Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa anavyoendelea kuilea hii Wizara akiwa na matumaini makubwa kwamba ni Wizara ambayo kiukweli ikitendewa haki yake kutokana na wingi wa vivutio tulivyonavyo itaweka mchango mkubwa sana kwenye Pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuona hayo ameendelea kufanya mabadiliko. Utaona amembadilisha Mheshimiwa Mchengerwa na Katibu Mkuu wake wote wameletwa kwenye Wizara hii. Lengo ni kuchochea ufanisi katika Wizara ili Taifa liweze kupata mapato kutokana na hifadhi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa namna alivyoanza kuyatekeleza majukumu yake kwenye Wizara hii, na ninaamini ataiweza. Ni Wizara ngumu lakini ninamfahamu kidogo, nimeweza kukaa nae nikiwa bosi wake kule Pwani, nilikuwa nikimfutilia, naamini ataiweza kazi hii. Kama alivyoweza Wizara ya Michezo sina mashaka naye. Lakini pia ana Naibu Waziri mzuri. Akiweza kumtumia vizuri Naibu Waziri wake ni mwanamke jasiri pia, ni jasiri na utaona hata kwenye matamko yake na yuko serious na kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yake ina changamoto kubwa mbili. Changamoto ya kwanza ni migogoro baini ya hifadhi zake pamoja na vijiji, na changamoto ya pili ni mwingiliano wa wanyama na binadamu. Hizi ni changamoto kubwa ambazo atategemea either zitamsumbua ama Mungu akimjalia akizipatia basi atakuwa ameweza kuitendea haki Wizara hii. Ataweka historia kubwa katika nchi hii, na unaona hata mwelekeo wa bajeti tunavyochangia hakuna ukali sana, kwa sababu tuna matumaini makubwa kwamba amekuja hapo pamoja na Katibu Mkuu wakishirikiana vizuri na Makamishna wale, ni watu wazuri. Wana Bodi nzuri, na kwa kweli wakishirikiana wataitendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifumo ya makusanyo tunaona wanaenda vizuri na tunaona ongezeko la watalii pamoja na fedha katika Taifa letu. Sasa waendelee kuimarisha hivyo ili wampe moyo Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la migogoro ya mipaka mimi nishauri jambo moja. Mheshimiwa Waziri hebu usirithi hii migogoro kwa maana ya historia yake, hebu jaribu make sasa vizuri wewe na cabinet yako yote muanze kuiangalia hii migogoro. Kuna migogoro mingine inaweza ikatatuliwa kwenye ngazi ya mapori yenyewe. Kuna baadhi ya maeneo, mimi nilipata bahati mmeniletea pale swagaswaga kijana Reuben ni kijana mzuri sana kwenye pori la swagaswaga, ni mkuu wa pori lile. Yeye ametumia mfumo wa kushirikisha wananchi katika ku-solve migogoro iliyopo katika eneo lake, na amefanikiwa sana. Ni kwa mara ya kwanza Reuben amekuwa akisifiwa na wananchi wa Kondoa wanaozunguka lile pori kwa sababu kwanza anafikika na anawafikia watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wameweza kutatua mgogoro wa mpaka ambao ulikuwa unataka uzuke kwenye maeneo ya Iyoli, Kingale na Tampori. Wamekuja maafisa ardhi walikotoka hatujajua wametoka wapi? wakaweka mipaka mipya iliyoanza kusababisha taharuki kwa wananchi. Wananchi waliponipigia nikampigia mkuu wa pori Bwana Reuben, amekwenda kwa wananchi wakashirikiana kwenda kuitambua mipaka ya asili na wakaiyona. Jana walikuwa wanashirikiana kuhamisha vile vigingi ambavyo viliwekwa kimakosa kuvirudishia pale, na hivyo mgogoro ule automatically unaondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo nikushauri kwamba hata ile taarifa ya Mawaziri nane usiitegemee sana, sehemu kubwa itakupotosha tu, kwa sababu kiukweli haijafanya kazi kama alivyokusudia Mheshimiwa Rais. Tumia sasa nafasi uliyonayo na nafasi yako wewe kwenda kuijua hii migogoro, utaimaliza kiuraisi kama ulivyoweza kwenda Mara kule kwa watani wetu hawa wakakuelewa, ukija pale Kondoa kwa Warangi watakuelewa tu. Kwa sababu ni watu waele sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro ambao uko pale Mongoroma ambao unasababisha wananchi wanashindwa kufanya kazi zao. Tunauita mgogoro ni kwa sababu tu tunaendelea kukubali kurithi maneno ya migogoro. Lakini hata ukimwagiza Reuben akaenda akaonyeshwa mipaka ambayo wananchi walishirikiana na wale waliyotangulia ataiona na atatoa hivyo vigingi vipya vilivyowekwa atavihamisha wananchi wataendelea na maisha yao. Kuna maeneo kama hilo nalozungumzia kuna wakazi zaidi ya 4,000 wakazi zaidi ya 2,000 wamekaa muda wote wanawajukuu na vitukuu leo kuu-solve mgogoro ule huwezi ukasema uwaondoe wale watu ilhali huna pakuwapeleka. Lakini kama tutafuata maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo alielekeza ile kamati kwamba kama maeneo yenyewe si mazalia ya wanyama na kama maeneo yenyewe si chanzo cha maji na wananchi wameisha kaa muda mrefu kuna haja gani ya kusema kwenda kuwatoa na hauna pakuwapeleka pale? nikuwaacha waendelee kukaa, kateni lile eneo waonyesheni wananchi mipaka yao ili waendelee kuishi na kujenga nyumba nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanashindwa hata kujenga nyumba kwa sababu ya hizo taharuki ambazo zisizo na msingi. Kwa hiyo ninakushauri Mheshimiwa Waziri, ni vema sasa wewe mwenyewe ukimtumia Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watalamu ulionao kwakweli mnaweza mkafanya mambo makubwa na mkaacha hizi hifadhi zikabaki kuwa salama. Hakuna namna leo mtawaweka salama hata askari wetu, kwa sababu leo kama kutakuwa na migogoro kati ya askari wetu wanaolinda kule na wananchi hatutafanikiwa kutunza hifadhi zetu vizuri. Lakini kama wananchi hawa watakuwa sehemu kama wale niliokwambia, wananchi wa Iyoli na Tampori ambao baada ya kuu-solve huo mgogoro sasa wenyewe wamekuwa ni walinzi. Ibaki sasa wananchi wawaombe tu kwamba tunaombeni mtuongezee maeneo halafu iwe ni hiari kwenu kuwapa au kutowapa lakini wawe wanajua haya maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo naweza nikakushauri sasa, ameongea vizuri Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, aliongea vizuri kuhusiana na mfumo za ajira za askari wetu hawa. Pamoja na ule mchango wake mzuri aliyoutoa nikuombe Mheshimiwa Waziri uangalie askari wetu hawa wote, wote askari hawa ni askari wa hifadhi wanasoma chuo kimoja, wanalinda wote tembo, wanalinda simba na mahifadhi yote wanalinda wao. Isije ikatokea sasa kuna taasisi nyingine wanapewa mishahara mikubwa na taasisi nyingine wanapewa mishahara midogo matokeo yake ufanisi unakuwa hakuna. Ndiyo maana unapata vijana ambao wanakwenda swaga ng’ombe za wananchi kwenye hifadhi halafu wanazichukua wanakwenda kuwapiga faini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wanakuwa hawana, kipato chao kinakuwa kidogo; na kama ilivyo kawaida, kwamba wanadamu huwa tuna wivu. Kwamba kwanini wenzetu walipwe kikubwa sisi tulipwe kidogo. hebu fanyeni ku-harmonize watu wote/askari wetu wote walipwe sawa. Makamishna wote wawe sawa katika level hiyo hiyo wote wafanane ili kuwe na ufanisi mzuri na isipatikane askari anaetamani kwenda kwenye taasisi nyinge kutokana na malipo madogo yanayopatikana kwenye taasisi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)