Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili namimi niweze kuchangia kwenye hii Bajeti ya Wizara ya Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wangu kipenzi Dtk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana aliyoifanya kupitia suala la Royal Tour, kiasi ambacho sasa imetoa taswira nyingine kabisa katika nchi yetu ya Tanzania kwenye masuala ya utalii. Nampongeza sana mama yetu huyu kwa sababu amekuwa akijitoa, ni mzalendo wa nchi yetu hii ya Tanzania. Hata nyinyi wenyewe pia Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi nchi imetulia kila kitu kinaenda sawa, uchumi unaendelea kukua, miradi yote inaendelea kutekelezwa, mikubwa na midogo yote inakwenda barabara, heko nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana ya utalii ambaye ni kaka yangu Mohamed Mchengerwa lakini pia na delegation yake yote kwa namna ambavyo wanachapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye matukio ya tembo kuuwa na kujeruhi katika Wilaya ya Tunduru kwa kipindi cha mwaka 2020 mpaka kufikia sasa 2023. Kwa masikitiko makubwa sana naomba niseme kwamba tembo tunawapenda sana, ni rasilimali ya Taifa na wamezaana sana na ni kivutio kikubwa sana kwa watalii. Lakini mimi najiuliza tu, hivi ili mtalii aje amtambue tembo inabidi tembo hao wawe wanasindikizwa na sifa ya maelfu ya tembo wangapi? Kwa sababu tembo hawa wamekithiri wanafika mpaka kwenye makazi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kama ni shambani ukiweka viazi kwenye nyumba wanapenda ile harufu ya viazi wanakuja wanabomoa mpaka nyumba wanachukua viazi wanaenda kuvitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niseme hivi, natoa wazo sasa kwamba ni kwanini Mheshimiwa Waziri hawa tembo tusifikirie kuwavuna baadhi? tunawavuna wapungue kidogo kwa sababu bado wana kizazi waendelee kuzaa. Wale wanaopungua sasa maana yake ni nini, tutaenda kutoa yale meno tutayaweka kwenye Benki yetu ya Taifa ya Rasilimali za Taifa lakini pia nyama zile tutaweza kuuza kwenye mabucha yetu kwa sababu wako watu ambao wanakula. Kwa hiyo hii ni mali kwa mali. Tukiwavuna hadha pia itapungua. Wakati wanaendelea kuzaa basi wanachi wapate hafuweni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba mwaka 2020 katika Wilaya ya Tunduru pamoja na Namtumbo pia watu tisa walikufa na watatu kujeruhiwa; 2021 kufa watu wawili na saba kujeruhiwa, 2022 kufa watu nane na sita kujeruhiwa, 2023 kufa watu sita na sita kujeruhiwa katika Wilaya ya Tunduru tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya watu ambao wamekufa katika Wilaya ya Tunduru tangu mwaka 2020 mpaka 2023 walikuwa ni watu 25 na waliyojeruhiwa ni watu kumi saba, ni watu wengi sana, rasilimali ya nchi hii inapotea. Hata hivyo endapo kama wanapata majeraha na kufa bado inaonekana kwamba mnyama anathamani zaidi kuliko binadamu. Sasa hebu tuondoke kwenye hiyo adha. Kama kuna kanuni au sheria inatakiwa irekebishwe kwa mustakabali huo kwa maana yaku-balance binadamu na wanyama basi mimi nataka niseme hivi sheria hiyo iletwe hapa Bungeni ili tuirekebishe. Na kimsingi hauwezi kulinganisha mnyama na binadamu hasilani abadani haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niseme kwamba fidia inayotolewa kwa mwananchi akiuwa ni shilingi laki moja tofauti na thamani ya binadamu lakini pia mwananchi aendapo kama ataliwa mazao yake fidia anayopewa ni shilingi laki mbili, laki moja mpaka laki tano. Mwisho huyo anakuwa amefilisika kabisa na wameona kwamba hili shamba ni kubwa wanaona aibu hata kumwambia kwamba haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye migogoro ya vijiji ambavyo vinazungukwa na wanyamapori. Nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kushughulikia migogoro hii. Kwamba sasa hivi punde nimesikia kuna taasisi au nchi imetoa fedha takriban bilioni 149 hivi kwa jili ya kusaidia mikoa ambayo inakutana na changamoto hiyo ya kuvamiwa na kushughulikiwa na wanyamapori. Kwa hiyo changamoto za wakulima na hifadhi za wanyamapori imekuwa ni kubwa kiasi ambacho sasa ameona kwamba atafute fedha kwa ajili ya kwenda kushughulikia changamoto hizo. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, na niombe Wizara ifanye vizuri sana kwa ajili ya kumpa sapoti Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye suala ambalo kimsingi nataka niliseme, linahusiana na suala la kauli, lugha mbaya kwa wananchi. Kabla sijalisema hilo naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa, Mheshimiwa Mchengerwa anafanya kazi nzuri sana. Tunamsemea hapa vizuri kwa sababu you deserve the best, unafanya vizuri kabisa si, kwamba unapendelewa, sifa hiyo unastahili. Kwakweli unafanyakazi nzuri; na wengine wamesema ulitoka kwenye michezo, ulitoka kwenye utumishi kote huko umefanya vizuri umeacha alama. Sasa hivi uko maliasili na utalii tunategemea kwamba Wizara hii sasa inakwenda kuchanja mbuga na kuleta matokeo chanya katika nchi yetu hii ya Tanzania. Hongera sana nikutie moyo, endelea kufanya kazi na sisi kama kuna jambo lolote la kukusaidia ndani ya Bunge hili lilete tukusaidie, tuchakate ili kazi iweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia kwa namna ambavyo amekuwa akitatua migogoro anatatua migogoro kidiplomasia, anakwenda site anazungumza na wananchi. Mwananchi hata kama alikuwa ana-burden gani anajikuta kabisa anacheka, anafurahi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mchengerwa akiwa Wilaya ya Mbarali ambako kulitokea changamoto, ameondoka kule wananchi wanafuraha sana; endelea kufanya hivyo Mheshimiwa Mchengerwa. Lakini pia nimesikia amekwenda kule Tarime Vijijini, nako amefanya vizuri, tumeoa clip zake na ambavyo anaongea na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Mchengerwa anafahamu kwamba ili sisi tukae humu ndani ya jumba hili ni lazima wananchi wapige kura kumchagua Mheshimiwa Rais, kuwachagua Wabunge, kuwachagua Madiwani na hata Wenyeviti wa Vitongoji anafanyakazi nzuri. Lakini wako wengine wanasahau kwamba ili kukaa humu ndani basi hakuna haja ya kutambua hivyo vitu. Ni muda mfupi sana jamani, tusisahau, na ni muda mfupi sana wa kukaa humu baadaye tunatoka kwenda kuomba kura kule. Sasa kama hatutambui umuhimu wa wale wananchi maana yake mwisho wa siku tutakwenda kule na tutarushiwa mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja kwa masikitiko makubwa sana. Leo hii niseme kwamba nilikuwa nategemea Wizara hii inapokuja na bajeti yake basi Naibu Waziri wa Maliasili awe alishakwenda kule Tarime Vijijini ameomba msamaha kwa wale wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetembea clip yake nchi nzima ambayo ilikuwa na maneno, ambayo siyo mazuri, siyo maneno ya kiungwana, maneno ambayo kiukweli hayana mahusiano mazuri na wananchi yanachonganisha baina ya Serikali na wananchi, ni maneno ya udhalilishaji kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niseme ni maneno ya udhalilishaji kwa wananchi. Huwezi kwenda kuwaambia wananchi eti kwamba mnageuza huko porini ni sehemu ya kwenda kujisaidia, hapana siyo sawa. Kwa sababu hawa wananchi maana yake ni nini? Hawajui suala la usafi, hawana vyoo, hawajawahi kujenga vyoo. Naomba kupitia Bunge lako Tukufu huyu Mheshimiwa Naibu Waziri aende kuomba msamaha, sisi kama wananwake wenzake tunaksikia aibu kuongea maneno ya udhalilishaji kama yale kwa wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana aende akaombe msamaha kwa wananchi wale ambao alitumia kauli mbaya kuwajibu, wale ni wananchi wa Tanzania. Tunawategemea kwa kazi alizofanya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anastahili apewe kura zote 100% badala…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi muda wako umekwisha.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, umesahau, kwa hiyo naomba sekunde moja tu. Kwa hiyo sasa nataka mimi nitashika shilingi kwenye eneo hili endapo kama Naibu Waziri hataomba msamaha hapa wakati tuna - wind up, aombe msamaha kwa wananchi wale kwa kile ambacho aliwatendea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)