Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. Napongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na juhudi aliyoifanya kwenye ile shughuli ya Royal Tour ambayo ameendelea kuitangaza Tanzania katika uso wa dunia, lakini pia kuongeza mapato ya Taifa, kuongeza idadi ya utalii wa ndani na nje ya nchi, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza juhudi za Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua migogoro na kushirikiana na wizara hii kwa ajili ya kuweka hali iwe ya usalama katika Nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona amepambana na amejitahidi sana kwa shughuli ile kwa kazi ile na kadhia ile iliyokuwa ya Ngorongoro lakini pia na nchi nzima kona zote wanashuhudia utendaji wake wa kazi wa uweledi na ufanisi mkubwa, tunamshukuru sana. Alikuja hata maeneo ya huko Lindi, maeneo ya Nachingwea akaenda kuona na kuwapa pole wananchi waliotajwa na kadhia ya Tembo mwaka jana lakini pia akawapatia chakula na kuwapa pole wale walioathirika kwa kuuliwa na ndugu zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kazi ya Wizara hii, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii ya Maliasili na utalii hata kwenye ngazi ya mikoa kule na wilaya mbalimbali kwa kweli tunashukuru utendaji wao wa kazi tunauona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara hii ndio inatunza ule uhalisia wa siri ambao Mwenyezi Mungu alitupatia. Tuendelee kuitunza ardhi na miti na kila kitu ili itupatie usalama na afya kwa ujumla kwa kweli tunawapongeza sana. Sisi Wanalindi tunaahidi kabisa kutunza vyanzo vile vya maji na misitu na tuona kwa kiasi kikubwa Mkoa wa Lindi unachangia maji na uhalisia na uasili wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha kabisa sustainability ya ile bwawa na tumeona matokeo yake na mafanikio yake tutayaona kama waziri wa jana aliyekuwa amemalizia ku-present jana katika ile Wizara ya Nishati. Tunaona kazi ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kazi ya Wizara hii ambayo inaendelea kutunza Utalii. Hata sisi Lindi pia tuna vivutio vingi vya utalii. Tunaona kule Kilwa Kisiwani, Tendaguru, tunaona kule pia kwenye Bwawa ambalo lina viboko ambao wana rangi ya pink ambao ni nadra sana katika dunia hii kuwaona. Kuna vivutio vingi, karibuni sana Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi ni mojawapo ya mikoa iliyoathirika sana katika kadhia ya tembo. Hali kule siyo shwari, ni tete. Tumeona mwaka 2022 Wizara hii ilijitahidi, katika mikakati yake mojawapo ni kupeleka ndege kule. Walipeleka ndege ya kuswaga wale tembo kuwapeleka kwenye hifadhi na jambo lile lilifanikiwa na wananchi walifurahia sana wakaendelea na kilimo na maendeleo kwa ujumla. Tuliwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanyama wale wamerudi tena. Wamerudi tena kwa kasi kubwa, wako makundi kwa makundi, wameendelea kuharibu mazao, wameua watu na wanaendelea kuua kila kuchapo. Wilaya zile za Nachingwea, Liwale, Milola, Kilwa na maeneo yote yale kule yameathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali siyo shwari. Hivi sasa ninapozungumza, maeneo yale kuna njaa kali. Wananchi wale hawana chakula, watoto hawaendi shuleni kwa sababu ya tembo. Tembo wanazagaa kama vile unavyoona ng’ombe walivyozagaa. Kwa kweli hali siyo shwari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua pia mchango mkubwa…

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Tecla Ungele kwamba hali kweli siyo shwari, kuna tembo wengi ambao wanazagaa katika maeneo ambayo ameyataja, lakini kwa nyongeza sasa kuna fisi ambao wanasumbua wananchi nawanakula wananchi. Wananchi wameathirika sana na wanyama hawa, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ungele, unapokea taarifa?

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua pia mchango mkubwa anaofanya Mkuu wa Mkoa wetu wa Lindi Mama Zainab Telack na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Lindi na viongozi wengine, na pia hata Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kusini wanafanya kazi kubwa kweli. Wakiitwa mahali wanakwenda. Ninachosema ni kwamba, wahifadhi wale wamezidiwa na idadi ya tembo. Nakumbuka Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga alishukuru kwa kujengewa kituo pale Milola na kupatiwa Askari na gari jipya, tukafurahi sana, lakini bado Askari wale wamezidiwa. Namomba wapewe chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi tumezawadiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na eneo kubwa lakini lenye rutuba na wananchi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wanaopenda kulima chakula, wakala chakula chao na mazao ya kilimo na mazao ya biashara. Sisi kwa desturi yetu tusingependa kupewa chakula. Mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, anafanya kazi akapata chakula, kwa sababu tunaamini chakula cha kuletewa hakiwezi kukidhi mahitaji ya familia, lakini pia kwetu sisi ni fedheha kuletewa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hali ilivyo, kuna ulazima kabisa Serikali ipeleke chakula. Wananchi hawana chakula, watoto wa shule hawana chakula, na pia hii kadhia ya tembo hii inaathiri hata utendaji wa Wizara nyingine, Wizara ya Kilimo watu hawalimi vizuri; Wizara ya Elimu, watoto hawasomi. Kwa hiyo, naona miaka ijayo 10, 20 au 50 kule tutaendelea kuwa masikini kwa sababu mojawapo ya kumkomboa mwananchi ni elimu. Sasa kama leo mtoto haendi shuleni kwa sababu ya kadhia ya tembo, unategemea tutaendelea kuwa na maisha gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Nasema hili kwa maumivu na uchungu na unyenyekevu mkubwa. Tunaomba huo mkakati wa kurekebisha sheria na sera za uhifadhi ufanyike haraka iwezekanavyo. Tumesikia Kamati wame-suggest hicho kitu, lakini pia tunaomba fidia. Kuna watu walioathirika wale, tunaona kimya tu, hakuna kinachoendelea. Kuna watu wamekufa pale Nungunichile, Namikango, Iyonja, kule Barikiwa na maeneo mengi tu kule Liwale vifo vinaendelea siku kwa siku. Tunaomba fidia zao zifanyike angalau ndugu zao wafute machozi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kufanyike utafiti wa kina kwenye Wizara hii, kwa nini bado kunaendelea? Tulisema kwamba shoroba unapita mahali fulani lakini mbona sasa hivi ng’ombe ndiyo wamehamia kwenye vijiji vyetu kabisa na vijiji vile vilikuwepo miaka yote? Kwa nini sasa hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba ufanyike mkakati mkubwa wa kuondoa wale wanyama.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri afike kule Nachingwea, Liwale, Kilwa na Milola aje aone hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)