuja na kitu cha peke yako kutoka peponi ni suala la kukopi vyeo vya polisi ku-paste huku biashara imeisha, wakijichekecha nani anatosha wapi, lakini hawafanyi. Kwa hiyo nikushauri Mheshimiwa Waziri lifanyie kazi hili kwa sababu ni kituko. Jeshi jipya bado halija-commend…

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kweli nataka kumsaidia mchangiaji, kama ni kweli hawa hawaeleweki, wana vyeo lakini havieleweki vyeo vyao ni vipi basi tuseme tu hawa ni Mgambo. (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Antipas, unapokea taarifa?

MHE. ANTIPAS. Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napata ukakasi kwa jina alilolitumia lakini kimsingi ni kweli, ni Jeshi ambalo halijanyooka, sasa jina zuri sijalifahamu ni lipi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mgeni nikushauri kwa nia njema kabisa hata mimi nilikuwa Officer nilikuwa Assistant Inspector nimestaafu nikiwa na nyota yangu pale nikikutana na wenzangu nimevaa kiraia nashindwa kujieleza, story ni nyingi. kwamba unajua hii iko vile, why? Nyota moja ni Assistant Inspector, inyooke hivyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba hili ushauriane na makamishna usishauriane na watumishi wenzangu wa Jeshi hili, tafuta vyomba, kaa navyo, wapeni mfumo maelekezo watekeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye angle hii, nilizungumza, hata kitabu changu niliandika kuhusu maisha yangu ya jeshi, na nimeshauri vitu vingi sana. Tungekuwa Jeshi linalofanya kazi kwa umoja hizi division, TAWA na TANAPA, wangekuwa pamoja kusingekuwa na utitiri wa hivi vyeo na kadhalika. Leo hii kuna Kamishna wa TANAPA wa Kanda ya, lakini wakati huo TAWA nao wana Kamishna wa Kanda ya Kusini, TFS wanafanya vivyohivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku Iringa, Mbeya kuna Kimondo sijui kuna vitu kama viwili vya Ngorongoro. Kwa hiyo Ngorongoro nao waweke Kamishna wao kwa ajili ya vitu, havieleweki. Alipaswa awepo mtu mmoja ndiye awe Kamishna wa Jeshi la Uhifadhi wa Kanda fulani, wengine wote wadogo wenye station watalipoti kwake na yeye atapeleka juu. Lakini kinachofanyika sasa hivi kwa kweli sina imani nacho. Naamini wenzangu Wizarani mnakiona, naongea kwa nia njema kabisa. Tunatengeneza mfumo wa jeshi ambao umenyooka na si kwa ajili ya mtu mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri natamani Bunge la mwezi wa tisa tusiongee mambo haya na wala tusigombane. Nashukuru sana, ahsante sana. (Makofi)