Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya kwenye Wizara hii yeye pamoja na Naibu Waziri. Mko vizuri, chapeni kazi, Mheshimiwa Rais amewaamini na sisi wenzenu tunawaombea mweze kutimiza matarajio ya wananchi na matarajio ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni mhifadhi pia kwenye eneo letu, anatusaidia sana kutunza mazingira pale. Huyu mtu bingwa, Nurdin Babu tunamshukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, mtu bingwa, Amiri Mkalipa, kwa kazi kubwa anayoifanya pale Hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niseme hapa kidogo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kubuni na kuja na Royal Tour, imebadilisha maisha yetu kwa kiwango kikubwa. Nami nitasema kwa sababu, kama ni mnufaika namba moja, wote mnakumbuka Mheshimiwa Rais alipotoka huko alishukia pale Hai, Uwanja wetu wa KIA. Sasa nataka niwaeleze mambo tunayojifunza na yaliyopatikana kutokana na filamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 watalii waliokuwa wanashuka pale KIA walikuwa ni 354,000, hiyo ni mwaka 2021. Leo mwezi Aprili, watalii ambao wanashuka pale Uwanja wa KIA uliopo Jimbo la Hai ni 728,000. Hayo ni mabadiliko makubwa sana, lakini ndege zinapishana. Leo unaambiwa KLM wanatua pale mara sita kwa wiki na ndege nyingine zinaendelea kuja. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa aliyoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia na wewe Waziri nikushukuru, wananchi wa Hai wanasema ahsante. Nimepiga kelele hapa kuhusu CSR, nimeambiwa tayari mmetupelekea fedha pale Shule ya Mure iliyoko Nuni kwa ajili ya kufanya ukarabati wa majengo, Shule ya Mkoeshoo iliyoko Mkuu, lakini shule ya Kiarasa iliyoko kule Sawe, Shule ya Mkweseko na shule iliyoko kule Foo, lakini pia pale Lukani mnafanya Mradi wa gesi. Tunawashukuru sana kwa kusikia maombi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri. Nimekuwa nikisema hapa, tunazungumza utalii, tunazungumza Mlima Kilimanjaro, namwomba sana Waziri, natamani kuona huku ameweka fedha kwa ajili ya kupanda miti Kilimanjaro. Hii mnayosema wanaleta wadau, wanaleta wanapanda, lakini hakuna mechanism ya kuitunza. Hata sisi tunapanda sana miti kule, lakini mechanism ya kuhakikisha miti hii inapona, haipo. Hizi idadi unazozitaja kwenye hotuba zako Mheshimiwa Waziri, tukienda kukagua iliyopandwa na iliyopona ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, naombe kwa kweli kwenye bajeti yako utakapokuja kuhitumisha hapa, utuambie bajeti uliyoipanga ya kupanda miti na kuhakikisha miti hiyo inapona. Nakuomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni sambamba na lile la vibali. Niliuliza swali hapa jana, miti inakatwa kwa kiwango kikubwa sana. Ni kweli zipo zile kamati zinazohusika na utoaji kwa mwongozo ule wa mwaka 2017, lakini Wenyeviti hawashirikishwi. Ile barua inayoandikwa ya anayeomba kibali anapitisha kwa Mtendaji wa Kijiji, anapitisha, inaenda kwa Mkuu wa Wilaya anakaa na timu yake, inarudi. Ninachoshauri, Ward DC wote, Diwani na viongozi wote washiriki kwenye maombi yale, ikirudi Mkutano Mkuu wa Kijiji ushiriki. Tumeona mazingira yanavyoharibika. Nimesema pale Uswaa miti inakatwa, Bonde lile la Weruweru miti imekwisha. Naomba sana hili ulichukulie kwa umakini wake mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tuimarishe mifumo ya watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro. Moja, nimekuomba kufungua ile barabara mpya. Nadhani Mheshimiwa Waziri umenielewa na umesema timu yako ikafungue barabara ile tuwe na barabara nyingi, lakini kuna jambo, watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro isiwe ni adhabu, iwe ni watu wanaenda kwenye furaha. Naomba mageti yote mkubali kutolewe vibali, watu wajenge hoteli ili mtu anayetaka kupanda mlima, akichoka apumzike, aendelee na safari kuliko ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na malalamiko kwa wale wanaopandisha mlima. Sasa hivi wametangaziwa kuanzia mwezi wa Saba kwamba kila mtalii anayepanda lazima afanye booking kwa siku saba, kitu ambacho siyo sawa. Watu walishafanya booking kwa siku tano. Kingine ambacho kinafanyika, mtalii akifanya booking kwa siku sita, ikatokea hapo katikati ameumwa akashindwa kuendelea na safari, akija ku-resume tena anaongezewa siku. Kwa hiyo, burden inabaki kwa wale wapandisha mlima. Naomba sana na hili ukatazame, linarudisha nyuma maendeleo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ninaloliomba, watalii wanapanda Mlima Kilimanjaro, umesikia hapa hakuna Mbunge wa Kilimanjaro anayezungumza kuhusu mgogoro, tunaishi vizuri na watu wa KINAPA. Kwa nini? Kwa sababu, tunaendanao na CSR mmetuletea, lakini vijana wa Hai hawapati kazi hizi Mheshimiwa Waziri. Kampuni ya Utalii inatoka Arusha inakuja na watu wake, tumeshasema hapa, naomba na wewe utusaidie kusimamia hili. Vijana wa Hai wako tayari kufanya kazi hii na tumeshatengeneza umoja wetu, tumetengeneza kikundi, kama wanaopandisha mlima ni watu saba, basi waje na watu watatu, wanne wachukuliwe pale Hai ili vijana wapate kazi. Hii ni kuongeza sense of ownership, hili tunalizungumza mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikwambie leo, Wilaya ya Hai ina vivutio vingi, nami nakukaribisha, usije kwa haraka haraka. Kwanza ukija Wilaya ya Hai unakuja kujifunza namna ya kuondoa migogoro maeneo mengine, maana pale hatuna migogoro. Pili, ukija kuna vivutio vingi, njoo ukae hata siku tatu. Pale tuna daraja linaitwa Daraja la Mungu, halipo sehemu nyingine, liko Hai. Tuna maporomoko ya maji kule Kihori, Mshara, Mpeseko, na tuna kituo chetu cha maji ya tofauti. Nmekuwa nakitangaza mara kwa mara, nawe Mheshimiwa Waziri ufike pale. Tuna samaki wanafanya massage, maji mazuri yako pale Chemka, lakini watu wanaanza kukigombania. Watu wa Arusha Tech ambao wanajenga chuo pale nao wanakitaka, watu wa Pangani nao wanakitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea na Mheshimiwa Mabula hapa, Waziri wa Ardhi ameshanikubalia. Lile eneo litengwe liwe la Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili tukusanye mapato pale na tukitunze kwa sababu ni cha kwetu na bahati mbaya sana ni eneo letu la kimila, haliwezi kuchukuliwa na watu wa maeneo mengine. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kusimamia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, mimi nishauri jambo, kwenye hii migogoro inayozungumzwa hapa, Waziri umeingia kwenye hii Wizara. Huko ulikotoka, umefanya vizuri sana, hebu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Saashisha Elinikiyo Mafuwe kwa mchango wako.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.