Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RIZIKI S. LULINDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nami kwa kunipatia hii nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Maliasili. Mimi naitwa Mama mjusi, Mama Selous, Mama Mazingira lakini vilke vile ni Balozi wa Utalii; nilipewa tuzo hii na Mheshimiwa Rais. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa tuzo aliyonipa, kwa hiyo nitasema nitaongea ukweli na sitamwangusha. Kwa vile mimi ni mwanahifadhi lazima kwanza nitasimama na hifadhi na haki za binadamu ndani ya maliasili zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilikuwa naye katika michezo, kazi aliyoifanya katika michezo mpaka timu ya watu wenye ulemavu tuliweza kufikia katika mpira wa World Cup. Na imani yangu wale waliokwenda kurithi kule watafanya kazi kama aliyofanya Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu tufike tena, maana mwaka huu tena kuna mpira wa Afrika utafanyika Misri. Matumaini yangu ni kwamba timu yangu imejiandaa, na wale tuliokuwa naowalioingia sasa hivi tuwe nao vizuri ili hawa vijana ambao wamecheza katika mpira wa watu wenye ulemavu; sasa hivi tunazungumzia vijana kumi wako Ulaya huko wanalipwa katika professional soccer; Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu hongereni sana. Vilevile nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ya kupambana na hali ngumu sana. Hii ni Wizara moja wpo katika Wizara ambazo ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika uhifadhi nitazungumzia kwanza Mbuga kubwa, ikiwemo Ruaha, Serengeti lakini pia tuna Mbuga ya Selous nayo ni mbuga kubwa ya kwanza Afrika lakini ya pili duniani. Lakini niizungumzie ya tatu, tuna corrido za wanyama ambazo ni ambazo wanapita. Asilimia 20 ya ardhi ya Tanzania ilitengwa kwa ajili ya uhifdhi, faida yake ya Uhifadhi tumetegemea kupata mvua, tunategemea mito itatiririka ili maji yasaidie katika kilimo, hivyo kuondoa uhifadhi ndio maana unaona sasa hivi ni ukame unakuwa mwingi kutokana na maeneo mengi yameharibiwa. Mimi nalizungumza hili kwa ninayoyajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbuga ya kwanza ambayo ninataka niizungumzie ni Mbuga ya Ruaha (Ruaha National Park). Ruaha National Park inategemea maporomoko ya Congo Basin ambayo yanateremsha Usangu, Usangu inaingia Ruaha, Ruaha maji yake yanakwenda Kihansi, kilombero yanaingia Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maji yanasaidia Wizara ya Nishati na Madini, tukiyaharibu maeneo haya nchi itaingia gizani na matokeo yake itakuwa ni malalamiko makubwa zaidi. Na gizani hapa siyo Tanzania Bara tu, umeme unatoka katika maeneo ya Kilombero mpaka Rufiji unakwenda mpaka Zanzibar. Ina maana nchi itakuwa gizani, na itakapokuwa nchi gizani uchumi wa nchi utaporomoka, hivyo tuwe waangalifu sana. Na ukiangalia Ruaha National Park ukubwa wake si mkubwa hivyo kama watu wanavyofikiria. Niliangalia katika google wameniambia Ruaha National Park ina ukubwa wa square mita za mraba 13,800, nimeangalia Selous 44 niliangalia Serengeti 12,500. Niwapongeze ma-DG, Wakurugenzi Wakuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa Ngorongoro, TAWA na washikadau wote wa maliasili kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana ya kupambana na watu ambao si waaminifu. Kuna watu waaminifu na watu wengine wanaingia ndani siyo watu waaminifu. Mimi nuilikuwa na mojawapo mdau ambaye nimezunguka Tanzania nzima na Wabunge baada ya kupata kelele kelele hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tukaenda kujionea uhalisia, wafugaji wanaingia ndani ya mbuga na ng’ombe wakiwa na bunduki za kihalifu machine gun. Hivi kweli wewe katika mbuga kuna simba kuna tembo, kuna nyati makundi kwa makundi, wewe unaingiaje pale, ina maana wewe ni muhalifu na wafugaji wengi wanatumika. Tukubaliane Waheshimiwa Wabunge wafugaji wengi wanatumika na una muona mfugaji ana mifugo 4,000, ukiwa na ng’ombe 4,000 zungumza kuwa wewe ni bilionea una bilioni 1.2. Kitu ambacho hata Mbunge sitegemei kuwa na hela kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu tufanye database ya kuwajua wafugaji wote wenye ng’ombe wengi halafu tuwatengenezee mifumo utajiri wao ule uweze kuwasaidia na tutajua kama wafugaji hawa ng’ombe wale ni wao au wanatumika na watu wengine kama mlivyoona Ngorongoro. Katika kuhamisha Ngorongoro tulitegemea watu watakuja Handeni na ng’ombe wengi sana. Waliambiwa kuna ng’ombe 5,000, 4,000, 3,000 siku wanakuja kuhama mtu anakuja na ng’ombe watano, ng’ombe 10 kitu ambacho mengi yalioletwa katika taarifa unaweza ukapata katika mitandao ni vitu vya kuzusha na kuwafanya watu na nchi iingie katika taharuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza hiyo ukiichukulia Mbuga ya Serengeti kwa ukubwa wa square mita za mraba 12,500, kwa kweli unategemea Mto Mara upate maji na kama utakuwa unategemea Mto Mara kupata maji watavua, watapata samaki na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unamuona mfugaji anaingia mule ndani kila siku tumege tumege tukapomaliza kumega mtasema bado Mto Mara umeshakauka. Je, mimi nayaona mapori makubwa makubwa yameachwa Tanzania hayajatumika, naomba Wizara ya Ardhi isimame na Wizara ya Maliasili watengeneze mfumo na mpango mkakati wa kuhakikisha baadhi ya wafugaji wanakaa katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano hai, wafugaji walipelekwa Mkoa wa Lindi, Mtwara walikataa leo Lindi maeneo yote waliyopewa wamehama, wamekimbilia Selous, unaona neno hilo. Wamehakikisha kuwa misitu yote kuanzia Rufiji wamekata na sasa hivi Lindi ni jangwa. Wamekimbia maeneo walipewa kila mfugaji square mita za mraba 5,000 mtu wa kawaida ambaye huwezi kupata lakini wameshakata misitu, wamekata kila kitu wamechoma mkaa, sasa hivi tunazungumzia Selous wanakwenda Selous. Sasa tunajiuliza kweli huu ni ufugaji au ni uharibu, tujiulize na tujipe tathmini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbuga ya Tendaguru; Tendaguru ni eneo ambalo tuna misitu ya na miti aina ya mipingo hapa ndipo alipotoka yule mjusi mpaka mimi napata jina la Mama mjusi. Tumekwenda na Naibu Waziri, wafugaji wote wamehamia pale waliokatiwa maeneo yao maeneo chungu nzima walipewa wamekwenda kukaa Tendaguru. Matokeo yake Tendaguru tembo hawakanyagi anamuogopa mfugaji, Tendaguru simba hakanyagi anamuogopa mfugaji, Tendaguru unaiona imekaa pale wamejaa wafugaji na mifugo yao wanaharibu mazingira wanamaliza miti ya mipingo kauli za viongozi nazo zinarudi kwenda kuangali nilitoa amri hawa wafugaji waende katika maeneo yao lakini bado wamebakia maeneo hayo kwa nini hawajaondoka lakini akiongea mtu akiondoka wafugaji hawagusi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo tunaizungumzia Milola, tembo wanakimbilia Milola tembo wanakimbilia maeneo ya pembeni kwa vile nini, maeneo yao yamezingirwa. Tunaanzia Nyasa anavukwa corridor kuingia Namtumbo, corridor limevamiwa na hizo ziko ndani ya GN. Tunatoka Namtumbo tunaingia ndani ya Selous wafugaji wako ndani ya Selous hivyo wakikaa ndani ya Selous na wanaingia na magobore tembo wanakimbia katika maeneo ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, sasa hii kitu tukubaliane ninaomba tukitoka hapa tutaandaa timu ya kuhakikisha timu hii itakwenda kujua wafugaji hawa ni wapi? Na ni wachache kweli, wafugaji wako Kilimanjaro, wanafuga hakuna migogoro, wafugaji wako Arusha, wanafuga hakuna migogro wafugaji wako Shinyanga Mwanza lakini hawa wanayehamahama si wafugaji ni wafanyabiashara na wanatumika na hii kutumika tunaifanya nchi ina - paralyze. (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lulida pokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Mama yangu pale Mheshimiwa Lulida, kwa kweli kule kusini hakuna wafugaji kule kuna wachungaji. Wafugaji wapo hapo Ruvu kama ulivyosema wako Ruvu wako huko Kigoma wapo hapo Kongwa wale ndio wafugaji, kule kuna wachungaji na ndio maana wanasumbua.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Riziki Said Lulida, unapokea taarifa?

MHE. RIZIKI SAID LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokea taarifa mimi natoka Selous, nimezaliwa Selous, ninaijua Selous tumekaa na tembo tukiwa marafiki lakini baada ya …

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, … wafugaji kwenda kuhama hama Tanzania nzima leo nasikia Mbeya…

MWENYEKITI: Ahsante sana na muda wako umekwisha.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haijafika dakika kumi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.