Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Hoja ya Wizara ya Maliasili. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri kwa kuteuliwa kuongoza wizara hiyo ni miongoni mwa Wizara ambazo tuseme ni ngumu au zina changamoto nyingi. Historia inaonesha Wizara hii haijawahi kuwaacha Mawaziri salama huwa hawamalizi muda wao, huo ndio ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunakutakia kheri na tumeona jinsi ambavyyo umefanya kwenye Wizara ya Utamaduni, sasa uko Wizara ya Maliasili, jitahidi tu utulie, uielewe vizuri wizara na sekta zake zote, upate ufahamu ufanye engagement na wadau mbalimbali, usikilize maoni ya wananchi, usikilize maoni ya Wabunge, utatue changamoto za muda mrefu na utafanikiwa na unaweza ukadumu hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo nianze pia kwa kutoa pole kwa familia ya baba mmoja wa familia ambaye ameuwawa leo asubuhi na tembo akiwa shambani kwake katika Kata ya Oldeani, Wilaya ya Karatu, Mungu amlaze mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia hoja yangu ya kwanza migogoro mingi ambayo tunaiona kati ya hifadhi na wananchi na yote ambayo yanaendelea kwa namna moja ama nyingine, migogoro hii ni ya siku nyingi baadhi ya maeneo ni migogoro ambayo imechukua muda mrefu. Ni migogoro ambayo ukimuuliza leo mwananchi wa kawaida ambaye yupo kwenye haya maeneo ambayo yanazunguka hifadhi, kwanza mwananchi huyo haioni umuhimu wa hifadhi wala haitamani kwa sababu anapambana na hiyo changamoto ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwambia mwananchi kwamba sekta hii ni sekta muhimu kwa uchumi wa nchi, ni sekta muhimu kwa kuliingizia nchi fedha za kigeni hawezi kukuelewa. Kwa sababu wameshakumbana na changamoto ya muda mrefu ambayo haitatuliki. Kwa hiyo, tunahitaji Mheshimiwa Waziri, unahitajika kwanza kurudisha imani kwa wananchi wote ambao wamekumbwa na hizi changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kujenga mahusiano mazuri, kumfanya mwananchi aone umuhimu wa hifadhi katika eneo lake yaani aone umuhimu na kutambua. Sasa wataweza kuona na kutambua kama atasikilizwa na baadhi ya changamoto ambazo amekumbana nazo za muda mrefu ziweze kuondoka na hatimaye kwisha kabisa. Naamini inawezekana, hasa migogoro hii ukisikiliza wataalamu wanasema kabisa migogoro hii ni kwa sababu kuna wananchi wamevamia shoroba, kuna wananchi wameingia kwenye maeneo ya hifadhi, kuna mifugo inaingizwa hifadhini na mambo wakadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza mfano swali moja ni kwa namna gani kwanza tumetambua shoroba zote? Hivi kuna takwimu sahihi ya kutambua shoroba zote ndani ya nchi hii? Halafu kuziainisha kwa kuweka labda category A, B, C zipi ambazo zimevamiwa kabisa kiasi kwamba hakuna namna inabidi tuziachie au zipi ambazo sasa zimevamiwa kwa kiasi kidogo zinaweza zikanusurika kwa kufanya maamuzi magumu ku-compensate na kuondoa wale wananchi na kuwapelekea maeneo mengine ili kuhakikisha shoroba zinaweza kendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo yanatakiwa yafanyike kwa utulivu kwa usahihi na kufanya maamuzi magumu kwa kuwekeza fedha kama kweli tunataka kuona migogoro hii ina pungua lakini kuimarisha hizo shoroba. Ni kwa sababu tunahitaji hifadhi, tunahitaji wananchi wetu tunawahitaji, tunahitaji mambo yote. Tunahitaji hifadhi na sekta kwa ujumla isaidie katika uchumi wa nchi lakini haya yote tutakapoyahitaji maana yake lazima tufanye balancing ya mambo yote haya kwa pamoja lakini kingine kinachokosekana, unakuta kwenye eneo la shoroba kumejengwa mpaka ofisi hata za Serikali. Tunaambiwa hapo Mvomero, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imejengwa kwenye shoroba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza hivi mpaka inajengwa inatengenezwa plan mpaka inajengwa kumbe imejengwa kwenye shoroba. Tafsiri yake ni kwamba ama hakuna proper coordination sahihi ama utaratibu wa kupanga ardhi yetu haukamiliki au haufanyiki kwa wakati ama kuna uzembe na vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naamini kati ya kazi kubwa ambayo itakiwa kufanywa sasa ushirikiane na sekta zingine zinazohusika kwa maana ya Wizara zingine. Mfanye matumizi bora na kuzitambua haya yanayoenekana leo yasijirudie. Yaani tujue na kuzitambue kwamba hapa ni shoroba, hapa panatakiwa kujengwa hapa hapatakiwi hapa ni hifadhi hapa ni mpaka na kila kitu ndipo ambavyo tutaweza kwenda kupunguza na kuondoa migogoro hii ambayo inatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa ambayo wananchi wengi wanajiuliza na mimi nikiwepo najiuliza. Hivi ni kwa nini inapotokea mwananchi kwa namna moja ama nyingine ama amekutwa kwenye shoroba au ameingia hifadhini au wanyama wamekufa, kwa nini inatumika nguvu kubwa na askari wa Jeshi la Uhifadhi, hivi ni kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea vizuri sana Mheshimiwa Musukuma asubuhi hapa ni kwa nini ni mafunzo yao ndio yanawafanya kwamba ukimuona mtu ni sawa sawa umemuona jangili unamfyatua tu risasi au ni nini yaani kwanini nguvu kubwa sana inatumika? Haya mambo yanasikitisha sana, yaani iko namna ya kuangalia ama kulifumua jeshi hili kwa ujumla na kuangalia namna iliyobora ama sijui wapewe maelekezo ama wapewe mafunzo kwa upya ama kuangalia mafunzo yao. Nadhani hatua ya kwanza sio kutumia nguvu kubwa, tuone namna ambayo inaweza kama kweli mwananchi ana makosa kuna namna, ndipo ambavyo hata askari akimkuta mwizi hawezi kumpiga risasi hivi hivi si atamkamata atampeleka kituoni na hatua zingine zitaweza kuendelea. Kwa hiyo, nadhani hata jeshi hili liwe na namna bora ya kuhakikisha inakabiliana na migogoro hii kwa namna iliyo sahihi bila kumuumiza mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu la Karatu tunapakana na Hifadhi ya Ngorongoro, tuna changamoto kubwa sana ya wanyama kuingia kwenye vijiji vya wananchi. Tuna kata karibia sita ambazo tumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya wanyama kutoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya wananchi. Kama ambavyo nimeeleza kuna mtu mmoja leo amefariki na wengine kadhaa huko nyuma wamejeruhiwa na mazao kuweza kuharibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafahamu kuna mpango kupitia bajeti ya mwaka huu ambayo inafanywa na Hifadhi ya Ngorongoro kujenga fensi ya umeme ya kilometa 30 ili wanyama wasianze kutoka kwenda kwenye maeneo ya hifadhi. Hili ni jambo jema sana tunawapongeza kwa hilo lakini kama haitoshi pia kuna vituo vya polisi vitajengwa takribani 15 kupitia fedha za mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kama ambavyo mmeweka kwenye bajeti yenu hiyo electrical fence ambayo mnataka kuweka tunaomba muweke kwenye vipaumbele yale maeneo ambayo ni korofi zaidi. Muyatangulize haya na maeneo mengine yaweze kufuata lakini pia Mheshimiwa Waziri unaweza kuchukua sample hii ya Ngorongoro kupeleka kwenye maeneo mengine Nchi nzima ambapo kwa kiwango kikubwa wanakabiliana na changamoto hii ya wanyama kutoka kwenye maeneo ya hifadhi kwenda kwenye maeneo yao kwa kuweka hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua ni gharama kidogo lakini ifike mahali hichi tunachokipata kutokana na Sekta hii ya Utalii irudi kwa wananchi kwa kuwapa unafuu, kwa kuweka hizo fensi ili wananchi waendelee kuishi kwa amani katika maeneo yao. Mifano mizuri mnaweza kwenda kujifunza hata South Africa wanatumia sana hii ili kuhakikisha wanyama wanabaki salama kwenye eneo la hifadhi lakini mwananchi kwenye eneo lake nalo anabaki salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze sana Ngorongoro kwa hatua hii tunamba basi mtekeleze ili Wananchi wa Karatu kwenye haya maeneo waweze kuishi salama katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala liliotokea juzi Mto wa Mbu, eneo la Jangwani. Mheshimiwa Waziri nimekusikiliza pia kwenye hotuba yako, nimesikitika kidogo. Kwanza mpaka leo vijana wawili ambao walikutwa kwenye ziwa na askari wa uhifadhi ambao walifungwa pingu walipigwa, mpaka leo hawajulikani walipo. Tunaomba mtuambie hawa vijana wako wapi familia zao zinalia, zinawatafuta kijana mmoja ni wa Karatu na kijana mwingine ni wa Mto wa Mbu. Vijana hawa mpaka leo hawajulikani, tunatamani kujua na wanatamani kujua na Mheshimiwa Waziri ikikupendeza uende ukae na hawa wananchi wa maeneo haya uwaambie na uwasikilize, kwa sababu kwenye hotuba yako umesema hawa wananchi walikuwa wanavamia walikuwa wanavamia boti ya askari wa uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sikiliza, askari wa uhifadhi wana boti za umeme, wananchi wa kawaida wanabodi za kawaida. Hivi inakuaje yaani mwenye boti ya kawaida ambaye haina nguvu na huyu mwenye boti ya umeme eti huyu wa umeme anatishiwa na mwingine, how come? Yaani haingii akilini. Mkatuambia hapa juzi kuna wananchi wameondoka na pingu, hivi askari wale wa Jeshi la Uhifadhi wana bunduki na mitutu, kuna mwananchi atathubutu kwenda kumchukulia hiyo pingu wakati amebeba hizo silaha, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba haki za wananchi hawa familia hizi zinalia halafu msiseme uongo pale ambapo pana ukweli mseme muombe radhi kwa sababu makosa yanatokea hakuna aliyemkamilifu, muombe radhi mseme ukweli, mzifikie familia hizi, msikie kilio hichi kilichofanyika ni unyama wa kupitiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hawa vijana wawili waliopotea, wawili wamefariki wengine bado majeruhi, kwa nini haya? Ndio haya nasema kwa nini inafikia askari hawa wa Jeshi la Uhifadhi wanatumia nguvu kubwa kukabiliana na wananchi pale ambapo inatokea hii changamoto? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ikikupendeza na kama utaona inafaa basi watembelee wananchi hao ukutane nao, usikie kutoka kwenye midomo yao itakuwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala mengine mawili kwa haraka haraka nimesikia kengele imegongwa. Suala moja ni mamlaka ya usimamizi ya wanyamapori TAWA. Hii TAWA imeanzishwa kwa amri ya kisheria chini ya kifungu cha nane cha Sheria ya Uhifadhi ya Wanyamapori na ina bodi ya ushauri haina bodi ya kiutendaji. Huko nyuma Kamati imeshauri mara nyingi sana iletwe sheria hapa Bungeni ya kuhakikisha TAWA inaundwa properly kwa mujibu wa sheria. Tuonaomba Mheshimiwa Waziri utapitia ripoti za Kamati utaziona, tunaomba TAWA ipewe mamlaka yenye nguvu kwa sababu ina kazi kubwa ya kusimamia mapori mengi ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Ziwa Manyara, Ziwa Manyara linaendakwisha na linaenda kupotea kabisa kwa sababu ziwa lile limejaa tope, maji hata yakiingia pale yakae muda mrefu. Mwisho wa siku tutaipoteza Hifadhi ya Manyara, tunaomba sana zifanyike jitihada za kuhakikisha Ziwa Manyara linakombelewa na linarudi kwenye hali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, …tunaomba ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ujenzi wa Barabara ya Serengeti, barabara ile haipendezi kwa wageni wanaofika kwenye eneo hili. Tunaomba mlifikirie mjenge kwa namna iliyobora bila kuharibu mazingira bila kuleta athari yeyote kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.