Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi, Mwenyezi Mungu akubariki. Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka jitihada kubwa katika Wizara hii ili iendelee kutuongezea mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa mambo yote ambayo ameyafanya kwenye Wizara alikotoka huko, kuhakikisha mpaka Yanga wamefikia hiyo hatua ambayo wameifikia, tunaamini pia ni jitihada zako zimeonekana huko. Yupo msanii mmoja alishawahi kuimba huko nyuma kwamba, “Hiki ni kisiki cha mpingo, wenye shoka wameshindwa, unakuja na panga unajisumbua.”
Sasa tunaamini kwamba Mheshimiwa Waziri, wewe umekuja kwenye hii Wizara yenye kisiki cha mpingo, uje na msumeno ili uweze kutoa hicho kisiki cha migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba tu kuchangia katika maeneo mawili. Moja ni ushauri. Ushauri wangu kwanza niombe Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara nyingine zile ambazo zinaunda ile Kamati ya Mawaziri Nane kwamba tuangalie hata nchi nyingine ambazo zimeendelea, mfano, South Africa wame-specialize kwenye mambo kadhaa. Kwa mfano ukienda Durban ni sehemu inayohusika na viwanda tu. Ukienda Johannesburg ni sehemu ambayo inahusika na biashara na sisi tuangalie kwamba yako baadhi ya maeneo ambapo tutenge maeneo iwe ni special kwa ajili ya wafugaji wetu ili pia mifugo isiingie hifadhini na pia isiwaingilie wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, iko mikoa hapa inajulikana kabisa kwamba ni mikoa ambayo inategemewa na nchi hii kwa ajili ya kuzalisha chakula. Mfano Songea, Iringa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Rukwa, lakini hata Mkoa wa Morogoro. Sasa pia mikoa hii ambapo inaendelea kugubikwa na wafugaji pia tunashindwa hata kuitambua mifugo yetu tuwaweke sehemu moja ili ile azma ya Mheshimiwa Ulega ya kutaka kuwapandia majani sehemu moja, itakuwa ni rahisi kuitambua mifugo hii na tuweze kuwahudumia vizuri lakini itawasaidia sana watu wa maliasili mifugo hii isiendelee kuingia hifadhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi nina maombi hapa kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Momba. Kwa ridhaa yako naomba mhudumu apite aweze kumpelekea Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri sisi watu wa Jimbo la Momba miaka ya 1974 kipindi kile cha Sogea cha Mwalimu Nyerere, wazazi wetu kutoka huko vijijini nikimaanisha babu zetu, waliambiwa watoke kwenye vijiji vya mbali wakae sehemu za karibu ili huduma za kijamii ziweze kuwapata kwa pamoja, kukiwa kuna lengo zuri na wakaachia mapori yao ya kutosha ili wakae kwenye vijiji kwa pamoja waweze kupata huduma za kijamii kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wazazi hawa, babu zetu hawa, waliamua kuachia hayo maeneo kwa nia njema kwa Serikali na maeneo hayo yakawa ni maeneo ya hifadhi. Sasa kipindi hicho cha mwaka 1974, watu hawa walikuwa wanakadiriwa kuwa chini ya watu 20,000. Sasa hivi tunavyoongea kwenye sensa ambayo imefanyika mwaka jana 2022, wananchi wa Jimbo la Momba tuko zaidi ya 270,000. Sasa tumeongezeka, katika vijiji hivyo 72 kuna maeneo machache tu wanaomba wapate kipande kidogo cha ardhi Mheshimiwa Waziri ili waendelee kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu sisi shughuli yetu kubwa ni kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa moyo wa unyenyekevu na uadilifu mkubwa, kwenye Kitongoji cha Kanyara ambacho kijiji chake ni Tontera kwenye Kata ya Chilulumo kwenye Kitongoji cha Mbaro kwenye Kijiji cha Mlomba Kata ya Chitete, kwenye Kitongoji cha Moravian Kijiji cha Itumbula Kata ya Ivuna, kwenye Kitongoji cha Mbao na Chiula kwenye Kijiji cha Ntungwa na Mkomba ambapo Kata yake ni Mkomba. Wananchi hawa wote wamezungukwa na hifadhi. Wananchi hawa wote wamezaliana hawana mahali pa kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba nia ya Serikali ni njema, nia ya Serikali ni nzuri kwamba ni lazima tutunze maeneo yetu ili vizazi na vizazi vije kurithi. Sasa kama msipotaka kutupa hata kipande kidogo cha ardhi, hawa babu zetu ambao waliamua kuyaachia maeneo haya wakaamua ku-sacrifice kwa ajili ya sisi kizazi chetu, tusipopewa sisi tutaenda wapi? Wananchi hawa wasipokumbukwa ili wapate kipande kidogo; na hawaombi ekari 1,000, hawaombi ekari 500, wanaomba ekari chache tu ili waweze kuendelea kuendesha shughuli zao. Mtakapoendelea kutuacha hatuna mahali pa kwenda, sisi tutageuka kuwa watumwa ndani ya ardhi yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoongea miaka 30 iliyopita Bunge lilikuwa kule Msekwa ndiko Wabunge walikuwa wanakaa, lakini baada ya mahitaji kuongezeka sasa hivi tuko mahali hapa. Maana yake kulionekana kuna uhitaji wa kuongezewa Bunge ili kuwe na uwakilishi. Kwa hiyo, sisi mkituweka kwenye kundi la kutufunga kwamba tunatunza kwa ajili ya vizazi vijavyo, maana yake mnakihukumu kizazi cha sasa kwa ajili ya kizazi kinachokuja. Sasa hawa wananchi ambao babu zao waliamua kutunza kwa ajili ya wajukuu zao, baba zetu wamevumilia sasa tumezaliwa kizazi kama hiki cha kwangu. Vijana hawana mahali pa kulima, vijana hawana mahali wanaweza wakajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa dhati ya moyo wangu nikuombe sana sana Mheshimiwa Waziri na ikikupendeza nikuombe sana tunaomba uje ufanye ziara kwenye Jimbo la Momba kwa masikio yako ili angalau uweze kusikia namna ambavyo wananchi hawa wanaendelea kuomba. Tunakuomba sana, tunakuomba mno na kwa unyenyekevu mkubwa, kama ambavyo wananchi wa maeneo mengine wamefurahishwa. Wananchi wa Mara ambavyo Mheshimiwa Rais aliwaona akawakumbuka akaona iko haja ya kurekebisha tena mipaka ya uhifadhi. Hata sisi tunaomba mipaka ya uhifadhi ije irekebishwe ili wananchi hawa kwa moyo wa unyenyekevu waweze kupata sehemu ya kuendesha shughuli zao. Mimi nakuomba sana na ninarudia tena kuomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama bajeti hii itapita sisi hatukupata tena eneo la kulima, hata yale ambayo tulikuwa tumeendelea kuwaahidi wananchi kwamba watapata afadhali, tutaonekana ni waongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)