Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tangu asubuhi jina langu linakosewa. Ninaitwa Mwita Mwikwabe Waitara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa nafasi ya kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii, na nataka nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Tarime Vijijini, kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa sababu ya maelekezo yake mazuri ambayo angalau hali ya utulivu imerejea kule jimboni kwangu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kauli yake ambayo aliitoa hapa Bungeni amabyo pia iliendelea kupooza watu wa Tarime. Nimshukuru pia Mheshimiwa Spika, alitoa mwongozo mzuri mara kadhaa. Lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Comrade Mohamed Mchengerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu Waheshimiwa Wabunge ndiye Waziri wa Maliasili wa kwanza kufanya mkutano Tarime na ukaisha kwa amani watu wakacheka wakaondoka. Na Mheshimiwa Mchengerwa Wazee wa Tarime wamekuandalia zawadi, siku ukirudi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kama ulivyoahidi kabla ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda pale utapata kitu kinaitwa kichuli ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Mchengerwa, anajua kutibu makovu. Mheshimiwa Mchengerwa namna ambavyo uliingia Tarime uliacha hawa wanaitwa Majeshi ya Uhifadhi pembeni ukaenda kiraia ukaingia moja kwa moja kwenye mkutano, walijenga imani kuanzia muda ule mpaka unaondoka Tarime, nakushukuru sana. Na ile, walisema tu kuwa Mheshimiwa Mbunge tukipata watu kama akina Mheshimiwa Mchengerwa kwenye migogoro, hata kama mgogoro hauishi watu wanapona bila kupata matibabu, hongera sana Mheshimiwa Mchengerwa. Ndiyo maana unasifiwa namna ambavyo uli-handle mambo ya Michezo. Hii ni Wizara ambayo ilikuwa haina jina kubwa lakini ameipa heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaturajia sisi ambao tunakaa karibu na Hifadhi ya Serengeti Mheshimiwa Mchengerwa ufanye mambo makubwa zaidi yale ya Wizara ya Michezo, na usuluhishe migogoro kwa sababu asilimia 50 ya nchi hii ni hifadhi za Taifa. Kwa hiyo ukiweza kuleta amani na mahusiano mazuri kati ya wananchi na hifadhi zetu maana yake kura za Mama Samia, kura za Wabunge, kura za Madiwani na kura za Chama cha Mapinduzi ziko kwenye mikono salama. Tunakutakia kila la kheri katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mhcengerwa alipokuja kule alipewa ujumbe, kwamba pamoja na kwamba yamefanyika mambo mazuri sana lakini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri watu wa Tarime wanahitaji waombe radhi kwa kauli ile. Kwamba yeye ametumwa na Serikali ni kauli ya Mama na kwa hiyo kule si chooni. Watu tisa walikufa wakapotea mpaka leo; aliulizwa na akina mama wenzake. Mheshimiwa Rais ndiye mfariji namba moja wa Taifa kwa mujibu wa Katiba. Viongozi lazima mkinge kumuongelesha Mheshimiwa Rais mambo maovu ambayo hayana maana sana, lakini pia kutoa matumaini pasipokuwa na matumaini, kupeleka amani mahali ambapo hakuna amani. Kauli ile tu Mheshimiwa Waziri ndiyo imebaki kwenye Wizara yako; mengine yote Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa humu Bungeni ilisheheni vitu vingi sana, alizungumza namna ambavyo ng’ombe wa watu wanataifishwa, alionyesha mahusiano mabovu yaliyopo, aliangalia shida ya malisho, akaangalia shida za kilimo, akaangalia kila kitu. Mimi ningekushauri, pamoja na Waziri wa Ardhi, ile hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya hali ya migogoro nchini ichukuliwe, kila Waziri achukue kipande chake atengeneze mpango kazi wa utekelezaji, mtakuwa mmetibu sehemu kubwa sana ya migogoro ya ardhi na mahusiano katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, amesema jambo zuri na wenzangu wamezungumza. Kwamba, migogoro hii huwezi kufanya peke yako, kuna viongozi kule. Kuwa kiongozi, kwamba umekuwa Waziri au umekuwa si kwamba umekuwa na akili nyingi kuliko wote, shirikisha. Kuna watu wana utashi pale na kuna watu wana uelewa. Timu uliyosema utaunda tushirikishe tukushauri ni jambo jema, utapata mambo mengi sana na utamsaidia Mheshimiwa Rais na migogoro; tunaamini kwamba bajeti ijayo malalamiko ya Mbuga kuwalipa wananchi itapaungua humu Bungeni. Kwa hiyo tunakushukuru kwa hatua hiyo ambayo umeona. Mimi namfuatilia; hata kama amekaa Wizara tatu kwa miaka mitatu, ni kwamba Mheshimiwa Rais anamtumia vizuri, kuna vitu vya msingi sana kwake na ndiyo maana watu wote wanamuunga mkono katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo migogoro kule Mkoa wa Mara. Hifadhi ya Serengeti asilimia 75 iko katika Mkoa wa Mara. Lakini mgogoro huu utaukuta Bunda, Tarime, Serengeti, na unakwenda mpaka kule Arusha, mgogoro unaenda mpaka Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, ni vizuri ukae vizuri na watu hawa ili uweze kutatua. Mnapokwenda kujadili migogoro ya hifadhi msione kuwa wanyama ni bora kuliko watu. Kuona kwamba wanyama ni bora lakini pia na watu ni bora pia tuna wahitaji. Kama tunafanya uhifadhi tunufaike ni kwa ajili ya watu wetu. Ni vizuri watu wasilie wanyama wanacheka, watoto wafurahie matunda ya nchi hii. Kazi hiyo umepewa Mheshimiwa Mchengerwa, na tunaamini kwamba unaweza ukaifanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tunayo barabara ya kutoka Serengeti kule inaenda mpaka Ngorongoro, imeahidiwa ijengwe kwa kiwango cha lami lakini hijajengwa. Pale Serengeti hakuna hata uwanja wa ndege. Ukiuliza inakotoka bidhaa inayotumika pale hifadhini inatoka nje ya Mkoa wa Mara. Hakuna ajira, hakuna kazi kwa akina mama, vijana wetu wanazurura pale mtaani wanakutana hawapati ajira, mahusiano mema hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata mazungumzo yanakuwa ya uadui mkubwa kwa sababu wanaona kwamba wanufaika ni watu wengine ilhali Hifadhi ipo kwetu. Kwa mfano Tarime, mimi nalalamika hapa kila siku lakini hakuna hata senti moja kama service levy kutoka Hifadhi ya Serengeti kuja Tarime pale. Sisi tunaambulia tembo kuua watu, tembo kula mazao, ng’ombe kupotea, watu kupotea, watu kufirisika na uhasama. Pia hata hiyo CSR hakuna mpango mkakati, ukiuliza hawezi kukuambia ni kitu gani hasa wanataka kufanya. Wanaweza wakachimba kisima leo kesho wakakuambia kisima kipo hifadhini. Tunaomba hii mipango pia iwekwe sawasawa ili watu waweze kunufaika vizuri, tunahitaji pale uwanja wa ndege ili tuweze kufanya kazi ya kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Mchengerwa amekuja kule Kuhancha Golong’a na Nyanungu, yote tutazungumza lakini watu wangu pale ambao ninawawakilisha hapa Bungeni wanahitaji sehemu ya kuchungia mifugo yao, wanahitaji sehemu ya kulima, wanahitaji sehemu ya kuishi. Wale ni wakulima na wafugaji wala si wafanyabiashara. hata ukiwapelekea fedha wakila ikiisha watarudi palepale, na ndiyo maana walikwa na hasira kubwa. Lakini maneno yako yana matumaini, kwamba tulieni Mama anawasikiliza na utarudi mgogoro utaisha, na kwamba waendelee kulima. Kauli hiyo imeponya makovu yote ambayo ambayo yalikuwa yanakwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri. Tulimpa risala Kalikatonga, alipata risala Nyanungu na Gorong’a, yale ndiyo maombi ya watu wa Tarime na mimi ndiye Mbunge wao; naomba ayafanyie kazi tutampa heko sana kwa kufanya kazi hiyo. Wale watu wana makovu tangu wakati wa uhuru. Ni wakati huu wa Mama Samia, kama Mama, mzazi, mlezi na mwenye huruma wapete unafuu wa maisha yao. Wao wana matumaini, wajenge nyumba za kudumu, mifugo yao iishi wasomeshe watoto ili wapate maisha bora sawa na Watanzania wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hakuna namna ya kupata maji kule tofauti na kuchota maji ya Mto Mara. Kama mtaweka miundombinu pale kwa teknolojia ya kupata maji wakati wote tutawashukuru sana. Maji ya chumvi hata mimi nimekulia pale wote wamepeleka katika Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie Mheshimiwa Mchengerwa jambo ambalo linajadiliwa sana kule Bunda. Habari ya Nyatwali imeleta taharuki kubwa na kwa kweli wanaona kama watu hawa wanabaguliwa. Tusifanye double standard, watu wale wa Ngorongoro wamepelekwa kule Kilindi wale wamepewa usafiri watu wa Tarime na Bunda waliona. Wamewezeshwa kwa miundombinu, kuna huduma za kijamii, kuna maji, kuna shule, kuna huduma za afya zinapatikana, wakapata pia na fedha ya kuanzia maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watu wa Nyatwali wakipewa milioni mbili hauwapi eneo la kwenda kuishi, wana makaburi yao, wana familia kubwa, wana watoto, wanasomesha, wakaanze maisha lakini mambo haya Mheshimiwa Waziri hebu jiweke ungekuwa ni wewe ungefanyaje? Ni very unfair. Hapa mimi naona ni kama kuna watu wengine wanapendwa zaidi wengine hawapendwi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mngetaka kutatua migogoro hii ni vizuri mkaangalia as whole, kwa ujumla wake. Wote ni Watanzania tunapenda hifadhi ziwepo, nchi ni ya kwetu lakini watu wasiishe kulalamika na kulialia kama wanabaguliwa. Kazi hiyo Mheshimiwa Waziri umepewa, mimi naamini unaweza kuifanya kazi hiyo, na nitakupa ushirikiano na Mheshimiwa Rais amekuamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa nilipo leo naweza nikaenda Nyanungu nikatembea mtaani kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametoa kauli nzuri sana. Naweza nikaenda Kuyanja nikapokelewa nikapewa uji na Kichuli kwa sababu umetoa kauli nzuri. Nikienda Nyakatonga nitalala, nilikuwa siwezi kwenda kulala. Na kwa taarifa yako Mheshimiwa Waziri nilikuwa nimeamua nisiende maeneo yale mpaka mtakapo toa kauli. Kwa hiyo sasa Bunge likiisha nimeshapanga ratiba ya kwenda kuongea na watu wangu kwa kuwa Mama amesema mgogoro utaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote hawa wanampongeza sana Mheshimiwa Mchengerwa, wanampa ushirikiano na wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tunachotaka ni kutatua migogoro hii ya hifadhi na wananchi. Hifadhi iwepo, watu wawepo, maendeleo yawepo, watu wasome, watu wajenge na siasa iendelee, na 2025 tunataka Chama cha Mapinduzi kishinde kila kona kupitia kwako kwa kuondoa migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sishiki shilingi ninafuraha kubwa kwa kweli kwa Mheshimiwa Waziri nakuunga mkono kwa asilimia 100. Ahsante sana kwa nafasi.