Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna anavyotafuta fursa za utalii na kuongeza utalii katika nchi yetu. Hongera sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako, Naibu Waziri kwa kazi ambazo mnafanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Wizara hii inaendelea kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana ambayo nataka nichangie leo. Mheshimiwa Waziri ulichokifanya Tarime sasa ni muda muafaka wa kuja kufanya vilevile kuwasikiliza wananchi wa Busega na wananchi wa Magu. Tuna Pori la Sayaka, umefanya kitu kikubwa sana pale Tarime, namna ulivyowasikiliza wananchi kwa kweli uliwapa faraja kubwa sana. Leo wananchi wa Busega na Magu wanataka waje wakusikilize, uwasikilize katika Pori la Sayaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Busega kwa maana ya Kata ya Nyaluhande kuna Kijiji kinaitwa Nyaluhande, Mamkala pamoja na Mwagindi. Vijiji hivi vilikuwa vinanufaika na sehemu ya eneo ambalo sasa limetafsirika kuwa ni pori. Wameendelea kulitumia zaidi ya miaka 40, wamelima zaidi ya miaka 40 maeneo yale, lakini sasa wamekuja kunyang’anywa na kuyafanya mapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na pori, na tunatamani na tuko tayari sisi wananchi wa Busega kufanya uhifadhi, kuhakikisha kwamba, mapori yanalindwa na hili pori lilindwe. Hata hivyo, kuna eneo la mita 840 wananchi wetu wamekuwa wakilihitaji siku zote, wamekuwa wakilitumia katika kazi ya kilimo, lakini sasa hawawezi kulitumia. Hivi karibuni viongozi wanawaambia limeni kwa mwaka huu, mwakani msilime, ufugaji nao umekuwa shida, wakipeleka mifugo wanakamatwa, wanataifishwa na wengine kuuzwa. Sasa ni wakati muafaka Mheshimiwa mchengerwa uje sasa uwasikilize wananchi wa jimbo la Busega na Magu, ili tuweze kujadili tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi hapa nilikuwa nasikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika suala zima la migogoro. Amezungumza pia kwamba migogoro inaongezeka kwa sababu pia wananchi wameongezeka. Nikawa najiuliza swali la kawaida kabisa, ni lini wananchi watapungua? Jibu unapata, hapana, hawatapungua kwa sababu tunaongezeka kila siku. Ukiangalia hata Sensa ya 2012, tulikuwa wananchi milioni 44, Sensa ya 2022 tuko milioni 61.7. Maana yake ni kwamba tumeongezeka kuwa watu 35 katika 1,000. Nini maana yake? kila mwaka wanaongezeka asilimia asilimia tatu. Sasa asilimia tatu ya milioni 61.7 maana yake katika miaka inayofuata kila mwaka watakuwa wanaongezeka watu milioni moja na laki nane. Sasa watu milioni moja na laki nane kwa miaka kumi ijayo tunategemea wataongezeka kuanzia milioni 15 mpaka milioni 20. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake? Mwaka 2032 tunategemea kuwa na watu milioni 75 mpaka milioni 80. Hii ni hesabu ya kawaida, haihitaji nguvu nyingi, inafahamika kulingana na sensa tuliyonayo na birth rate ya asilimia tatu ambayo imeonekana katika sensa ya mwaka 2022. Sasa mje na mpango kwa sababu watu hawatapungua. Njooni na mpango wa nini kifanyike kupunguza migogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itakuwa watu wanavyoongezeka na migogoro inaongezeka, maana yake wataongezeka 2023, 2024, na hata migogoro itaongezeka. Ni lazima sasa mje na mpango, ni kwa namna gani watu wataongezeka, lakini migogoro ipungue. Hiyo ndiyo mjenayo ili mweze kuona namna ya kutatua. Mkae Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI, mje na mpango wa pamoja ili mweze kutusaidia kuhakikisha kwamba wananchi wetu waweze kupata nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza hapa ni suala la tembo na viboko. Sasa hivi limejitokeza la fisi, hususan katika moja ya kata huko Wilayani kwangu. Sasa ni wakati muafaka wa kuvuna baadhi ya viboko ili wananchi wetu waweze kupata nafuu, pale Jimboni Busega watu wamekufa, mwaka 2022 zaidi ya watu watatu wamekufa kwa sababu ya viboko. Ni wakati muafaka sasa mje mwavune ili wananchi wawe na amani katika yale mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa kufanya research. Mfanye tu reseach kwa nini hili? Moja ya majibu mtakayoyapata ni kwamba wamezaliana sana. Watu tunaongezeka na wanyama wanazaliana. Sasa ifike muafaka wanyama tuwapunguze kwa sababu si hatujawatolea uzazi, kwa hiyo, tutakapowapunguza, wachache wataendelea kuzaliana. Kwa hiyo, watakapokuwa wanazaliana, wengine tunawapunguza. Tusipofanya hivyo, maana yake tatizo litaendelea kuwa kubwa, watu watakufa, watu watauawa na pia migogoro itaongezeka. Ni lazima pia baadhi ya wanyama kwa mfano tembo na viboko tuone namna ya kuwapunguza ili tuweze kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kuchangia hapa ni juu ya watalii na matumizi ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Ukiangalia katika hali ya kawaida kutoka pale Mwanza kwenda Serengeti kwa maana ya lile geti ambalo liko pale Lamadi, ni kilometa chache, nafikiri ni kilometa 120. Sasa hapo ni karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwekeze katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili watalii wengine waanze sasa kushukia pia Mwanza ili nasi huku upande wa Kanda ya Ziwa tuweze kupata watalii. Watalii wataingilia huku kwenye geti la Serengeti ambalo liko Lamadi na wananchi wangu wa Lamadi na wenyewe watapata vipato kutokana na watalii watakaopita maeneo haya.nini maana yake? Watu watajenga hoteli, watapata ajira ambayo itatokana na watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ndugu yangu hapa Mheshimiwa Boniventura Kiswaga na wenyewe watajenga pale hoteli. Kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mabula, hapa katikati nao watakuwa na hoteli pale. Hii itasaidia sana watalii wetu sasa kuongeza kipato katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la mwisho, limezungumzwa hapa suala la Nyatwali. Kuna wananchi wangu ambao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)